Walawi 4:20-35
Walawi 4:20-35 Biblia Habari Njema (BHN)
Kwa hiyo atamfanya fahali huyu kama alivyomfanya yule mwingine wa sadaka ya kuondoa dhambi. Basi, huyo kuhani atawafanyia watu ibada hiyo ya upatanisho kwa ajili ya dhambi, nao watasamehewa. Kisha atamchukua fahali huyu na kumpeleka nje ya kambi na kumteketeza kwa moto kama alivyomfanya yule mwingine. Hiyo ni sadaka ya kuondoa dhambi ya jumuiya. “Ikiwa mtawala ametenda dhambi bila kukusudia kwa kufanya kitu kilichokatazwa na amri ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, na hivyo akawa na hatia, mara akijulishwa dhambi hiyo aliyotenda, ataleta sadaka yake ya beberu asiye na dosari. Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha beberu na kumchinjia mahali wanapochinjia sadaka za kuteketezwa mbele ya Mwenyezi-Mungu; hiyo ni sadaka ya kuondoa dhambi. Kuhani atachovya kidole chake katika damu ya sadaka ya kuondoa dhambi na kuzipaka pembe za madhabahu ya kuteketezea sadaka. Damu inayobaki ataimwaga chini kwenye tako la madhabahu ya kuteketezea sadaka. Mafuta yote ya beberu huyo atayateketeza madhabahuni, kama afanyavyo na mafuta ya mnyama wa sadaka ya amani. Kwa hiyo kuhani atamfanyia mtawala ibada hiyo ya upatanisho kwa ajili ya dhambi yake, naye atasamehewa. “Kama mtu wa kawaida ametenda dhambi bila kukusudia, kwa kufanya kitu kilichokatazwa na amri ya Mwenyezi-Mungu na hivyo akawa na hatia, mara atakapojulishwa kuwa ametenda dhambi, ataleta sadaka ya mbuzi jike asiye na dosari kwa ajili ya kuondoa dhambi aliyotenda. Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha mbuzi huyo wa sadaka ya kuondoa dhambi, na kumchinjia mahali wanapochinjia wanyama wa sadaka za kuteketezwa. Kuhani atachovya kidole chake katika damu ya sadaka ya kuondoa dhambi na kuzipaka pembe za madhabahu ya kuteketezea sadaka. Damu iliyobaki ataimwaga chini kwenye tako la madhabahu. Mafuta yote ya mbuzi huyo atayaondoa kama aondoavyo mafuta ya wanyama wa sadaka za amani, naye kuhani atayateketeza madhabahuni, na harufu yake nzuri itampendeza Mwenyezi-Mungu. Basi, kuhani atamfanyia huyo mtu hiyo ibada ya upatanisho, naye atasamehewa. “Ikiwa mtu huyo ataleta mwanakondoo kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi, basi, ataleta mwanakondoo jike asiye na dosari. Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha mwanakondoo huyo wa sadaka ya kuondoa dhambi, na kumchinjia mahali pale wanapochinjia wanyama wa sadaka za kuteketezwa. Kisha kuhani atachovya kidole chake katika damu ya sadaka ya kuondoa dhambi na kuzipaka pembe za madhabahu ya kuteketezea sadaka. Damu inayobaki ataimwaga chini kwenye tako la madhabahu. Kisha atayaondoa mafuta yote kama aondoavyo mafuta ya mwanakondoo wa sadaka ya amani, na kuhani atayateketeza juu ya madhabahu, pamoja na sadaka zitolewazo kwa Mwenyezi-Mungu kwa moto. Naye kuhani atamfanyia ibada ya upatanisho kwa ajili ya dhambi yake, naye atasamehewa.”
