Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 14:19-31

Kutoka 14:19-31 SRUV

Kisha malaika wa Mungu, aliyetangulia mbele ya jeshi la Israeli, akaondoka akaenda nyuma yao; na ile nguzo ya wingu ikaondoka hapo mbele yao, ikasimama nyuma yao; ikawa katikati ya jeshi la Misri na jeshi la Israeli; napo palikuwa na lile wingu na lile giza, lakini lilitoa nuru wakati wa usiku; na hawa hawakuwakaribia hawa usiku kucha. Musa; akanyosha mkono wake juu ya bahari; BWANA akaifanya bahari irudi nyuma kwa upepo wa nguvu utokao mashariki, usiku kucha, akaifanya bahari kuwa nchi kavu, maji yakagawanyika. Wana wa Israeli wakaenda ndani wakipita kwenye nchi kavu ndani ya bahari; huku maji yakiwa ukuta kwao mkono wa kulia na mkono wa kushoto. Na wale Wamisri wakawafuata, wakaingia ndani kati ya bahari, farasi wote wa Farao, na magari yake, na wapanda farasi wake. Ikawa katika zamu ya alfajiri, BWANA akalichungulia jeshi la Wamisri katika ile nguzo ya moto na ya wingu, akalifadhaisha jeshi la Wamisri. Akayakwamisha magurudumu ya magari yao, hata yakaenda kwa shida; na Wamisri wakasema, Na tuwakimbieni Waisraeli; kwa kuwa BWANA anawapigania. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako juu ya bahari, ili maji yarudi tena juu ya Wamisri, juu ya magari yao, na juu ya farasi wao. Musa akaunyosha mkono wake juu ya bahari, na kulipopambazuka, bahari ikarudi kwa nguvu zake; Wamisri wakajaribu kuyakimbia maji na BWANA akawaangamiza hao Wamisri katika bahari. Yale maji yakarudi yakafunikiza magari na wapanda farasi, hata jeshi lote la Farao lililoingia katika bahari nyuma yao; hakusalia hata mtu mmoja. Lakini wana wa Israeli wakaenda katika nchi kavu katikati ya bahari; na hayo maji yalikuwa ni kuta upande wao wa kulia, na upande wao wa kushoto. Ndivyo BWANA alivyowaokoa Israeli siku ile mikononi mwa Wamisri; Waisraeli wakawaona Wamisri ufuoni mwa bahari, wamekufa. Israeli akaiona ile kazi kubwa aliyoifanya BWANA juu ya Wamisri, ndipo hao watu wakamcha BWANA, wakamwamini BWANA, na Musa mtumishi wake.

Soma Kutoka 14

Video ya Kutoka 14:19-31