Mathayo 14:1-12
Mathayo 14:1-12 NENO
Wakati huo, Mfalme Herode, mtawala wa Galilaya, alisikia habari za Yesu, akawaambia watumishi wake, “Huyu ni Yohana Mbatizaji; amefufuka kutoka kwa wafu! Hii ndiyo sababu nguvu za kutenda miujiza zinafanya kazi ndani yake.” Herode alikuwa amemkamata Yohana, akamfunga na kumweka gerezani kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake, kwa kuwa Yohana alikuwa amemwambia Herode: “Si halali kwako kuwa na huyo mwanamke.” Herode alitaka sana kumuua Yohana, lakini akaogopa watu, kwa maana walimtambua kuwa ni nabii. Katika siku ya kuadhimisha sikukuu ya kuzaliwa kwa Herode, binti Herodia alicheza mbele ya watu waliohudhuria. Alimfurahisha Herode sana, kiasi kwamba aliahidi kwa kiapo kumpa huyo binti chochote angeomba. Huyo binti, akiwa amechochewa na mama yake, akasema, “Nipe kichwa cha Yohana Mbatizaji kwenye sinia.” Mfalme alisikitika, lakini kwa sababu ya viapo alivyoapa mbele ya wageni, akaamuru kwamba apatiwe ombi lake. Hivyo akaagiza Yohana Mbatizaji akatwe kichwa mle gerezani. Kichwa chake kikaletwa kwenye sinia, akapewa yule binti, naye akampelekea mama yake. Wanafunzi wa Yohana wakaja na kuuchukua mwili wake, wakamzika. Kisha wakaenda wakamwambia Yesu.