Walawi 4:20-35 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndivyo atakavyomfanyia huyo ng'ombe; kama alivyomfanyia huyo ng'ombe wa sadaka ya dhambi, atamfanyia na huyu hivyo; naye kuhani atawafanyia upatanisho, nao watasamehewa. Kisha atamchukua huyo ng'ombe nje ya kambi, na kumteketeza vile vile kama alivyomteketeza ng'ombe wa kwanza; ni sadaka ya dhambi kwa ajili ya mkutano. Mtawala atakapofanya dhambi, na kutenda pasipo kukusudia neno lolote kati ya hayo ambayo BWANA, Mungu wake, aliyazuilia yasifanywe, naye amepata hatia; akijulishwa hiyo dhambi yake aliyoifanya, ataleta mbuzi dume asiye na dosari awe matoleo yake; kisha ataweka mkono wake kichwani mwake huyo mbuzi, na kumchinja hapo wachinjapo sadaka ya kuteketezwa mbele za BWANA; ni sadaka ya dhambi. Kisha kuhani atatwaa baadhi ya damu ya hiyo sadaka ya dhambi kwa kidole chake, na kuitia katika pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, nayo damu yake ataimwaga hapo chini ya madhabahu ya kuteketeza. Na mafuta yake yote atayateketeza juu ya madhabahu, kama alivyoyateketeza mafuta ya hizo sadaka za amani; naye kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya dhambi yake, naye atasamehewa. Na mtu yeyote kati ya watu wa nchi akifanya dhambi pasipo kukusudia, kwa kufanya neno lolote katika hayo ambayo BWANA alizuilia yasifanywe, naye akapata hatia; akijulishwa hiyo dhambi yake aliyoifanya, ndipo atakapoleta mbuzi wa kike mkamilifu, awe matoleo yake kwa ajili ya dhambi yake aliyoifanya. Naye ataweka mkono wake kichwani mwake hiyo sadaka ya dhambi, na kumchinja sadaka ya dhambi mahali hapo pa sadaka ya kuteketezwa. Kisha kuhani atatwaa baadhi ya hiyo damu yake kwa kidole chake, na kuitia katika pembe za madhabahu ya kuteketeza na damu yake yote ataimwaga chini ya madhabahu. Kisha atayaondoa mafuta yake yote, kama vile mafuta yanavyoondolewa katika hizo sadaka za amani; kisha kuhani atayateketeza juu ya madhabahu, iwe harufu ya kupendeza kwa BWANA; na kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atasamehewa. Naye akileta mwana-kondoo kuwa sadaka ya dhambi, ataleta wa kike mkamilifu. Naye ataweka mkono wake kichwani mwake sadaka ya dhambi, kisha atamchinja awe sadaka ya dhambi, mahali hapo wachinjapo sadaka ya kuteketezwa. Kisha kuhani atatwaa katika hiyo damu ya sadaka ya kuteketezwa kwa kidole chake na kuitia katika pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, kisha damu yake yote ataimwaga hapo chini ya madhabahu; kisha atayaondoa mafuta yake yote, kama mafuta ya mwana-kondoo yalivyoondolewa katika hizo sadaka za amani; kisha kuhani atayateketeza juu ya madhabahu, kwa desturi ya hizo sadaka za BWANA zilizosongezwa kwa njia ya moto; na kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya hiyo dhambi yake aliyoifanya, naye atasamehewa.
Walawi 4:20-35 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndivyo atakavyomfanyia huyo ng’ombe; kama alivyomfanyia huyo ng’ombe wa sadaka ya dhambi, atamfanyia na huyu vivyo; naye kuhani atawafanyia upatanisho, nao watasamehewa. Kisha atamchukua huyo ng’ombe nje ya marago, na kumchoma moto vile vile kama alivyomchoma moto ng’ombe wa kwanza; ni sadaka ya dhambi kwa ajili ya mkutano. Mtawala atakapofanya dhambi, na kutenda pasipo kukusudia neno lo lote katika hayo ambayo BWANA, Mungu wake, aliyazuilia yasifanywe, naye amepata hatia; akijulishwa hiyo dhambi yake aliyoifanya, ataleta mbuzi awe matoleo yake, mume, mkamilifu; kisha ataweka mkono wake kichwani mwake huyo mbuzi, na kumchinja hapo wachinjapo sadaka ya kuteketezwa mbele za BWANA; ni sadaka ya dhambi. Kisha kuhani atatwaa katika damu ya hiyo sadaka ya dhambi kwa kidole chake, na kuitia katika pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, nayo damu yake ataimwaga hapo chini ya madhabahu ya kuteketeza. Na mafuta yake yote atayateketeza juu ya madhabahu, kama alivyoyateketeza mafuta ya hizo sadaka za amani; naye kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya dhambi yake, naye atasamehewa. Na mtu awaye yote katika watu wa nchi akifanya dhambi pasipo kukusudia, kwa kufanya neno lo lote katika hayo ambayo BWANA alizuilia yasifanywe, naye