Mathayo 14:1-12
Mathayo 14:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati huo, mtawala Herode alisikia sifa za Yesu. Basi, akawaambia watumishi wake, “Mtu huyu ni Yohane Mbatizaji, amefufuka kutoka kwa wafu; ndiyo maana nguvu za miujiza zinafanya kazi ndani yake.” Herode ndiye aliyekuwa amemtia Yohane nguvuni, akamfunga minyororo na kumtia gerezani kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake. Kisa ni kwamba Yohane alikuwa amemwambia Herode, “Si halali kwako kuishi na huyo mwanamke!” Herode alitaka kumuua Yohane, lakini aliogopa watu kwa sababu kwao Yohane alikuwa nabii. Katika sherehe za sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti ya Herodia alicheza mbele ya wageni. Herode alifurahiwa, hata akaahidi kwa kiapo kumpa huyo msichana chochote atakachoomba. Naye, huku akichochewa na mama yake, akaomba, “Nipe papa hapa katika sinia kichwa cha Yohane Mbatizaji.” Mfalme alihuzunika, lakini kwa sababu ya kile kiapo chake na kwa sababu ya wale wageni karamuni, akaamuru apewe. Basi, Herode akatuma mtu gerezani amkate kichwa Yohane. Kichwa chake kikaletwa katika sinia, wakampa yule msichana, naye akampelekea mama yake. Wanafunzi wa Yohane wakaja, wakauchukua mwili wake, wakauzika. Kisha wakaenda kumpasha habari Yesu.
Mathayo 14:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wakati ule mfalme Herode alisikia habari za Yesu, akawaambia watumishi wake, Huyo ndiye Yohana Mbatizaji; amefufuka katika wafu; na kwa hiyo nguvu hizo zinatenda kazi ndani yake. Maana Herode alikuwa amemkamata Yohana, akamfunga, akamtia gerezani, kwa ajili ya Herodia, mke wa Filipo nduguye. Kwa sababu Yohana alimwambia, Si halali kwako kuwa naye. Naye alipotaka kumwua, aliwaogopa watu, maana walimwona Yohana kuwa nabii. Hata ilipofika sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti ya Herodia alicheza mbele ya watu, akampendeza Herode. Hata akaahidi kwa kiapo ya kwamba atampa lolote atakaloliomba. Naye, huku akichochewa na mamaye, akasema, Nipe hapa katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji. Naye mfalme akasikitika; lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya wale walioketi karamuni pamoja naye, akaamuru apewe; akatuma mtu, akamkata kichwa Yohana mle gerezani. Kichwa chake kikaletwa katika kombe, akapewa yule msichana; akakileta kwa mamaye. Wanafunzi wake wakaenda, wakamchukua yule maiti, wakamzika; kisha wakaenda wakampasha Yesu habari.
Mathayo 14:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wakati ule mfalme Herode alisikia habari za Yesu, akawaambia watumishi wake, Huyo ndiye Yohana Mbatizaji; amefufuka katika wafu; na kwa hiyo nguvu hizo zinatenda kazi ndani yake. Maana Herode alikuwa amemkamata Yohana, akamfunga, akamtia gerezani, kwa ajili ya Herodia, mke wa Filipo nduguye. Kwa sababu Yohana alimwambia, Si halali kwako kuwa naye. Naye alipotaka kumwua, aliwaogopa watu, maana walimwona Yohana kuwa nabii. Hata ilipofika sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti Herodia alicheza mbele ya watu, akampendeza Herode. Hata akaahidi kwa kiapo ya kwamba atampa lo lote atakaloliomba. Naye, huku akichochewa na mamaye, akasema, Nipe hapa katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji. Naye mfalme akasikitika; lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya wale walioketi chakulani pamoja naye, akaamuru apewe; akatuma mtu, akamkata kichwa Yohana mle gerezani. Kichwa chake kikaletwa katika kombe, akapewa yule kijana; akakichukua kwa mamaye. Wanafunzi wake wakaenda, wakamchukua yule maiti, wakamzika; kisha wakaenda wakampasha Yesu habari.
Mathayo 14:1-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Wakati huo, Mfalme Herode, mtawala wa Galilaya, alisikia habari za Yesu, akawaambia watumishi wake, “Huyu ni Yohana Mbatizaji; amefufuka kutoka kwa wafu! Hii ndiyo sababu nguvu za kutenda miujiza zinafanya kazi ndani yake.” Herode alikuwa amemkamata Yohana, akamfunga na kumweka gerezani kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake, kwa kuwa Yohana alikuwa amemwambia Herode: “Si halali kwako kuwa na huyo mwanamke.” Herode alitaka sana kumuua Yohana, lakini akaogopa watu, kwa maana walimtambua kuwa ni nabii. Katika siku ya kuadhimisha sikukuu ya kuzaliwa kwa Herode, binti Herodia alicheza mbele ya watu waliohudhuria. Alimfurahisha Herode sana, kiasi kwamba aliahidi kwa kiapo kumpa huyo binti chochote angeomba. Huyo binti, akiwa amechochewa na mama yake, akasema, “Nipe kichwa cha Yohana Mbatizaji kwenye sinia.” Mfalme alisikitika, lakini kwa sababu ya viapo alivyoapa mbele ya wageni, akaamuru kwamba apatiwe ombi lake. Hivyo akaagiza Yohana Mbatizaji akatwe kichwa mle gerezani. Kichwa chake kikaletwa kwenye sinia, akapewa yule binti, naye akampelekea mama yake. Wanafunzi wa Yohana wakaja na kuuchukua mwili wake, wakamzika. Kisha wakaenda wakamwambia Yesu.