Zaburi 106:24-35
Zaburi 106:24-35 NENO
Kisha waliidharau ile nchi nzuri, hawakuiamini ahadi yake. Walinungʼunika ndani ya mahema yao, wala hawakumtii BWANA. Kwa hiyo akaapa kwa mkono ulioinuliwa kwamba atawafanya waanguke jangwani, kuwatawanya wazao wao waanguke miongoni mwa mataifa, na kuwatawanya katika nchi zote. Walijifunga nira na Baali wa Peori, wakala dhabihu zilizotolewa kwa miungu isiyo na uhai. Waliichochea hasira ya BWANA, wakamkasirisha kwa matendo yao maovu, nayo tauni ikazuka katikati yao. Lakini Finehasi alisimama na kuingilia kati, nayo tauni ikazuiliwa. Hili likahesabiwa kwake haki, kwa vizazi visivyo na mwisho vijavyo. Kwenye maji ya Meriba, walimkasirisha BWANA, janga likampata Musa kwa sababu yao; kwa maana walimwasi Roho wa Mungu, na maneno yasiyofaa yakatoka mdomoni kwa Musa. Hawakuyaangamiza yale mataifa kama BWANA alivyowaagiza, bali walijichanganya na mataifa na wakazikubali desturi zao.

