Yoshua 9:16-27
Yoshua 9:16-27 NENO
Siku ya tatu baada ya kufanya mkataba na Wagibeoni, Waisraeli wakapata habari kuwa watu hao ni majirani zao, walioishi karibu nao. Ndipo Waisraeli wakasafiri, na siku ya tatu wakafika kwenye miji yao: yaani Gibeoni, Kefira, Beerothi na Kiriath-Yearimu. Lakini Waisraeli hawakuwashambulia kwa kuwa viongozi wa kusanyiko walikuwa wamewaapia kwa BWANA, Mungu wa Israeli. Kusanyiko lote wakanungʼunika dhidi ya hao viongozi, lakini viongozi wote wakawajibu, “Tumeshawaapia kwa BWANA, Mungu wa Israeli, kwa hiyo hatuwezi kuwagusa sasa. Hivi ndivyo tutakavyowafanyia: Tutawaacha waishi, ili ghadhabu isije juu yetu kwa kuvunja kiapo tulichowaapia.” Wakaendelea kusema, “Waacheni waishi, lakini wawe wapasua kuni na wachota maji kwa ajili ya jamii yote.” Hivyo ahadi waliyoweka viongozi kwao ikawa hivyo. Kisha Yoshua akawaita Wagibeoni na kuwaambia, “Kwa nini mmetudanganya kwa kutuambia, ‘Tunaishi mbali nanyi,’ ilhali mnaishi karibu nasi? Sasa mko chini ya laana: Daima mtakuwa wapasua kuni na wachota maji kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu.” Wakamjibu Yoshua, “Watumwa wako waliambiwa waziwazi jinsi BWANA Mungu wenu alivyomwamuru mtumishi wake Musa kuwapa ninyi nchi hii yote na kuwaangamiza wakazi wake wote toka mbele zenu. Kwa hiyo tuliogopa mno kwa ajili ya uhai wetu kwa sababu yenu, ndiyo maana tukafanya neno hili. Sasa tupo mikononi mwako. Tufanyieni lolote mnaloona kuwa jema na haki kwenu.” Kwa hiyo Yoshua akawaokoa mikononi mwa Waisraeli, nao hawakuwaua. Siku hiyo Yoshua akawafanya Wagibeoni wapasua kuni na wachota maji kwa ajili ya jamii na kwa ajili ya madhabahu ya BWANA mahali pale BWANA angepachagua. Hivyo ndivyo walivyo hadi hivi leo.