Mithali 28:7-17
Mithali 28:7-17 NENO
Yeye anayetii sheria ni mwana mwenye ufahamu, bali rafiki wa walafi humwaibisha baba yake. Yeye aongezaye utajiri wake kwa riba kubwa mno hukusanya kwa ajili ya mwingine, ambaye atawahurumia maskini. Mtu yeyote akikataa kusikia sheria, hata maombi yake ni chukizo. Yeye anayemwongoza mwenye haki kwenye mapito mabaya, ataanguka kwenye mtego wake mwenyewe, bali wasio na lawama watapokea urithi mwema. Mtu tajiri anaweza kuwa na hekima machoni pake mwenyewe, bali mtu maskini mwenye busara humtambua alivyodanganyika. Mwenye haki ashindapo, kuna furaha kubwa, bali waovu watawalapo, watu hujificha. Yeye afichaye dhambi zake hatafanikiwa, bali yeyote aziungamaye na kuziacha hupata rehema. Amebarikiwa mtu ambaye siku zote humcha BWANA, bali yeye afanyaye moyo wake kuwa mgumu huanguka kwenye taabu. Kama simba angurumaye au dubu ashambuliaye, ndivyo alivyo mtu mwovu anayetawala wanyonge. Mtawala dhalimu hana akili, bali yeye achukiaye mapato ya udhalimu atafurahia maisha marefu. Mtu mwenye kusumbuliwa na hatia ya kuua atakuwa mtoro hadi kufa; mtu yeyote asimsaidie.