Maombolezo 2:7-22
Maombolezo 2:7-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu ameipuuza madhabahu yake na hekalu lake amelikataa. Kuta za majumba mjini amewaachia maadui wazibomoe, wakapiga kelele humo nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu kama kelele za wakati wa sikukuu. Mwenyezi-Mungu alipania kuubomoa ukuta wa mji wa Siyoni; aliupima na kuhakikisha kila kitu kimeharibiwa; minara na kuta za nje ya mji akazifanya ukiwa, zote kwa pamoja zikaangamia. Malango yake yameanguka chini, makomeo yake ameyaharibu na kuyavunjavunja. Mfalme na wakuu wake wako uhamishoni kati ya mataifa. Mwongozo wa sheria umetoweka kabisa, manabii wake hawapati tena maono kutoka kwake Mwenyezi-Mungu. Wazee wa Siyoni wameketi chini kimya, wamejitia mavumbi vichwani na kuvaa mavazi ya gunia. Wasichana wa Yerusalemu wameinamisha vichwa. Macho yangu yamevimba kwa kulia, roho yangu imechafuka. Moyo wangu una huzuni nyingi kwa sababu ya kuangamizwa kwa watu wangu kwa sababu watoto wachanga wanazirai katika barabara za mji. Wanawalilia mama zao: “Wapi chakula, wapi kinywaji?” Huku wanazirai kama majeruhi katika barabara za mjini, na kukata roho mikononi mwa mama zao. Nikuambie nini ee Yerusalemu? Nikulinganishe na nini? Nikufananishe na kitu gani ili niweze kukufariji, ee Siyoni uliye mzuri? Maafa yako ni mengi kama bahari. Ni nani awezaye kukuponya? Manabii wako wamekuonea maono madanganyifu, hawakufichua wazi uovu wako ili wapate kukurekebisha, bali walikuonea kauli ya uongo na ya kupotosha. Wapita njia wote wanakudhihaki; wanakuzomea, ee Yerusalemu, wakitikisa vichwa vyao kwa dharau na kusema: “Je, huu ndio ule mji uliofikia upeo wa uzuri, mji uliokuwa furaha ya dunia nzima?” Maadui zako wote wanakuzomea, wanakufyonya na kukusagia meno, huku wakisema, “Tumemwangamiza! Kweli, siku ile tuliyoingojea kwa hamu sasa imefika na tumeiona!” Mwenyezi-Mungu amefanya yale aliyokusudia, ametekeleza yale aliyotishia; kama alivyopanga tangu kale ameangamiza bila huruma yoyote; amewafanya maadui wafurahie adhabu yako, amewakuza mashujaa wa maadui zako. Kuta zako, ee mji wa Siyoni, zimlilie Mwenyezi-Mungu! Machozi na yatiririke kama mto mchana na usiku! Lia na kuomboleza bila kupumzika! Usiku kucha uamkeamke ukalie. Mfungulie Mwenyezi-Mungu yaliyo moyoni mwako. Mwinulie mikono yako kuwaombea watoto wako, watoto wanaozirai kwa njaa popote barabarani. Tazama ee Mwenyezi-Mungu uone! Je, kuna yeyote uliyemtendea ulivyotutendea sisi? Je, hata kina mama wawale watoto wao? Je, nao makuhani wauawe hekaluni mwako? Maiti za vijana na wazee zimelala vumbini barabarani, wasichana na wavulana wangu wameuawa kwa upanga; umewaua bila huruma siku ya hasira yako. Umewaalika kama kwenye sikukuu maadui zangu walionitisha kila upande. Katika siku ya hasira yako ee Mwenyezi-Mungu, hakuna aliyetoroka au kunusurika. Wale niliowazaa na kuwalea adui zangu wamewaangamiza.
