Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yoshua Mwana wa Sira 40

40
Umaskini wa Binadamu
1Taabu nyingi sana Mungu amemgawia kila mtu, na nira nzito ipo juu ya wanadamu; tangu siku yao ya kutoka tumboni mwa mama zao, hata siku ile watakapoirudia nchi, mama wa wote walio hai. 2Kutazamia mambo yatakayokuja, na siku ya kufariki, huwahangaisha mawazo yao, na kuwaletea hofu ya moyoni; 3tangu yeye aketiye juu ya kiti cha utukufu, hata yeye naye ajidhiliye katika mavumbi na majivu; 4tangu yeye aliyevikwa kilemba au taji, hata yeye naye aliyevaa mavazi ya nywele. Hakuna ila wivu, na matata, na udhia, na hofu ya mauti, na ghadhabu, na ugomvi. 5Hata na wakati wa mtu kupata raha kitandani pake, usingizi wake wa usiku hutaabisha fahamu zake. 6Ama hupata raha kidogo tu, ama hapati; na baadaye katika usingizi wake, kama katika zamu ya kukesha, amefadhaika katika maono ya moyo wake, kama mtu aliyeokoka na ghasia ya vita; 7naam, wakati ule ule wa kuokoka huamka, na kushangaa kuona ya kuwa hofu yake si kitu. 8Ndivyo ilivyo kwa wote wenye mwili, binadamu na hayawani; hata zaidi mara saba juu ya wenye dhambi. 9Mauti, na kumwaga damu, na ugomvi, na upanga; misiba, njaa, dhiki, na tauni; 10mambo hayo yote yaliumbwa kwa ajili ya waovu; pia na kwa sababu yao kulikuja gharika. 11Yote yaliyo ya nchi yairudia nchi, na yote yaliyotoka juu yatarudi huko tena.
Asiye Haki Hatafaulu
12Rushwa na udhalimu utafutiwa mbali,
Bali uaminifu utakaa hata milele.
13Mapato ya mwovu yatakauka kama mto.
Na kama ngurumo penye mvua yatapita.
14Kwa kufumbua mkono mtu atafurahishwa,
Bali wanyimivu watapotelea mbali.
15Watoto wa waasi hawana chipukizi,
Na shina la wasio haki li juu ya jabali.
16Nyasi ya mtoni iotayo ukingoni mwa maji
Itang'olewa kutangulia majani yote.
17Bali ukunjufu ni bustani ya mibaraka,
Na kutoa sadaka kunadumu milele.
Furaha za Maisha
18Mtenda kazi ana maisha mema
Naye pia aliyeona radhi,
Naye aonaye dafina hupita wote wawili.
19Watoto na kujenga mji
Hulithibitisha jina la mtu,
Naye apataye hekima hupita wote wawili,
Kufuga ng'ombe na ulimaji
Hulifanikisha jina la mtu,
Naye mke mpendwa kupita yote mawili.
20Kunywa mvinyo na kuimba
Kunachangamsha moyo,
Na upendano wa rafiki hupita yote mawili.
21Filimbi na kinubi
Hutoa sauti nzuri,
Na ulimi wenye neema hupita vyote viwili.
22Neema na uzuri
Hulifurahisha jicho,
Na jani bichi la mpunga hupita yote mawili.
23Rafiki na mwenzake
Hawakutani vibaya,
Na mke na mumewe hupita wote wawili.
24Udugu na msaada
Hufaa siku ya taabu,
Na sadaka huokoa kupita yote mawili.
25Dhahabu na fedha
Huuimarisha mguu wako,
Na shauri lina staha kupita vyote viwili.
26Mali na nguvu
Vitauinua moyo wako,
Na kumcha BWANA hupita vyote viwili.
Hakuna upungufu katika kumcha BWANA,
Wala hakuna haja kutafuta msaada zaidi;
27Kumcha BWANA ni bustani ya baraka,
Nayo humfunika mtu kupita utukufu wote.
Aibu ya Kuombaomba
28Mwanangu, usiishi maisha ya mwombaji
Ni afadhali kufa kuliko kuomba.
29Mtu anayetazamia meza ya mgeni, maisha yake si maisha. Atainajisi roho yake kwa vyakula vya mtu mwingine, walakini mtu mwenye ufahamu ataviona vinaleta uchungu. 30Kinywani pake mwenye choyo kuomba ni kutamu; bali tumboni mwake huwashwa moto.

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha