Waamuzi 12:1-7
Waamuzi 12:1-7 NENO
Watu wa Efraimu wakaita majeshi yao, wakavuka kwenda Zafoni. Wakamwambia Yefta, “Kwa nini mmeenda kupigana na Waamoni bila kutuita ili twende pamoja nawe? Basi tutaichoma moto nyumba yako, pamoja nawe ukiwa ndani yake.” Yefta akajibu, “Mimi na watu wangu tulikuwa na ugomvi mkubwa na Waamoni. Ingawa niliwaita, hamkuniokoa kutoka mkono wao. Nilipoona kuwa hamniokoi, nikauhatarisha uhai wangu, nikavuka kupigana na Waamoni. Naye BWANA akanipatia ushindi dhidi yao. Sasa kwa nini mnanijia leo ili kupigana nami?” Ndipo Yefta akakusanya wanaume wa Gileadi pamoja na kupigana na Efraimu. Wagileadi wakawashinda Waefraimu, kwa kuwa Waefraimu walisema, “Ninyi Wagileadi ni waasi mliotoroka toka Efraimu na Manase.” Wagileadi wakaviteka vivuko vya Mto Yordani kuelekea Efraimu. Kisha ilikuwa yeyote aliyenusurika kutoka Efraimu aliposema, “Niache nivuke,” hao wanaume wa Gileadi walimuuliza, “Je wewe ni Mwefraimu?” Akijibu “Hapana,” walimwambia, “Sawa, sema ‘Shibolethi’.” Iwapo alitamka, “Sibolethi”, kwa sababu hakuweza kutamka hilo neno sawasawa, walimkamata na kumuua hapo kwenye vivuko vya Mto Yordani. Waefraimu elfu arobaini na mbili waliuawa wakati huo. Yefta akawa mwamuzi wa Waisraeli kwa muda wa miaka sita. Kisha Yefta akafa, akazikwa katika mmoja wa miji ya Gileadi.