1 Samweli 14:1-15
1 Samweli 14:1-15 SRUV
Basi ikatukia siku moja, ya kwamba Yonathani, mwana wa Sauli, akamwambia yule kijana aliyembebea silaha zake, Haya! Na tuvuke twende kwa Wafilisti ngomeni, pale ng'ambo ya pili. Lakini hakumwarifu babaye. Naye Sauli alikuwa akikaa katika Viunga vya Gibea, chini ya mkomamanga uliokuwa kwenye uwanja huko Migroni; na hao watu waliokuwa pamoja naye walikuwa watu mia sita; pamoja na Ahiya, mwana wa Ahitubu nduguye Ikabodi, mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa BWANA huko Shilo, aliyevaa naivera. Tena hao watu hawakujua ya kwamba Yonathani ameondoka. Na katikati ya mapito, ambayo Yonathani alitaka kuipitia ili kuifikia hiyo ngome ya Wafilisti, palikuwa na kilima cha mwamba upande huu, na kilima cha mwamba upande huu; kimoja kiliitwa Bosesi, na cha pili Sene. Hicho kilima kimoja kimesimama upande wa kaskazini, mbele ya Mikmashi, na hicho cha pili upande wa kusini, mbele ya Geba. Basi, Yonathani akamwambia yule kijana aliyembebea silaha zake, Haya! Na twende tukavuke ngomeni mwa hao wasiotahiriwa; yamkini BWANA atatutendea kazi; kwa maana hakuna la kumzuia BWANA asiokoe, kama ni kwa wengi au kama ni kwa wachache. Naye huyo mbebaji silaha akamjibu, Fanya yote yaliyomo moyoni mwako; angalia, mimi hapa ni pamoja nawe, moyo wangu ni kama moyo wako. Ndipo Yonathani akasema, Tazama, sisi tutavuka kwa watu hawa, na kujidhihirisha kwao. Nao wakituambia hivi, Ngojeni, hadi sisi tuwafikie; ndipo tusimame pale pale mahali petu, tusiwaendee. Lakini wakisema hivi, Haya! Ninyi, njoni; hapo ndipo tutakapoenda; kwa maana BWANA amewatia mikononi mwetu; na hii itakuwa ndiyo ishara kwetu. Basi, hao wote wawili wakajidhihirisha mbele ya ngome ya Wafilisti, na wale Wafilisti wakasema, Kumbe! Wale Waebrania wanatoka katika mashimo walimojificha! Nao watu wa ngomeni wakamjibu Yonathani na mbebaji silaha zake, wakasema, Haya! Ninyi, pandeni juu hapa tulipo, na sisi tutawaonesha jambo. Yonathani akamwambia yule aliyezichukua silaha, Haya! Panda nyuma yangu; kwa kuwa BWANA amewatia mikononi mwa Israeli. Basi Yonathani akapanda kwa mikono na miguu yake, na mbebaji silaha nyuma yake; na hao watu wakaanguka mbele ya Yonathani; na huyo mbemba silaha zake akawaua akiwa nyuma yake. Na uuaji huo wa kwanza walioufanya Yonathani na mchukua silaha zake, ulikuwa kama watu ishirini, katika eneo la kama nusu ya kiwanja kiwezacho kulimwa katika siku nzima. Kukawa na tetemeko katika kambi, na katika mashamba, na katikati ya watu wote; watu wa ngomeni, na watekaji nyara, wakatetemeka nao; hata na nchi ikatetemeka pia; basi kulikuwa na tetemeko kubwa mno.