Maombolezo 2:7-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Bwana ameitupilia mbali madhabahu yake, Amepachukia patakatifu pake; Amezitia katika mikono ya hao adui Kuta za majumba yake; Wamepiga kelele ndani ya nyumba ya BWANA Kama katika sikukuu. BWANA amekusudia kuuharibu Ukuta wa binti Sayuni; Ameinyosha hiyo kamba, Hakuuzuia mkono wake usiangamize; Bali amefanya boma na ukuta kuomboleza; Zote pamoja hudhoofika. Malango yake yamezama katika nchi; Ameyaharibu makomeo yake na kuyavunja; Mfalme wake na wakuu wake wanakaa Kati ya mataifa wasio na sheria; Naam, manabii wake hawapati maono Yatokayo kwa BWANA. Wazee wa binti Sayuni huketi chini, Hunyamaza kimya; Wametupa mavumbi juu ya vichwa vyao, Wamejivika viunoni nguo za magunia; Wanawali wa Yerusalemu huinama vichwa vyao Kuielekea nchi. Macho yangu yamechoka kwa machozi, Mtima wangu umetaabika; Ini langu linamiminwa juu ya nchi Kwa uharibifu wa binti ya watu wangu; Kwa sababu watoto wachanga na wanyonyao, Huzimia katika mitaa ya mji. Wao huwauliza mama zao, Ziko wapi nafaka na divai? Hapo wazimiapo kama waliojeruhiwa Katika mitaa ya mji, Hapo walipomiminika nafsi zao Vifuani mwa mama zao. Nikushuhudie nini? Nikufananishe na nini, Ee Binti Yerusalemu? Nikulinganishe na nini, nipate kukufariji, Ee bikira binti Sayuni? Kwa maana uvunjifu wako ni mkuu kama bahari, Ni nani awezaye kukuponya? Manabii wako wameona maono kwa ajili yako Ya ubatili na upumbavu Wala hawakufunua uovu wako, Wapate kurudisha kufungwa kwako; Bali wameona mabashiri ya ubatili kwa ajili yako Na sababu za kuhamishwa. Hao watu wote wapitao Hukupigia makofi; Humzomea binti Yerusalemu, Na kutikisa vichwa vyao; Je! Mji huu ndio ulioitwa, Ukamilifu wa uzuri, Furaha ya dunia yote? Juu yako adui zako wote Wamepanua vinywa vyao; Huzomea, husaga meno yao, Husema, Tumemmeza; Hakika siku hii ndiyo tuliyoitazamia; Tumeipata, tumeiona. BWANA ameyatenda aliyoyakusudia; amelitimiza neno lake, Aliloliamuru siku za kale; Ameangusha hata chini, Wala hakuona huruma; Naye amemfurahisha adui juu yako, Ameitukuza pembe ya watesi wako. Mioyo yao ilimlilia Bwana; Ee ukuta wa binti Sayuni! Machozi na yachuruzike kama mto Mchana na usiku; Usijipatie kupumzika; Mboni ya jicho lako isikome. Inuka, ulalamike usiku, Mwanzo wa mikesha yake; Mimina moyo wako kama maji usoni pa Bwana; Umwinulie mikono yako; Kwa uhai wa watoto wako wachanga wazimiao kwa njaa, Mwanzo wa kila njia kuu. Tazama, BWANA, uangalie, Ni nani uliyemtenda hayo! Je! Wanawake wale mazao yao, Watoto waliowabeba? Je! Kuhani na nabii wauawe Katika patakatifu pa Bwana? Kijana na mzee hulala chini Katika njia kuu; Wasichana wangu na wavulana wangu Wameanguka kwa upanga; Umewaua katika siku ya hasira yako; Umeua, wala hukuona huruma. Umeziita kama katika siku ya mkutano wa makini; Hofu zangu zije pande zote; Wala hapana hata mmoja aliyepona wala kusalia Katika siku ya hasira ya BWANA; Hao niliowabeba na kuwalea Huyo adui yangu amewakomesha.
