Zaburi 80
80
Zaburi 80
Maombi kwa ajili ya kuponywa kwa taifa
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Yungiyungi za Agano”. Zaburi ya Asafu.
1 Ee Mchungaji wa Israeli tusikie,
wewe umwongozaye Yusufu kama kundi;
wewe uketiye kwenye kiti cha enzi
katikati ya makerubi, angaza
2 mbele ya Efraimu, Benyamini na Manase.
Uamshe nguvu zako,
uje utuokoe.
3 Ee Mungu, uturejeshe,
utuangazie uso wako,
ili tuweze kuokolewa.
4 Ee Bwana Mungu wa majeshi,
hata lini hasira yako itawaka
dhidi ya maombi ya watu wako?
5 Umewalisha kwa mkate wa machozi,
umewafanya wanywe machozi bakuli tele.
6 Tumekuwa chanzo cha ugomvi kwa majirani zetu,
na adui zetu wanatudhihaki.
7 Ee Mungu wa majeshi, uturejeshe;
utuangazie uso wako,
nasi tuweze kuokolewa.
8 Ulileta mzabibu kutoka Misri,
ukawafukuza mataifa, ukaupanda.
9Uliandaa shamba kwa ajili yake,
mizizi ikawa imara, ukajaza nchi.
10Milima ilifunikwa kwa kivuli chake,
matawi yake yakafunika mierezi mikubwa.
11 Matawi yake yalienea hadi Baharini#80:11 pengine ni Bahari ya Mediterania,
machipukizi yake hadi kwenye Mto#80:11 yaani Mto Frati.
12 Mbona umebomoa kuta zake
ili wote wapitao karibu
wazichume zabibu zake?
13 Nguruwe mwitu wanauharibu,
na viumbe wa kondeni hujilisha humo.
14 Turudie, Ee Mungu wa majeshi!
Tazama chini kutoka mbinguni na uone!
Linda mzabibu huu,
15 mche ulioupanda kwa mkono wako wa kuume,
mwana uliyemlea
kwa ajili yako mwenyewe.
16 Mzabibu wako umekatwa, umechomwa moto,
unapowakemea, watu wako huangamia.
17Mkono wako na utulie juu ya mtu aliye katika mkono wako wa kuume,
mwana wa mtu uliyemlea kwa ajili yako mwenyewe.
18Ndipo hatutakuacha tena,
utuhuishe, nasi tutaliitia jina lako.
19Ee Bwana Mungu wa majeshi, uturejeshe;
utuangazie uso wako,
ili tuweze kuokolewa.
Iliyochaguliwa sasa
Zaburi 80: NEN
Kuonyesha
Nakili
Linganisha
Shirikisha
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Holy Bible, Kiswahili Contemporary Version™ (Neno: Biblia Takatifu™) | Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.
Biblica® Cross Reference System | Copyright © 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.