Zaburi 41
41
Zaburi 41
Maombi ya mtu mgonjwa
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.
1 Heri mtu yule anayemjali mnyonge,
Bwana atamwokoa wakati wa shida.
2 Bwana atamlinda na kuyahifadhi maisha yake,
atambariki katika nchi
na hatamwacha katika tamaa ya adui zake.
3 Bwana atamtegemeza akiwa mgonjwa kitandani,
na atamwinua kutoka kitandani mwake.
4 Nilisema, “Ee Bwana nihurumie,
niponye, maana nimekutenda dhambi wewe.”
5 Adui zangu wanasema kwa hila,
“Lini atakufa, na jina lake litokomee kabisa.”
6 Kila anapokuja mtu kunitazama,
huzungumza uongo,
huku moyo wake ukikusanya masingizio;
kisha huondoka na kuyasambaza.
7 Adui zangu wote hunongʼonezana dhidi yangu,
hao huniwazia mabaya sana, wakisema,
8 “Ugonjwa mbaya sana umempata,
kamwe hatainuka tena kitandani mwake.”
9 Hata rafiki yangu wa karibu niliyemwamini,
yule aliyekula chakula changu
ameniinulia kisigino chake.
10 Lakini wewe, Ee Bwana, nihurumie,
ukaniinue tena, ili niweze kuwalipiza kisasi.
11 Najua kwamba wapendezwa nami,
kwa kuwa adui yangu hanishindi.
12 Katika uadilifu wangu unanitegemeza
na kuniweka kwenye uwepo wako milele.
13 Mtukuzeni Bwana, Mungu wa Israeli,
tangu milele na hata milele.
Amen na Amen.
Iliyochaguliwa sasa
Zaburi 41: NEN
Kuonyesha
Nakili
Linganisha
Shirikisha
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Holy Bible, Kiswahili Contemporary Version™ (Neno: Biblia Takatifu™) | Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.
Biblica® Cross Reference System | Copyright © 2025 by Biblica, Inc. | Used with permission. All rights reserved worldwide.