Maombolezo 2:7-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Bwana ameitupilia mbali madhabahu yake, Amepachukia patakatifu pake; Amezitia katika mikono ya hao adui Kuta za majumba yake; Wamepiga kelele ndani ya nyumba ya BWANA Kama katika siku ya kusanyiko la makini. BWANA amekusudia kuuharibu Ukuta wa binti Sayuni; Ameinyosha hiyo kamba, Hakuuzuia mkono wake usiangamize; Bali amefanya boma na ukuta kuomboleza; Zote pamoja hudhoofika. Malango yake yamezama katika nchi; Ameyaharibu makomeo yake na kuyavunja; Mfalme wake na wakuu wake wanakaa Kati ya mataifa wasio na sheria; Naam, manabii wake hawapati maono Yatokayo kwa BWANA. Wazee wa binti Sayuni huketi chini, Hunyamaza kimya; Wametupa mavumbi juu ya vichwa vyao, Wamejivika viunoni nguo za magunia; Wanawali wa Yerusalemu huinama vichwa vyao Kuielekea nchi. Macho yangu yamechoka kwa machozi, Mtima wangu umetaabika; Ini langu linamiminwa juu ya nchi Kwa uharibifu wa binti ya watu wangu; Kwa sababu watoto wachanga na wanyonyao, Huzimia katika mitaa ya mji. Wao huwauliza mama zao, Zi wapi nafaka na divai? Hapo wazimiapo kama waliojeruhiwa Katika mitaa ya mji, Hapo walipomiminika nafsi zao Vifuani mwa mama zao. Nikushuhudie nini? Nikufananishe na nini, Ee Binti Yerusalemu? Nikusawazishe na nini, nipate kukufariji, Ee bikira binti Sayuni? Kwa maana uvunjifu wako ni mkuu kama bahari, Ni nani awezaye kukuponya? Manabii wako wameona maono kwa ajili yako Ya ubatili na upumbavu Wala hawakufunua uovu wako, Wapate kurudisha kufungwa kwako; Bali wameona mabashiri ya ubatili kwa ajili yako Na sababu za kuhamishwa. Hao watu wote wapitao Hukupigia makofi; Humzomea binti Yerusalemu, Na kutikisa vichwa vyao; Je! Mji huu ndio ulioitwa, Ukamilifu wa uzuri, Furaha ya dunia yote? Juu yako adui zako wote Wamepanua vinywa vyao; Huzomea, husaga meno yao, Husema, Tumemmeza; Hakika siku hii ndiyo tuliyoitazamia; Tumeipata, tumeiona. BWANA ameyatenda aliyoyakusudia; amelitimiza neno lake, Aliloliamuru siku za kale; Ameangusha hata chini, Wala hakuona huruma; Naye amemfurahisha adui juu yako, Ameitukuza pembe ya watesi wako. Mioyo yao ilimlilia Bwana; Ee ukuta wa binti Sayuni! Machozi na yachuruzike kama mto Mchana na usiku; Usijipatie kupumzika; Mboni ya jicho lako isikome. Inuka, ulalamike usiku, Mwanzo wa makesha yake; Mimina moyo wako kama maji usoni pa Bwana; Umwinulie mikono yako; Kwa uhai wa watoto wako wachanga wazimiao kwa njaa, Mwanzo wa kila njia kuu. Tazama, BWANA, uangalie, Ni nani uliyemtenda hayo! Je! Wanawake wale mazao yao, Watoto waliowabeba? Je! Kuhani na nabii wauawe Katika patakatifu pa Bwana? Kijana na mzee hulala chini Katika njia kuu; Wasichana wangu na wavulana wangu Wameanguka kwa upanga; Umewaua katika siku ya hasira yako; Umeua, wala hukuona huruma. Umeziita kama katika siku ya mkutano wa makini; Hofu zangu zije pande zote; Wala hapana hata mmoja aliyepona wala kusalia Katika siku ya hasira ya BWANA; Hao niliowabeba na kuwalea Huyo adui yangu amewakomesha.
