Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 40

40
Zaburi 40
Wimbo wa sifa
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.
1 Nilimngoja Bwana kwa saburi,
naye akanijia na kusikia kilio changu.
2 Akanipandisha kutoka shimo la uharibifu,
kutoka matope na utelezi;
akaiweka miguu yangu juu ya mwamba
na kunipa mahali imara pa kusimama.
3 Akaweka wimbo mpya kinywani mwangu,
wimbo wa sifa kwa Mungu wetu.
Wengi wataona na kuogopa
na kuweka tumaini lao kwa Bwana.
4 Heri mtu yule amfanyaye Bwana kuwa tumaini lake,
asiyewategemea wenye kiburi,
wale wenye kugeukia miungu ya uongo.
5 Ee Bwana Mungu wangu,
umefanya mambo mengi ya ajabu.
Mambo uliyopanga kwa ajili yetu
hakuna awezaye kukuhesabia;
kama ningesema na kuyaelezea,
yangekuwa mengi mno kuyatangaza.
6 Dhabihu na sadaka hukuvitaka,
lakini umefungua masikio yangu#40:6 au bali mwili uliniandalia;
sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi
hukuzihitaji.
7Ndipo niliposema, “Mimi hapa, nimekuja:
imeandikwa kunihusu katika kitabu.
8 Ee Mungu wangu,
natamani kuyafanya mapenzi yako;
sheria yako iko ndani ya moyo wangu.”
9 Nimehubiri haki katika kusanyiko kubwa,
sikufunga mdomo wangu,
Ee Bwana, kama ujuavyo.
10 Sikuficha haki yako moyoni mwangu;
ninasema juu ya uaminifu wako na wokovu wako.
Sikuficha upendo wako na kweli yako
mbele ya kusanyiko kubwa.
11 Ee Bwana, usinizuilie huruma zako,
upendo wako na kweli yako daima vinilinde.
12 Kwa maana taabu zisizohesabika zimenizunguka,
dhambi zangu zimenikamata, hata nisiweze kuona.
Zimekuwa nyingi kuliko nywele za kichwa changu,
nao moyo unazimia ndani yangu.
13 Ee Bwana, uwe radhi kuniokoa;
Ee Bwana, njoo hima unisaidie.
14 Wote wanaotafuta kuniua,
waaibishwe na kufadhaishwa;
wote wanaotamani kuangamizwa kwangu,
wafukuzwe mbali kwa aibu.
15 Wale wanaoniambia, “Aha! Aha!”
wafadhaishwe na iwe aibu yao.
16 Lakini wote wanaokutafuta
washangilie na kukufurahia,
wale wanaoupenda wokovu wako siku zote waseme,
Bwana atukuzwe!”
17 Lakini mimi bado ni maskini na mhitaji;
Bwana na anifikirie.
Wewe ndiwe msaada wangu na Mwokozi wangu;
Ee Mungu wangu, usikawie.

Iliyochaguliwa sasa

Zaburi 40: NEN

Kuonyesha

Nakili

Linganisha

Shirikisha

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia