Wagalatia 5:7-26
Wagalatia 5:7-26 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenendo wenu ulikuwa mzuri! Nani, basi, aliyewazuia kuuzingatia ukweli? Aliyesababisha hali hiyo si Mungu ambaye amewaiteni. “Chachu kidogo tu huchachusha donge lote la unga!” Kutokana na kuungana kwetu na Bwana, nina tumaini kubwa kwamba nyinyi hamtakuwa na msimamo tofauti nami. Tena yeyote huyo anayewavurugeni – awe nani au nani – hakika ataadhibiwa. Na kwa upande wangu, ndugu zangu, kama bado ninahubiri kwamba kutahiriwa ni lazima, kwa nini basi, bado ninadhulumiwa? Kama ingalikuwa hivyo, mahubiri yangu juu ya msalaba wa Kristo yasingalileta aibu yoyote. Laiti hao wanaowavurugeni wangejihasi wenyewe! Nyinyi ndugu, mliitwa muwe watu huru. Lakini uhuru huo usiwe kisingizio cha kutawaliwa na tamaa za kidunia; ila mnapaswa kutumikiana kwa upendo. Maana sheria yote hutimizwa katika kushika amri hii moja: “Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.” Lakini ikiwa mtaumana na kutafunana kama wanyama, jihadharini msije mkaangamizana wenyewe kwa wenyewe! Basi, nasema hivi: Mwenendo wenu na uongozwe na Roho, nanyi hamtafuata tena tamaa za kidunia. Maana, tamaa za kidunia hupingana na matakwa ya roho; na matakwa ya Roho hupingana na tamaa za kidunia. Mambo hayo mawili hayaafikiani; kwa sababu hiyo hamwezi kufanya yale mnayotaka nyinyi wenyewe. Kama mkiongozwa na Roho, basi, hamko tena chini ya sheria. Basi, matendo ya kidunia yanajulikana: Uzinzi, uasherati, ufisadi; kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, choyo, mabishano, mafarakano; husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine kama hayo. Nawaambieni tena kama nilivyokwisha sema: Watu wanaotenda mambo hayo hawataupata ufalme wa Mungu uwe wao. Lakini matokeo ya kuongozwa na Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Hakuna sheria inayoweza kupinga mambo hayo. Wale walio na Kristo wameisulubisha hali yao ya kidunia pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake. Tukiishi kwa msaada wa Roho, na tuufuate mwongozo wake. Basi, tusijivune, tusichokozane wala kuoneana wivu.
Wagalatia 5:7-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mlikuwa mkipiga mbio vizuri; ni nani aliyewazuia msiitii kweli? Kushawishi huku hakukutoka kwake yeye anayewaita ninyi. Chachu kidogo huchachua donge zima. Nina matumaini kwenu katika Bwana, ya kwamba hamtakuwa na nia ya namna nyingine. Lakini yeye anayewasumbua atachukua hukumu yake, awaye yote. Nami, ndugu zangu ikiwa ninahubiri habari ya kutahiriwa, kwa nini ningali ninaudhiwa? Kwa kufanya hivyo kikwazo cha msalaba kimeondolewa! Laiti hao wanaowatia mashaka wangejikata nafsi zao! Maana ninyi, ndugu, mliitwa mpate uhuru; lakini uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo. Maana torati yote imetimilika katika neno moja, nalo ni hili, Umpende jirani yako kama nafsi yako. Lakini mkiumana na kulana, angalieni msije mkaangamizana. Basi nasema, Nendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka. Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria. Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, mafarakano, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu. Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria. Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake. Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho. Tusijisifu bure, tukichokozana na kuhusudiana.
Wagalatia 5:7-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mlikuwa mkipiga mbio vizuri; ni nani aliyewazuia msiitii kweli? Kushawishi huku hakukutoka kwake yeye anayewaita ninyi. Chachu kidogo huchachua donge zima. Nina matumaini kwenu katika Bwana, ya kwamba hamtakuwa na nia ya namna nyingine. Lakini yeye anayewafadhaisha atachukua hukumu yake, awaye yote. Nami, ndugu zangu ikiwa ninahubiri habari ya kutahiriwa, kwa nini ningali ninaudhiwa? Hapo kwazo la msalaba limebatilika! Laiti hao wanaowatia mashaka wangejikata nafsi zao! Maana ninyi, ndugu, mliitwa mpate uhuru; lakini uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo. Maana torati yote imetimilika katika neno moja, nalo ni hili, Umpende jirani yako kama nafsi yako. Lakini mkiumana na kulana, angalieni msije mkaangamizana. Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka. Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria. Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu. Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria. Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake. Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho. Tusijisifu bure, tukichokozana na kuhusudiana.
Wagalatia 5:7-26 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mlikuwa mkipiga mbio vizuri. Ni nani aliyewazuia msiitii kweli? Ushawishi kama huo haukutoka kwa yule anayewaita. “Chachu kidogo huchachua donge zima.” Nina hakika katika Bwana kwamba hamtakuwa na msimamo mwingine. Mtu anayewachanganya anastahili adhabu, hata awe nani. Lakini ndugu zangu, kama mimi bado ninahubiri kuhusu kutahiriwa, kwa nini bado ninateswa? Katika hiyo hali basi, kwazo la msalaba limeondolewa. Laiti hao wanaowavuruga wangejihasi wao wenyewe! Ndugu zangu, ninyi mliitwa ili mwe huru, hivyo msitumie uhuru wenu kama fursa ya kufuata tamaa za mwili, bali tumikianeni ninyi kwa ninyi kwa upendo. Kwa maana sheria yote hukamilika katika amri moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.” Lakini mkiumana na kutafunana, angalieni msije mkaangamizana. Kwa hiyo nasema, nendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa maana mwili hutamani yale yaliyo kinyume na Roho, naye Roho hutamani yale yaliyo kinyume na mwili. Roho na mwili hupingana na kwa sababu hiyo hamwezi kufanya mnayotaka. Lakini mkiongozwa na Roho, hamko chini ya sheria. Basi matendo ya mwili ni dhahiri, nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi, kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi ufalme wa Mungu. Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria. Wote walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili na shauku zake pamoja na tamaa zake. Kwa kuwa tunaishi kwa Roho, basi, tuenende kwa Roho. Tusijisifu bure, tukichokozana na kuoneana wivu.