Maombolezo 2:7-22 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Bwana amekataa madhabahu yake na kuacha mahali patakatifu pake. Amemkabidhi adui kuta za majumba yake ya kifalme; wameshangilia katika nyumba ya BWANA kama katika siku ya sikukuu iliyoamriwa. BWANA alikusudia kuangusha ukuta uliomzunguka Binti Sayuni. Ameinyoosha kamba ya kupimia na hakuuzuia mkono wake usiangamize. Alifanya maboma na kuta ziomboleze, vyote vikaharibika pamoja. Malango yake yamezama ardhini, makomeo yake ameyavunja na kuyaharibu. Mfalme wake na wakuu wake wamepelekwa uhamishoni miongoni mwa mataifa, sheria haipo tena, na manabii wake hawapati tena maono kutoka kwa BWANA. Wazee wa Binti Sayuni wanaketi chini kimya, wamenyunyiza mavumbi kwenye vichwa vyao na kuvaa gunia. Wanawali wa Yerusalemu wameinamisha vichwa vyao hadi chini. Macho yangu yamedhoofika kwa kulia, nina maumivu makali ndani, moyo wangu umemiminwa ardhini kwa sababu watu wangu wameangamizwa, kwa sababu watoto na wanyonyao wanazimia kwenye barabara za mji. Wanawaambia mama zao, “Wapi mkate na divai?” wazimiapo kama watu waliojeruhiwa katika barabara za mji, maisha yao yadhoofikavyo mikononi mwa mama zao. Ninaweza kusema nini kwa ajili yako? Nikulinganishe na nini, ee Binti Yerusalemu? Nitakufananisha na nini, ili nipate kukufariji, ee Bikira Binti Sayuni? Jeraha lako lina kina kama bahari. Ni nani awezaye kukuponya? Maono ya manabii wako yalikuwa ya uongo na yasiyofaa kitu, hawakuifunua dhambi yako ili kukuzuilia kwenda utumwani. Maneno waliyokupa yalikuwa ya uongo na ya kupotosha. Wote wapitiao njia yako wanakupigia makofi, wanakudhihaki na kutikisa vichwa vyao kwa Binti Yerusalemu: “Huu ndio ule mji ulioitwa mkamilifu wa uzuri, furaha ya dunia yote?” Adui zako wote wanapanua vinywa vyao dhidi yako, wanadhihaki na kusaga meno yao na kusema, “Tumemmeza. Hii ndiyo siku tuliyoingojea, tumeishi na kuiona.” BWANA amefanya lile alilolipanga; ametimiza neno lake aliloliamuru siku za kale. Amekuangusha bila huruma, amewaacha adui wakusimange, ametukuza pembe ya adui yako. Mioyo ya watu inamlilia Bwana. Ee ukuta wa Binti Sayuni, machozi yako na yatiririke kama mto usiku na mchana; usijipe nafuu, macho yako yasipumzike. Inuka, lia usiku, zamu za usiku zianzapo; mimina moyo wako kama maji mbele za Bwana. Mwinulie yeye mikono yako kwa ajili ya maisha ya watoto wako, ambao wanazimia kwa njaa kwenye kila mwanzo wa barabara. “Tazama, Ee BWANA, ufikirie: Ni nani ambaye umepata kumtendea namna hii? Je, wanawake wale wazao wao, watoto waliowalea? Je, kuhani na nabii auawe mahali patakatifu pa Bwana? “Vijana na wazee hujilaza pamoja katika mavumbi ya barabarani, wasichana wangu na wavulana wangu wameanguka kwa upanga. Umewaua katika siku ya hasira yako, umewachinja bila huruma. “Kama ulivyoita siku ya karamu, ndivyo ulivyoagiza mapigo dhidi yangu kila upande. Katika siku ya hasira ya BWANA hakuna yeyote aliyekwepa au kupona; wale niliowatunza na kuwalea, adui yangu amewaangamiza.”