Isa 54
SUV

Isa 54

54
Agano la Amani la Milele
1 # Gal 4:27 Imba, wewe uliye tasa, wewe usiyezaa; paza sauti yako kwa kuimba, piga kelele, wewe usiyekuwa na utungu; maana watoto wake aliyeachwa ni wengi kuliko watoto wake yeye aliyeolewa, asema BWANA. 2Panua mahali pa hema yako, na wayatandaze mapazia ya maskani yako; usiwakataze; ongeza urefu wa kamba zako; vikaze vigingi vya hema yako. 3Kwa maana utaenea upande wa kuume na upande wa kushoto; na wazao wako watawamiliki mataifa; wataifanya miji iliyokuwa ukiwa kukaliwa na watu. 4Usiogope; maana hutatahayarika; wala usifadhaike; maana hutaaibishwa; kwa kuwa utaisahau aibu ya ujana wako, pia mashutumu ya ujane wako hutayakumbuka tena. 5#Isa 41:14; 44:6; 49:7; Ayu 19:25; Rum 3:29Kwa sababu Muumba wako ni mume wako; BWANA wa majeshi ndilo jina lake; na Mtakatifu wa Israeli ndiye Mkombozi wako; Yeye ataitwa Mungu wa dunia yote. 6Maana BWANA amekuita kama mke aliyeachwa na kuhuzunishwa rohoni, kama mke wakati wa ujana, atupwapo, asema Mungu wako. 7#2 Kor 4:17Kwa kitambo kidogo nimekuacha; lakini kwa rehema nyingi nitakukusanya. 8#Yer 31:3Kwa ghadhabu ifurikayo nalikuficha uso wangu dakika moja; lakini kwa fadhili za milele nitakurehemu, asema BWANA, Mkombozi wako. 9#Yer 31:35; Mwa 9:8-17Kwa maana jambo hili limekuwa kama maji ya Nuhu kwangu; maana kama nilivyoapa ya kwamba maji ya Nuhu hayatapita juu ya dunia tena, kadhalika nimeapa ya kwamba sitakuonea hasira, wala kukukemea. 10#Zab 46:2; 89:33Maana milima itaondoka, na vilima vitaondolewa; bali wema wangu hautaondoka kwako, wala agano langu la amani halitaondolewa; asema BWANA akurehemuye.
11 # Ufu 21:18-21 Ewe uliyeteswa, uliyerushwa na tufani, usiyetulizwa, tazama, nitaweka mawe yako kwa rangi nzuri, nitaweka misingi yako kwa yakuti samawi. 12Nami nitaifanya minara yako ya akiki nyekundu, na malango yako ya almasi, na mipaka yako yote ya mawe yapendezayo. 13#Isa 11:9; 1 Kor 2:10; 1 The 4:9; Flp 4:7; Yn 6:45; 14:27Na watoto wako wote watafundishwa na BWANA; na amani ya watoto wako itakuwa nyingi. 14Utathibitika katika haki; utakuwa mbali na kuonewa, kwa maana hutaogopa; na mbali na hofu, kwa maana haitakukaribia. 15Tazama, yamkini watakusanyana; lakini si kwa shauri langu. Watu wo wote watakaokusanyana juu yako wataanguka kwa ajili yako. 16Tazama, nimemwumba mhunzi avukutaye moto wa makaa, akatoa silaha kwa kazi yake; nami nimemwumba mharibu ili aharibu. 17#Mdo 6:10; 2 Kor 2:14; Ufu 12:10; Isa 50:8,9; 45:24Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa BWANA, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema BWANA.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.


Jifunze Mengi Kuhusu Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia