Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yoshua Mwana wa Sira 39

39
Shughuli za Mwandishi
1Lakini mtu aikazaye roho yake kumcha Mungu, na kuitafakari torati yake Aliye Juu, hayupo mbali. Yeye ataitafuta hekima ya watu wote wa kale, na kujishughulisha na maneno ya manabii. 2Yeye ataweka akiba ya mazungumzo ya watu maarufu, na kujiingiza katika vikombo vya mafumbo, 3na kuchungulia maana ya ndani ya mifano, na kujizoeza katika maana iliyofichwa ya mithali. 4Atatumika miongoni mwa wakuu, na kuhudhuria mbele ya wafalme. Atasafiri katikati ya nchi za mataifa wageni; ambaye yeye mwenyewe amepatwa na mema na mabaya katika wanadamu. 5Atajikaza moyo kumwendea mapema BWANA aliyemuumba, na kuomba dua mbele zake Aliye Juu, na kufumbua kinywa chake kwa kusali, na kumsihi kwa ajili ya dhambi zake. 6Akijaliwa na BWANA aliye Mkuu, atajazwa roho ya ufahamu, na kukupua maneno ya hekima yake kama manyunyu, na kumshukuru BWANA katika sala zake. 7Atayaeleza mashauri yake na maarifa yake, na kuzitafakari siri zake. 8Atadhihirisha mafundisho ya hekima, na kuona fahari juu ya sheria ya agano la BWANA. 9Wengi watausifu ufahamu wake, wala kadiri ulimwengu udumuvyo haufutiki; wala ukumbusho wake hautaondoka; ila jina lake litaisha kizazi baada ya kizazi. 10Mataifa watatangaza habari za hekima yake, na makusanyiko watazihubiri sifa zake; 11katika kuishi kwake atabarikiwa kuliko watu elfu, naye atakapofariki atazidi kuwa heri.
Wimbo wa kumsifu Mungu
12Nitazidi kuyahubiri niliyoyafikiri; nimejazwa kama mbalamwezi. 13Enyi watoto watakatifu, mnisikilize, na kuchanua kama mwaridi uotao kandokando ya kijito cha maji. 14Toeni harufu nzuri kama ya manukato, chanueni maua kama nyinyoro, mkaeneze harufu iliyo tamu; na kuimba wimbo ulio wa kuhimidi. Mhimidini BWANA kwa ajili ya matendo yake yote. 15Likuzeni jina lake, na kuzitoa sifa zake, kwa nyimbo za midomo yenu na kwa kinubi. Nanyi mtakapotoa sifa zake imbeni hivi,
16Matendo yote ya BWANA ni mazuri mno,
Na kila haja huishibisha wakati wake.
17Kwa neno lake maji yalisimama kama fungu,
Na kwa neno la kinywa chake ikawa nuru.
18Upesi huyafanikisha mapenzi yake,
Wala hakuna atakayeupinga wokovu wake.
19Mambo yao wote wenye mwili ni mbele zake,
Wala haiwezekani kufichwa machoni pake.
20Huyachungulia tangu milele hata milele,
Kwa hiyo wokovu wake hauna mpaka;
Kwake hakuna dogo wala lililo hafifu,
Wala hakuna la ajabu lisilowezekana.
21Hakuna kusema, Nini hii? Au, Mbona hivi?
Maana yote yamechaguliwa kwa kusudi lake.
22Baraka yake ilifurika nchi kavu kama Nile,
Na kuinywesha maji mengi kama Mto.
23Vivyo hivyo laana yake hufukuza mataifa,
Na kuigeuza nchi ya neema kuwa ya chumvi;
24Njia zake ni sawa mbele ya watakatifu,
Ila zimejiinua kama milima kwa washupavu.
25Mema amewawekea watu wema tangu awali,
Na kwa waovu kuna mema na mabaya;
26Yale yaliyo faradhi kwa maisha ya binadamu,
Maji, na moto, na chuma, na chumvi,
Unga wa ngano, na asali, na maziwa,
Damu ya zabibu, na mafuta, na nguo;
27Vitu hivi vyote ni vyema kwa wenye adili,
Navyo kwa wakosaji vitageuka vibaya.
28Kuna pepo zilizoumbwa kwa kisasi,
Na kwa ghadhabu kali hupiga kwa nguvu;
Muhula ukiwadia humimina ukali wake,
Na kuikomesha hasira yake aliyezifanya.
29Moto, na mvua ya mawe, na njaa, na tauni,
Hayo yote yalihulukiwa kwa hukumu;
30Meno ya wanyama, na nge, na nyoka,
Na upanga ukiwaangamiza wenye dhambi.
31Hayo yote yakaumbwa kwa makusudi yake.
Yamo kanzini mwake yatakapotakiwa;
Yatashangilia wakati atakapoyaamuru,
Wakati huo wasilivunje neno lake.
32Kwa hiyo tangu mwanzo nilikusudia, nikafikiri hivyo, nami nitayaandika hayo. 33Matendo yote ya BWANA ni mazuri mno, na kila haja huishibisha wakati wake. 34Hakuna awezaye kusema, Hili ni baya kuliko hili; maana yote yatakuja kusifiwa kwa majira yake. 35Na sasa imbeni sifa kwa moyo wote na kwa vinywa vyenu, nanyi lihimidini jina lake Aliye Mtakatifu.

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha