Mit 10:1-14
Mit 10:1-14 SUV
Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye; Bali mwana mpumbavu ni mzigo wa mamaye. Hazina za uovu hazifaidii kitu; Bali haki huokoa na mauti. BWANA hataiacha nafsi ya mwenye haki ife na njaa; Bali tamaa ya mtu mwovu huisukumia mbali. Atendaye mambo kwa mkono mlegevu huwa maskini; Bali mkono wake aliye na bidii hutajirisha. Akusanyaye wakati wa hari ni mwana mwenye hekima; Bali asinziaye wakati wa mavuno ni mwana mwenye kuaibisha. Baraka humkalia mwenye haki kichwani; Bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu. Kuwakumbuka wenye haki huwa na baraka; Bali jina la mtu mwovu litaoza. Aliye na akili moyoni mwake atapokea agizo; Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka. Aendaye kwa unyofu huenda salama; Bali apotoshaye njia zake atajulikana. Akonyezaye kwa jicho huleta masikitiko; Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka. Kinywa chake mwenye haki ni chemchemi ya uzima; Bali jeuri hufunika kinywa chake mtu mwovu, Kuchukiana huondokesha fitina; Bali kupendana husitiri makosa yote. Hekima hupatikana midomoni mwa mwenye ufahamu; Bali fimbo hufaa kwa mgongo wake asiye na ufahamu. Watu wenye akili huweka akiba ya maarifa; Bali kinywa cha mpumbavu ni uangamivu ulio karibu.