Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Wagalatia 5:7-26

Wagalatia 5:7-26 SRUV

Mlikuwa mkipiga mbio vizuri; ni nani aliyewazuia msiitii kweli? Kushawishi huku hakukutoka kwake yeye anayewaita ninyi. Chachu kidogo huchachua donge zima. Nina matumaini kwenu katika Bwana, ya kwamba hamtakuwa na nia ya namna nyingine. Lakini yeye anayewasumbua atachukua hukumu yake, awaye yote. Nami, ndugu zangu ikiwa ninahubiri habari ya kutahiriwa, kwa nini ningali ninaudhiwa? Kwa kufanya hivyo kikwazo cha msalaba kimeondolewa! Laiti hao wanaowatia mashaka wangejikata nafsi zao! Maana ninyi, ndugu, mliitwa mpate uhuru; lakini uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo. Maana torati yote imetimilika katika neno moja, nalo ni hili, Umpende jirani yako kama nafsi yako. Lakini mkiumana na kulana, angalieni msije mkaangamizana. Basi nasema, Nendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka. Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria. Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, mafarakano, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu. Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria. Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake. Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho. Tusijisifu bure, tukichokozana na kuhusudiana.