Walawi 4:20-35
Walawi 4:20-35 NENO
naye atamfanyia fahali huyu kama alivyomfanyia yule fahali mwingine wa sadaka ya dhambi. Kwa njia hii kuhani atawafanyia watu upatanisho, nao watasamehewa. Kisha atamchukua yule fahali nje ya kambi na kumteketeza kama alivyomteketeza yule wa kwanza. Hii ni sadaka ya dhambi kwa ajili ya jumuiya. “ ‘Wakati kiongozi ametenda dhambi bila kukusudia na kufanya yaliyokatazwa katika amri yoyote ya BWANA Mungu wake, ana hatia. Atakapofahamishwa dhambi aliyotenda, ni lazima alete beberu asiye na dosari kuwa sadaka yake. Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha yule mbuzi na kumchinja mahali pale sadaka za kuteketezwa huchinjiwa mbele za BWANA. Hii ni sadaka ya dhambi. Kisha kuhani atachukua sehemu ya damu ya sadaka ya dhambi kwa kidole chake na kuitia kwenye pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketeza, na kuimwaga damu iliyobaki chini ya madhabahu. Atayateketeza mafuta yote juu ya madhabahu, kama alivyoteketeza mafuta ya mnyama wa sadaka ya amani. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho wa dhambi kwa ajili ya yule mtu, naye atasamehewa. “ ‘Kama mtu katika jumuiya ametenda dhambi pasipo kukusudia, na kufanya lile lililokatazwa katika amri yoyote ya BWANA, yeye ana hatia. Atakapofahamishwa dhambi aliyoitenda, ni lazima alete mbuzi jike asiye na dosari kuwa sadaka yake kwa ajili ya dhambi aliyotenda. Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha sadaka ya dhambi na kumchinjia mahali pa kuteketezea sadaka. Kisha kuhani atachukua sehemu ya ile damu kwa kidole chake na kuitia kwenye pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na kuimwaga damu iliyobaki chini ya madhabahu. Atayaondoa mafuta yote, kama vile mafuta yaondolewavyo kwenye sadaka ya amani, naye kuhani atayateketeza juu ya madhabahu kama harufu nzuri ya kumpendeza BWANA. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atasamehewa. “ ‘Akileta mwana-kondoo kuwa sadaka yake ya dhambi, atamleta jike asiye na dosari. Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha huyo mwana-kondoo na kumchinja kwa ajili ya sadaka ya dhambi mahali ambako sadaka ya kuteketezwa huchinjiwa. Kisha kuhani atachukua sehemu ya damu ya sadaka ya dhambi kwa kidole chake na kuitia juu ya pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, na ile damu iliyobaki ataimwaga chini ya madhabahu. Ataondoa mafuta yote, kama vile mafuta yaondolewavyo kutoka kwa mwana-kondoo wa sadaka ya amani, naye kuhani atayateketeza juu ya madhabahu juu ya zile sadaka zilizotolewa kwa BWANA kwa moto. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa dhambi aliyoitenda, naye atasamehewa.


