1 Samweli 14:1-15
1 Samweli 14:1-15 NENO
Siku moja Yonathani mwana wa Sauli akamwambia kijana mbeba silaha wake, akasema, “Njoo, tuwavukie Wafilisti kwenye doria upande ule mwingine.” Lakini hakumwambia baba yake. Sauli alikuwa akikaa kwenye viunga vya Gibea chini ya mkomamanga huko Migroni. Alikuwa pamoja na watu wapatao mia sita; miongoni mwao alikuwepo Ahiya, aliyekuwa amevaa kizibau. Alikuwa mwana wa Ikabodi, nduguye Ahitubu mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa BWANA huko Shilo. Hakuna yeyote aliyekuwa na habari kwamba Yonathani alikuwa ameondoka. Kila upande wa njia ambayo Yonathani alikusudia kupita ili kuvuka kufikia doria ya Wafilisti kulikuwa na jabali; moja lilikuwa linaitwa Bosesi, na jingine Sene. Jabali moja lilisimama kaskazini kuelekea Mikmashi na jingine upande wa kusini kuelekea Geba. Yonathani akamwambia kijana wake mbeba silaha, “Njoo, tuvukie doria ya wale jamaa wasiotahiriwa. Huenda BWANA atatenda kwa ajili yetu. Hakuna chochote kitakachoweza kumzuia BWANA kuokoa, kwamba ni kwa wingi au kwa uchache.” Mbeba silaha wake akamwambia, “Fanya yale yote uliyo nayo katika moyo wako. Songa mbele; moyo wangu na roho yangu viko pamoja nawe.” Yonathani akasema, “Basi njoo; tutavuka kuwaelekea hao watu na kuacha watuone. Wakituambia, ‘Subirini hapo hadi tuje kwenu,’ tutakaa pale tulipo na hatutakwea kwao. Lakini kama watasema, ‘Pandeni mje kwetu,’ tutakwea, kwa sababu hiyo itakuwa ishara yetu kwamba BWANA amewatia mikononi mwetu.” Basi wote wawili wakajionesha kwa doria ya Wafilisti. Wafilisti wakasema, “Tazama! Waebrania wanatambaa toka mashimoni walimokuwa wamejificha.” Wanaume wa kwenye doria wakawapazia sauti Yonathani na mbeba silaha wake, wakisema, “Njooni, pandeni kwetu, nasi tutawakomesha.” Basi Yonathani akamwambia mbeba silaha wake, “Panda nyuma yangu; BWANA amewatia mikononi mwa Israeli.” Yonathani akapanda juu, akitumia mikono yake na miguu, pamoja na mbeba silaha wake papo hapo nyuma yake. Wafilisti wakaanguka mbele ya Yonathani, naye mbeba silaha wake akamfuata akiwaua nyuma yake. Katika hilo shambulio la kwanza, Yonathani na mbeba silaha wake waliua kama watu ishirini kwenye eneo kama la nusu eka. Kisha fadhaa ikawapata jeshi lote, wale waliokuwa kambini na shambani, wale waliokuwa katika doria na makundi ya washambuliaji, nayo ardhi ilitetemeka. Ilikuwa ni hofu ya ghafula iliyotumwa na Mungu.