akapata hatia; akijulishwa hiyo dhambi yake aliyoifanya, ndipo atakapoleta mbuzi mke mkamilifu, awe matoleo yake kwa ajili ya dhambi yake aliyoifanya. Naye ataweka mkono wake kichwani mwake hiyo sadaka ya dhambi, na kumchinja sadaka ya dhambi mahali hapo pa sadaka ya kuteketezwa. Kisha kuhani atatwaa katika hiyo damu yake kwa kidole chake, na kuitia katika pembe za madhabahu ya kuteketeza na damu yake yote ataimwaga chini ya madhabahu. Kisha atayaondoa mafuta yake yote, kama vile mafuta yanavyoondolewa katika hizo sadaka za amani; kisha kuhani atayateketeza juu ya madhabahu, iwe harufu ya kupendeza kwa BWANA; na kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atasamehewa. Naye akileta mwana-kondoo kuwa sadaka ya dhambi, ataleta wa kike mkamilifu. Naye ataweka mkono wake kichwani mwake sadaka ya dhambi, kisha atamchinja awe sadaka ya dhambi, mahali hapo wachinjapo sadaka ya kuteketezwa. Kisha kuhani atatwaa katika hiyo damu ya sadaka ya kuteketezwa kwa kidole chake na kuitia katika pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, kisha damu yake yote ataimwaga hapo chini ya madhabahu; kisha atayaondoa mafuta yake yote, kama mafuta ya mwana-kondoo yalivyoondolewa katika hizo sadaka za amani; kisha kuhani atayateketeza juu ya madhabahu, kwa desturi ya hizo sadaka za BWANA zilizosongezwa kwa njia ya moto; na kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya hiyo dhambi yake aliyoifanya, naye atasamehewa.
Walawi 4:20-35 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
naye atamfanyia fahali huyu kama alivyomfanyia yule fahali mwingine wa sadaka ya dhambi. Kwa njia hii kuhani atawafanyia watu upatanisho, nao watasamehewa. Kisha atamchukua yule fahali nje ya kambi na kumteketeza kama alivyomteketeza yule wa kwanza. Hii ni sadaka ya dhambi kwa ajili ya jumuiya. “ ‘Wakati kiongozi ametenda dhambi bila kukusudia na kufanya yaliyokatazwa katika amri yoyote ya BWANA Mungu wake, ana hatia. Atakapofahamishwa dhambi aliyotenda, ni lazima alete beberu asiye na dosari kuwa sadaka yake. Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha yule mbuzi na kumchinja mahali pale sadaka za kuteketezwa huchinjiwa mbele za BWANA. Hii ni sadaka ya dhambi. Kisha kuhani atachukua sehemu ya damu ya sadaka ya dhambi kwa kidole chake na kuitia kwenye pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketeza, na kuimwaga damu iliyobaki chini ya madhabahu. Atayateketeza mafuta yote juu ya madhabahu, kama alivyoteketeza mafuta ya mnyama wa sadaka ya amani. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho wa dhambi kwa ajili ya yule mtu, naye atasamehewa. “ ‘Kama mtu katika jumuiya ametenda dhambi pasipo kukusudia, na kufanya lile lililokatazwa katika amri yoyote ya BWANA, yeye ana hatia. Atakapofahamishwa dhambi aliyoitenda, ni lazima alete mbuzi jike asiye na dosari kuwa sadaka yake kwa ajili ya dhambi aliyotenda. Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha sadaka ya dhambi na kumchinjia mahali pa kuteketezea sadaka. Kisha kuhani atachukua sehemu ya ile damu kwa kidole chake na kuitia kwenye pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na kuimwaga damu iliyobaki chini ya madhabahu. Atayaondoa mafuta yote, kama vile mafuta yaondolewavyo kwenye sadaka ya amani, naye kuhani atayateketeza juu ya madhabahu kama harufu nzuri ya kumpendeza BWANA. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atasamehewa. “ ‘Akileta mwana-kondoo kuwa sadaka yake ya dhambi, atamleta jike asiye na dosari. Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha huyo mwana-kondoo na kumchinja kwa ajili ya sadaka ya dhambi mahali ambako sadaka ya kuteketezwa huchinjiwa. Kisha kuhani atachukua sehemu ya damu ya sadaka ya dhambi kwa kidole chake na kuitia juu ya pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, na ile damu iliyobaki ataimwaga chini ya madhabahu. Ataondoa mafuta yote, kama vile mafuta yaondolewavyo kutoka kwa mwana-kondoo wa sadaka ya amani, naye kuhani atayateketeza juu ya madhabahu juu ya zile sadaka zilizotolewa kwa BWANA kwa moto. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa dhambi aliyoitenda, naye atasamehewa.