Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Maombolezo 2:7-22

Maombolezo 2:7-22 NENO

Bwana amekataa madhabahu yake na kuacha mahali patakatifu pake. Amemkabidhi adui kuta za majumba yake ya kifalme; wameshangilia katika nyumba ya BWANA kama katika siku ya sikukuu iliyoamriwa. BWANA alikusudia kuangusha ukuta uliomzunguka Binti Sayuni. Ameinyoosha kamba ya kupimia na hakuuzuia mkono wake usiangamize. Alifanya maboma na kuta ziomboleze, vyote vikaharibika pamoja. Malango yake yamezama ardhini, makomeo yake ameyavunja na kuyaharibu. Mfalme wake na wakuu wake wamepelekwa uhamishoni miongoni mwa mataifa, sheria haipo tena, na manabii wake hawapati tena maono kutoka kwa BWANA. Wazee wa Binti Sayuni wanaketi chini kimya, wamenyunyiza mavumbi kwenye vichwa vyao na kuvaa gunia. Wanawali wa Yerusalemu wameinamisha vichwa vyao hadi chini. Macho yangu yamedhoofika kwa kulia, nina maumivu makali ndani, moyo wangu umemiminwa ardhini kwa sababu watu wangu wameangamizwa, kwa sababu watoto na wanyonyao wanazimia kwenye barabara za mji. Wanawaambia mama zao, “Wapi mkate na divai?” wazimiapo kama watu waliojeruhiwa katika barabara za mji, maisha yao yadhoofikavyo mikononi mwa mama zao. Ninaweza kusema nini kwa ajili yako? Nikulinganishe na nini, ee Binti Yerusalemu? Nitakufananisha na nini, ili nipate kukufariji, ee Bikira Binti Sayuni? Jeraha lako lina kina kama bahari. Ni nani awezaye kukuponya? Maono ya manabii wako yalikuwa ya uongo na yasiyofaa kitu, hawakuifunua dhambi yako ili kukuzuilia kwenda utumwani. Maneno waliyokupa yalikuwa ya uongo na ya kupotosha. Wote wapitiao njia yako wanakupigia makofi, wanakudhihaki na kutikisa vichwa vyao kwa Binti Yerusalemu: “Huu ndio ule mji ulioitwa mkamilifu wa uzuri, furaha ya dunia yote?” Adui zako wote wanapanua vinywa vyao dhidi yako, wanadhihaki na kusaga meno yao na kusema, “Tumemmeza. Hii ndiyo siku tuliyoingojea, tumeishi na kuiona.” BWANA amefanya lile alilolipanga; ametimiza neno lake aliloliamuru siku za kale. Amekuangusha bila huruma, amewaacha adui wakusimange, ametukuza pembe ya adui yako. Mioyo ya watu inamlilia Bwana. Ee ukuta wa Binti Sayuni, machozi yako na yatiririke kama mto usiku na mchana; usijipe nafuu, macho yako yasipumzike. Inuka, lia usiku, zamu za usiku zianzapo; mimina moyo wako kama maji mbele za Bwana. Mwinulie yeye mikono yako kwa ajili ya maisha ya watoto wako, ambao wanazimia kwa njaa kwenye kila mwanzo wa barabara. “Tazama, Ee BWANA, ufikirie: Ni nani ambaye umepata kumtendea namna hii? Je, wanawake wale wazao wao, watoto waliowalea? Je, kuhani na nabii auawe mahali patakatifu pa Bwana? “Vijana na wazee hujilaza pamoja katika mavumbi ya barabarani, wasichana wangu na wavulana wangu wameanguka kwa upanga. Umewaua katika siku ya hasira yako, umewachinja bila huruma. “Kama ulivyoita siku ya karamu, ndivyo ulivyoagiza mapigo dhidi yangu kila upande. Katika siku ya hasira ya BWANA hakuna yeyote aliyekwepa au kupona; wale niliowatunza na kuwalea, adui yangu amewaangamiza.”