Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zab 78:40-72

Zab 78:40-72 SUV

Walimwasi jangwani mara ngapi? Na kumhuzunisha nyikani! Wakarudi nyuma wakamjaribu Mungu; Wakampa mpaka Mtakatifu wa Israeli. Hawakuukumbuka mkono wake, Wala siku ile alipowakomboa na mtesi. Alivyoziweka ishara zake katika Misri, Na miujiza yake katika konde la Soani. Aligeuza damu mito yao, Na vijito wasipate kunywa. Aliwapelekea mainzi wakawala, Na vyura wakawaharibu. Akawapa tunutu mazao yao, Na nzige kazi yao. Aliiharibu mizabibu yao kwa mvua ya mawe, Na mikuyu yao kwa mawe ya barafu. Akaacha ng’ombe zao wapigwe kwa mvua ya mawe, Na makundi yao kwa umeme. Akawapelekea ukali wa hasira yake, Ghadhabu, na uchungu, na taabu, Kundi la malaika waletao mabaya. Akiifanyizia njia hasira yake; Wala hakuziepusha roho zao na mauti, Bali aliiachia tauni uhai wao; Akampiga kila mzaliwa wa kwanza wa Misri, Malimbuko ya nguvu katika hema za Hamu. Bali aliwaongoza watu wake kama kondoo, Akawachunga kama kundi jangwani. Hao akawachukua salama wala hawakuogopa, Bali bahari iliwafunikiza adui zao. Akawapeleka hadi mpaka wake mtakatifu, Mlima alioununua kwa mkono wake wa kuume. Akawafukuza mataifa mbele yao, Akawapimia urithi kwa kamba, Na kuwakalisha kabila za Israeli katika hema zao. Lakini walimjaribu Mungu Aliye juu, wakamwasi, Wala hawakuzishika shuhuda zake. Bali walirudi nyuma, wakahaini kama baba zao; Wakaepea kama upinde usiofaa. Wakamkasirisha kwa mahali pao pa juu, Wakamtia wivu kwa sanamu zao. Mungu akasikia, akaghadhibika, Akamkataa Israeli kabisa. Akaiacha maskani ya Shilo, Hema aliyoiweka katikati ya wanadamu; Akaziacha nguvu zake kutekwa, Na fahari yake mkononi mwa mtesi. Akawatoa watu wake wapigwe kwa upanga; Akaughadhibikia urithi wake. Moto ukawala vijana wao, Wanawali wao hawakuimbiwa nyimbo za arusi, Makuhani wao walianguka kwa upanga, Wala wajane wao hawakuomboleza. Ndipo Bwana alipoamka kama aliyelala usingizi, Kama shujaa apigaye kelele sababu ya mvinyo; Akawapiga watesi wake akawarudisha nyuma, Akawatia aibu ya milele. Ila akaikataa hema ya Yusufu; Wala hakuichagua kabila ya Efraimu. Bali aliichagua kabila ya Yuda, Mlima Sayuni alioupenda. Akajenga patakatifu pake kama vilele, Kama dunia aliyoiweka imara milele. Akamchagua Daudi, mtumishi wake, Akamwondoa katika mazizi ya kondoo. Nyuma ya kondoo wanyonyeshao alimwondoa, Awachunge Yakobo watu wake, na Israeli urithi wake. Akawalisha kwa ukamilifu wa moyo wake, Na kuwaongoza kwa busara ya mikono yake.

Soma Zab 78