Zab 112:1-9
Zab 112:1-9 SUV
Haleluya. Heri mtu yule amchaye BWANA, Apendezwaye sana na maagizo yake. Wazao wake watakuwa hodari duniani; Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa. Nyumbani mwake mna utajiri na mali, Na haki yake yakaa milele. Nuru huwazukia wenye adili gizani; Ana fadhili na huruma na haki. Heri atendaye fadhili na kukopesha; Atengenezaye mambo yake kwa haki. Kwa maana hataondoshwa kamwe; Mwenye haki atakumbukwa milele. Hataogopa habari mbaya; Moyo wake u imara ukimtumaini BWANA. Moyo wake umethibitika hataogopa, Hata awaone watesi wake wameshindwa. Amekirimu, na kuwapa maskini, Haki yake yakaa milele, Pembe yake itatukuzwa kwa utukufu.