Warumi 3:9-31
Warumi 3:9-31 NENO
Tusemeje basi? Je, sisi ni bora kuliko wao? La hasha! Kwa maana tumekwisha kuhakikisha kwa vyovyote kwamba Wayahudi na watu wa Mataifa wote wako chini ya nguvu ya dhambi. Kama ilivyoandikwa: “Hakuna mwenye haki, hakuna hata mmoja. Hakuna hata mmoja mwenye ufahamu, hakuna hata mmoja amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wote wameoza pamoja; hakuna atendaye mema, naam, hakuna hata mmoja.” “Makoo yao ni makaburi wazi; kwa ndimi zao wao hufanya udanganyifu.” “Sumu ya nyoka iko midomoni mwao.” “Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu.” “Miguu yao ina haraka kumwaga damu; maangamizi na taabu viko katika njia zao, wala njia ya amani hawaijui.” “Hakuna hofu ya Mungu machoni pao.” Basi tunajua kwamba chochote sheria inachosema, inawaambia wale walio chini ya sheria ili kila kinywa kinyamazishwe na ulimwengu wote uwajibike kwa Mungu. Kwa hiyo hakuna binadamu hata mmoja atakayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa matendo ya sheria, kwa maana sheria hutufanya tuitambue dhambi. Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirishwa pasipo sheria, ambayo Sheria na Manabii wanaishuhudia. Haki hii inayotoka kwa Mungu hupatikana kwa Yesu Kristo kwa wote wanaomwamini. Kwa maana hapo hakuna tofauti, kwa kuwa wote wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu, wanahesabiwa haki bure kwa neema yake kupitia kwa ukombozi ulio katika Kristo Yesu. Mungu alimtoa awe dhabihu ya upatanisho kupitia kwa imani katika damu yake. Alifanya hivi ili kuonesha haki yake, kwa sababu kwa ustahimili wake, Mungu aliziachilia bila adhabu zile dhambi zilizotangulia kufanywa. Alifanya hivyo ili kuonesha haki yake wakati huu, ili yeye awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yule anayemwamini Yesu. Basi, kujivuna kuko wapi? Kumewekwa mbali. Kwa sheria gani? Je, ni kwa ile ya matendo? La, bali kwa ile sheria ya imani. Kwa maana twaona kwamba mwanadamu huhesabiwa haki kupitia kwa imani wala si kwa matendo ya sheria. Je, Mungu ni Mungu wa Wayahudi peke yao? Je, yeye si Mungu wa watu wa Mataifa pia? Naam, yeye ni Mungu wa watu wa Mataifa pia. Basi kwa kuwa kuna Mungu mmoja tu, atawahesabia haki wale waliotahiriwa kwa imani na wale wasiotahiriwa kwa imani hiyo hiyo. Je, basi ni kwamba tunaibatilisha sheria kwa imani hii? La, hasha! Badala yake tunaithibitisha sheria.