Mathayo 9:1-8
Mathayo 9:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Yesu alipanda mashua, akavuka ziwa na kufika katika mji wake. Hapo watu walimletea mtu mmoja aliyepooza mwili, amelazwa juu ya kitanda. Yesu alipoona imani yao, akamwambia huyo mtu aliyepooza, “Jipe moyo mwanangu! Umesamehewa dhambi zako.” Baadhi ya waalimu wa sheria wakaanza kufikiri, “Mtu huyu anamkufuru Mungu!” Yesu aliyajua mawazo yao, akasema, “Kwa nini mnawaza mabaya mioyoni mwenu? Ni lipi lililo rahisi zaidi: Kusema, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Simama, utembee?’ Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anao uwezo duniani wa kuwasamehe watu dhambi.” Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza, “Inuka, chukua kitanda chako, uende nyumbani kwako.” Huyo mtu aliyekuwa amepooza akainuka, akaenda nyumbani kwake. Watu wote katika ule umati walipoona hayo, walishangaa na kuogopa; wakamtukuza Mungu aliyewapa binadamu uwezo wa namna hiyo.
Mathayo 9:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akapanda katika mashua, akavuka, akafika mjini kwao. Na tazama, wakamletea mtu mwenye kupooza, akiwa amelala kitandani; naye Yesu, alipoiona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, Jipe moyo mkuu, mwanangu, umesamehewa dhambi zako. Na tazama, baadhi ya waandishi wakasema nafsini mwao, Huyu anakufuru. Naye Yesu, hali akijua mawazo yao, akasema, Mbona mnawaza maovu mioyoni mwenu? Kwa maana rahisi ni lipi, ni kusema, Umesamehewa dhambi zako, au ni kusema, Ondoka, uende? Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (amwambia yule mwenye kupooza) Inuka, ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwako. Akaondoka, akaenda zake nyumbani kwake. Makutano walipomwona, walishikwa na hofu, wakamtukuza Mungu, aliyewapa watu amri ya namna hii.
Mathayo 9:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akapanda chomboni, akavuka, akafika mjini kwao. Na tazama, wakamletea mtu mwenye kupooza, amelala kitandani; naye Yesu, alipoiona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, Jipe moyo mkuu, mwanangu, umesamehewa dhambi zako. Na tazama, baadhi ya waandishi wakasema nafsini mwao, Huyu anakufuru. Naye Yesu, hali akijua mawazo yao, akasema, Mbona mnawaza maovu mioyoni mwenu? Kwa maana rahisi ni lipi, ni kusema, Umesamehewa dhambi zako, au ni kusema, Ondoka, uende? Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (amwambia yule mwenye kupooza) Ondoka, ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwako. Akaondoka, akaenda zake nyumbani kwake. Makutano walipomwona, walishikwa na hofu, wakamtukuza Mungu, aliyewapa watu amri ya namna hii.
Mathayo 9:1-8 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Yesu akaingia kwenye chombo, akavuka na kufika katika mji wa kwao. Wakati huo huo wakamletea mtu aliyepooza, akiwa amelazwa kwenye mkeka. Yesu alipoiona imani yao, alimwambia yule mtu aliyepooza, “Mwanangu, jipe moyo mkuu. Dhambi zako zimesamehewa.” Kwa ajili ya jambo hili, baadhi ya walimu wa sheria wakasema mioyoni mwao, “Huyu mtu anakufuru!” Lakini Yesu akiyafahamu mawazo yao, akawaambia, “Kwa nini mnawaza maovu mioyoni mwenu? Je, ni lipi lililo rahisi zaidi: kusema, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uende’? Lakini nataka mpate kujua kwamba Mwana wa Adamu ana mamlaka duniani kusamehe dhambi.” Ndipo akamwambia yule aliyepooza, “Inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani mwako.” Yule mtu akasimama, akaenda nyumbani mwake. Umati wa watu walipoyaona haya, wakajawa na hofu ya Mungu, wakamtukuza Mungu aliyekuwa amewakabidhi wanadamu mamlaka kama haya.