Kutoka 14:19-31
Kutoka 14:19-31 NENO
Ndipo malaika wa Mungu, aliyekuwa akisafiri mbele ya jeshi la Israeli, akaondoka akakaa nyuma yao. Pia ile nguzo ya wingu ikaondoka hapo mbele yao na kusimama nyuma, ikakaa kati ya majeshi ya Misri na Israeli. Usiku kucha wingu likaleta giza upande mmoja na nuru kwa upande mwingine, kwa hiyo hakuna aliyemkaribia mwenzake usiku kucha. Ndipo Musa akanyoosha mkono wake juu ya bahari, naye BWANA akayasukuma maji ya bahari nyuma kwa upepo mkali wa mashariki usiku ule wote na kupafanya nchi kavu. Maji yakagawanyika, nao Waisraeli wakapita baharini mahali pakavu, maji yakiwa ukuta upande wao wa kuume na upande wao wa kushoto. Wamisri wakawafuatia ndani ya bahari, pamoja na farasi wote wa Farao, magari ya vita na wapanda farasi. Kukaribia mapambazuko, BWANA akaliangalia jeshi la Wamisri kutoka ile nguzo ya moto na ya wingu, akalifadhaisha. Mungu akayaondoa magurudumu ya magari yao ya vita, kwa hivyo wakayaendesha kwa shida. Nao Wamisri wakasema, “Tuachane na Waisraeli! BWANA anawapigania dhidi ya Misri.” Ndipo BWANA akamwambia Musa, “Nyoosha mkono wako juu ya bahari ili maji yarudi yawafunike Wamisri, magari yao ya vita, na wapanda farasi wao.” Musa akanyoosha mkono wake juu ya bahari, kulipopambazuka bahari ikarudi mahali pake. Wamisri wakajaribu kuyakimbia maji, lakini BWANA akawasukumia ndani ya bahari. Maji yakarudiana na kuyafunika magari ya vita na wapanda farasi pamoja na jeshi lote la Farao lililokuwa limewafuata Waisraeli ndani ya bahari. Hakuna hata mmoja wao aliyenusurika. Lakini Waisraeli wakapita baharini mahali pakavu, ukiwepo ukuta wa maji upande wao wa kuume na upande wao wa kushoto. Siku ile BWANA akawaokoa Waisraeli kutoka mikononi mwa Wamisri, nao Waisraeli wakawaona Wamisri wamelala ufuoni mwa bahari wakiwa wamekufa. Basi Waisraeli walipoona uwezo mkubwa BWANA aliodhihirisha dhidi ya Wamisri, watu wakamwogopa BWANA na wakaweka tumaini lao kwake na kwa Musa mtumishi wake.