Mithali 21:5-16
Mithali 21:5-16 NENO
Mipango ya mwenye bidii huelekeza kwenye faida, kama vile kwa hakika pupa huelekeza kwenye umaskini. Mali iliyopatikana kwa ulimi wa uongo ni mvuke upitao upesi na mtego wa kufisha. Jeuri ya waovu itawaburuta mbali, kwa kuwa wanakataa kufanya yaliyo sawa. Njia ya mwenye hatia ni ya upotovu, bali tabia ya mtu asiye na hatia ni nyofu. Ni afadhali kuishi pembeni mwa paa la nyumba, kuliko kuishi nyumba moja na mke mgomvi. Mtu mwovu hutamani sana ubaya, jirani yake hapati huruma kutoka kwake. Wakati mwenye mzaha ameadhibiwa, mjinga hupata hekima; wakati mtu mwenye hekima anafundishwa, hupata maarifa. Mwenye Haki huyajua yanayotendeka katika nyumba za waovu, naye atawaangamiza waovu. Mtu akiziba masikio asisikie kilio cha maskini, yeye pia atalia, wala hatajibiwa. Zawadi inayotolewa kwa siri hutuliza hasira, na rushwa iliyofichwa kwenye nguo hutuliza ghadhabu kali. Wakati haki imetendeka, huleta furaha kwa wenye haki, bali hofu kwa watenda maovu. Mtu anayepotea kutoka mapito ya ufahamu, hupumzika katika kundi la waliokufa.