Mt 22:15-46
Mt 22:15-46 SUV
Ndipo Mafarisayo wakaenda zao, wakafanya shauri, jinsi ya kumtega kwa maneno. Wakatuma kwake wanafunzi wao pamoja na Maherodi, wakasema, Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, na njia ya Mungu waifundisha katika kweli, wala hujali cheo cha mtu awaye yote, kwa maana hutazami sura za watu. Basi utuambie, Waonaje? Ni halali kumpa Kaisari kodi, ama sivyo? Lakini Yesu akaufahamu uovu wao, akasema, Mbona mnanijaribu, enyi wanafiki? Nionyesheni fedha ya kodi. Nao wakamletea dinari. Akawaambia, Ni ya nani sanamu hii, na anwani hii? Wakamwambia, Ni ya Kaisari. Akawaambia, Basi, mlipeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu. Waliposikia, walistaajabu, wakamwacha, wakaenda zao. Siku ile Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama, wakamwendea, wakamwuliza, wakisema, Mwalimu, Musa alisema, Mtu akifa, akiwa hana watoto, ndugu yake na amwoe yule mkewe, ili ampatie nduguye mzao. Basi, kwetu kulikuwa na ndugu saba; wa kwanza akaoa, akafariki, na kwa kuwa hana mzao, akamwachia nduguye mke wake. Vivyo hivyo wa pili naye, na wa tatu, hata wote saba. Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye. Basi, katika kiyama, atakuwa mke wa yupi katika wale saba? Maana wote walikuwa naye. Yesu akajibu, akawaambia, Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu. Kwa maana katika kiyama hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika mbinguni. Tena kwa habari ya kiyama ya watu, hamjalisoma neno lililonenwa na Mungu, akisema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo? Mungu si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Na makutano waliposikia, walishangaa kwa mafunzo yake. Na Mafarisayo waliposikia ya kwamba amewafumba kinywa wale Masadukayo, walifanya shauri pamoja. Mmoja wao, mwana-sheria, akamwuliza, akimjaribu; Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii. Na Mafarisayo walipokusanyika, Yesu aliwauliza, akisema, Mwaonaje katika habari za Kristo? Ni mwana wa nani? Wakamwambia, Ni wa Daudi. Akawauliza, Imekuwaje basi Daudi katika Roho kumwita Bwana, akisema, Bwana alimwambia Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, Hata niwawekapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako? Basi, Daudi akimwita Bwana, amekuwaje ni mwanawe? Wala hakuweza mtu kumjibu neno; wala hakuthubutu mtu ye yote tangu siku ile kumwuliza neno tena.