Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Lk 2

2
Kuzaliwa kwa Yesu
1Siku zile amri ilitoka kwa Kaisari Augusto ya kwamba iandikwe orodha ya majina ya watu wote wa ulimwengu. 2Orodha hii ndiyo ya kwanza iliyoandikwa hapo Kirenio alipokuwa liwali wa Shamu. 3Watu wote wakaenda kuandikwa, kila mtu mjini kwao. 4Yusufu naye aliondoka Galilaya, toka mji wa Nazareti, akapanda kwenda Uyahudi mpaka mji wa Daudi, uitwao Bethlehemu, kwa kuwa yeye ni wa mbari na jamaa ya Daudi; 5#Lk 1:27ili aandikwe pamoja na Mariamu mkewe, ambaye amemposa, naye ana mimba. 6Ikawa, katika kukaa huko, siku zake za kuzaa zikatimia, 7#Mt 1:25akamzaa mwanawe, kifungua mimba, akamvika nguo za kitoto, akamlaza katika hori ya kulia ng’ombe, kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni.
Wachungaji na Malaika
8Na katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku. 9Malaika wa Bwana akawatokea ghafula, utukufu wa Bwana ukawang’aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu. 10Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; 11maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. 12Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng’ombe. 13#Dan 7:10Mara walikuwapo pamoja na huyo malaika, wingi wa jeshi la mbinguni, wakimsifu Mungu, na kusema,
14 # Lk 19:38; Isa 57:19; Efe 2:14,17 Atukuzwe Mungu juu mbinguni,
Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.
15Ikawa, malaika hao walipoondoka kwenda zao mbinguni, wale wachungaji waliambiana, Haya, na twendeni mpaka Bethlehemu, tukalione hilo lililofanyika, alilotujulisha Bwana. 16Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini. 17#Lk 2:10-12Walipomwona wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto. 18Wote waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji. 19#Lk 2:51Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake. 20Wale wachungaji wakarudi, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona, kama walivyoambiwa.
Yesu Apewa Jina
21 # Law 12:3; Lk 1:31,59 Hata zilipotumia siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu; kama alivyoitwa na malaika kabla hajachukuliwa mimba.
Yesu Apelekwa Hekaluni
22 # Law 12:6-8 Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, 23#Kut 13:2,12,15(kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana), 24#Law 5:11; 12:8wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili. 25#Isa 40:1; 49:13Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. 26Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. 27Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, 28yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema,
29 # Mwa 46:30 Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako,
Kwa amani, kama ulivyosema;
30 # Isa 40:5; 52:10 Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako,
31Uliouweka tayari machoni pa watu wote;
32 # Isa 42:6; 49:6; 52:10 Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa,
Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli.
33Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. 34#Isa 8:14; Mt 21:42; 1 Kor 1:23; 1 Pet 2:8Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. 35Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi.
36Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. 37#1 Tim 5:5Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. 38#Isa 52:9Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake.
Kurudi huko Nazareti
39 # Mt 2:23 Basi, walipokwisha kuyatimiza yote kama yalivyoagizwa katika sheria ya Bwana, walirejea Galilaya mpaka mjini kwao, Nazareti. 40#Lk 1:80; 2:52Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.
Kijana Yesu Hekaluni
41 # Kut 12:1-27; 23:14-17; Kum 16:1-8 Basi, wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka. 42Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu; 43#Kut 12:18na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari. 44Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao; 45na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta. 46Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. 47Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake. 48Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni. 49#Yn 2:16Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? 50Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia. 51#Lk 2:19Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake.
52 # 1 Sam 2:26; Mit 3:4 Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.

Iliyochaguliwa sasa

Lk 2: SUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha