Mit 11:1-31
Mit 11:1-31 SUV
Mizani ya hadaa ni chukizo kwa BWANA; Bali vipimo vilivyo sawasawa humpendeza. Kijapo kiburi ndipo ijapo aibu; Bali hekima hukaa na wanyenyekevu. Ukamilifu wao wenye haki utawaongoza Bali ukaidi wao wenye fitina utawaangamiza. Mali hazifaidii kitu siku ya ghadhabu; Bali haki huokoa na mauti. Haki yake mtu mkamilifu itamwongoza njia yake; Bali mtu mwovu ataanguka kwa uovu wake. Haki yao wenye haki itawaokoa; Bali wafanyao fitina watanaswa kwa hila yao wenyewe. Mtu mwovu atakapokufa, taraja lake lapotea; Na matumaini ya uovu huangamia. Mwenye haki huokolewa katika dhiki, Na mtu mwovu ataiingia badala yake. Asiyemcha Mungu humpoteza jirani yake kwa kinywa chake; Bali wenye haki watapona kwa maarifa. Wenye haki wasitawipo, mji hufurahi; Waovu waangamiapo, watu hupiga kelele. Mji hutukuzwa kwa mbaraka wa mwenye haki; Bali mji hupinduliwa kwa kinywa cha mwovu. Asiye na akili humdharau mwenziwe; Bali mtu aliye na ufahamu hunyamaza. Mwenye kitango akisingizia hufunua siri; Bali mwenye roho ya uaminifu husitiri mambo. Pasipo mashauri taifa huanguka; Bali kwa wingi wa washauri huja wokovu. Amdhaminiye mgeni hakosi ataumia; Achukiaye mambo ya dhamana yu salama. Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima; Na watu wakali hushika mali siku zote. Mwenye rehema huitendea mema nafsi yake; Aliye mkali hujisumbua mwili wake. Mtu mwovu hupata mshahara wa udanganyifu; Apandaye haki ana thawabu ya hakika. Haki huelekea uzima; Afuataye maovu hufuata mauti yake mwenyewe. Wenye kuhalifu moyoni ni chukizo kwa BWANA; Walio wakamilifu katika njia zao humpendeza. Hakika, mtu mwovu hatakosa adhabu; Bali wazao wa wenye haki wataokoka. Kama pete ya dhahabu katika pua ya nguruwe, Kadhalika mwanamke mzuri asiye na akili. Haja ya mwenye haki ni mema tu; Bali kutaraji kwake mtu mwovu ni ghadhabu. Kuna atawanyaye, lakini huongezewa zaidi; Kuna azuiaye isivyo haki, lakini huelekea uhitaji. Nafsi ya mtu mkarimu itawandishwa; Anyweshaye atanyweshwa mwenyewe. Awanyimaye watu nafaka, watu watamlaani; Auzaye nafaka, baraka itakuwa kichwani pake. Atafutaye mema kwa bidii hutafuta fadhili; Atafutaye madhara, hayo yatamjia. Azitegemeaye mali zake ataanguka; Mwenye haki atasitawi kama jani. Ataabishaye nyumba yake mwenyewe ataurithi upepo; Mpumbavu atakuwa mtumwa wa mtu mwenye moyo wa akili. Mazao ya mwenye haki ni mti wa uzima; Na mwenye hekima huvuta roho za watu. Tazama, mwenye haki atalipwa duniani; Basi mwovu na mkosaji si mara nyingi zaidi?