Mathayo 9:1-8
Mathayo 9:1-8 NENO
Yesu akaingia kwenye chombo, akavuka na kufika katika mji wa kwao. Wakati huo huo wakamletea mtu aliyepooza, akiwa amelazwa kwenye mkeka. Yesu alipoiona imani yao, alimwambia yule mtu aliyepooza, “Mwanangu, jipe moyo mkuu. Dhambi zako zimesamehewa.” Kwa ajili ya jambo hili, baadhi ya walimu wa sheria wakasema mioyoni mwao, “Huyu mtu anakufuru!” Lakini Yesu akiyafahamu mawazo yao, akawaambia, “Kwa nini mnawaza maovu mioyoni mwenu? Je, ni lipi lililo rahisi zaidi: kusema, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uende’? Lakini nataka mpate kujua kwamba Mwana wa Adamu ana mamlaka duniani kusamehe dhambi.” Ndipo akamwambia yule aliyepooza, “Inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani mwako.” Yule mtu akasimama, akaenda nyumbani mwake. Umati wa watu walipoyaona haya, wakajawa na hofu ya Mungu, wakamtukuza Mungu aliyekuwa amewakabidhi wanadamu mamlaka kama haya.