Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 13:18-30

Mathayo 13:18-30 NEN

“Sikilizeni basi maana ya ule mfano wa mpanzi: Mtu yeyote anaposikia neno la ufalme naye asilielewe, yule mwovu huja na kunyakua kile kilichopandwa moyoni mwake. Hii ndiyo ile mbegu iliyopandwa kando ya njia. Ile mbegu iliyopandwa kwenye sehemu yenye mawe ni mtu yule ambaye hulisikia neno na hulipokea mara moja kwa furaha. Lakini kwa kuwa hana mizizi yenye kina ndani yake, lile neno hudumu kwa muda mfupi tu. Kisha dhiki au mateso yanapoinuka kwa ajili ya lile neno, yeye anarudi nyuma mara moja. Ile mbegu iliyopandwa katika miiba ni yule mtu anayelisikia neno, lakini masumbufu ya maisha haya na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno na kulifanya lisizae matunda. Lakini ile mbegu iliyopandwa kwenye udongo mzuri ni yule mtu ambaye hulisikia neno na kulielewa. Naye hakika huzaa matunda, akizaa mara mia, au mara sitini, au mara thelathini ya mbegu iliyopandwa.” Yesu akawaambia mfano mwingine, akasema: “Ufalme wa mbinguni unaweza kufananishwa na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake. Lakini wakati kila mtu alipokuwa amelala, adui yake akaja na kupanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. Ngano ilipoota na kutoa masuke, magugu nayo yakatokea. “Watumishi wa yule mwenye shamba wakamjia na kumwambia, ‘Bwana, si tulipanda mbegu nzuri shambani mwako? Basi, magugu yametoka wapi?’ “Akawajibu, ‘Adui ndiye alifanya jambo hili.’ “Wale watumishi wakamuuliza, ‘Je, unataka twende tukayangʼoe?’ “Lakini akasema, ‘Hapana, msiyangʼoe, kwa maana wakati mkingʼoa magugu mnaweza mkangʼoa na ngano pamoja nayo. Acheni ngano na magugu vikue vyote pamoja hadi wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavunaji wayakusanye magugu kwanza, wayafunge matita matita ili yachomwe moto; kisha wakusanye ngano na kuileta ghalani mwangu.’ ”