Yoshua 9:16-27
Yoshua 9:16-27 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku tatu baada ya kufanya agano nao, Waisraeli wakagundua kwamba watu hao walikuwa jirani zao na waliishi miongoni mwao. Basi, Waisraeli wakafunga safari, baada ya siku ya tatu wakafika katika miji yao. Miji hiyo ilikuwa Gibeoni, Kefira, Beerothi na Kiriath-yearimu. Lakini Waisraeli hawakuwaua, maana viongozi wa jumuiya ya Israeli walikuwa wamewaapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Hivyo basi, jumuiya yote ikawanungunikia viongozi wao. Lakini viongozi wa Waisraeli wakaiambia jumuiya ya watu wao, “Kwa vile tumewaapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, sasa hatuwezi kuwadhuru. Tutawaacha waishi, ili tusije tukaadhibiwa kwa sababu ya kiapo tulichokula. Waacheni waishi.” Hivyo Wagibeoni wakawa wanaitumikia jamii nzima ya Israeli, wakiwakatia kuni na kuwachotea maji, kama viongozi wa Waisraeli walivyosema. Yoshua akawaita Wagibeoni na kuwauliza, “Kwa nini mlitudanganya kwamba mlitoka nchi ya mbali na hali nyinyi mnaishi miongoni mwetu? Sasa, nyinyi mmelaaniwa na baadhi yenu daima mtakuwa watumwa wa kukata kuni na kuchota maji kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu.” Wakamjibu Yoshua, “Tuliambiwa kwamba kwa hakika Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alimwamuru mtumishi wake Mose awaangamize wakazi wote wa nchi hii na kuwapa nyinyi nchi hii iwe mali yenu. Kwa hivyo, tulihofia maisha yetu na ndipo tukafanya jambo hili. Sasa sisi tumo mikononi mwako, ututendee kama unavyoona inafaa.” Basi, alilowatendea ni kuwaokoa mikononi mwa Waisraeli ili wasiangamizwe; hivyo hawakuwaua. Lakini kutoka siku hiyo, Yoshua aliwafanya hao kuwa wakata-kuni na wachota-maji kwa ajili ya jumuiya nzima ya Waisraeli na kwa ajili ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu, popote pale Mwenyezi-Mungu alipochagua mpaka hivi leo.
Yoshua 9:16-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha ikawa, mwisho wa siku ya tatu baada ya kufanya hilo agano nao, walisikia habari ya kuwa watu hao ni jirani zao, na ya kwamba waliketi kati yao. Kisha wana wa Israeli walisafiri, wakaifikia miji ya watu hao siku ya tatu. Basi miji ya watu hao ilikuwa ni hii, Gibeoni, na Kefira, na Beerothi, na Kiriath-yearimu. Wana wa Israeli hawakuwapiga, kwa sababu wakuu wa mkutano walikuwa wamekwisha kuwaapia kwa BWANA, Mungu wa Israeli. Nao mkutano wote wakawanung'unikia hao wakuu. Lakini wakuu wote waliwaambia mkutano wote, Sisi tumewaapia kwa BWANA, Mungu wa Israeli; basi sasa hatuwezi kuwagusa watu hawa. Tutawafanyia neno hili, kisha tutawaacha wawe hai; hasira isije juu yetu, kwa ajili ya hicho kiapo tulichowaapia. Wakuu waliwaambia, Waacheni wawe hai; basi wakawa wenye kupasua kuni, na wenye kuteka maji, kwa ajili ya mkutano wote; vile vile kama hao wakuu walivyowaambia. Basi Yoshua akawaita, akanena nao, na kuwaambia, Mbona ninyi mmetudanganya, huku mkisema, Sisi tu mbali sana na ninyi; nanyi kumbe! Mnakaa kati yetu? Basi sasa mmelaaniwa kisha hatakosekana kuwapo mtu wa kwenu aliye mtumwa, wenye kupasua kuni, na wenye kuteka maji, kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu. Nao wakamjibu Yoshua, na kusema, Ni kwa sababu ya sisi watumishi wako kuambiwa hakika, jinsi huyo BWANA, Mungu wako alivyomwamuru mtumishi wake Musa kuwapa ninyi nchi hii yote, na kuwaangamiza wenyeji wote wa nchi hii watoke mbele zenu; kwa sababu hii tuliogopa mno kwa ajili ya uhai wetu kwa sababu yenu, nasi tumefanya neno hili. Basi sasa, tazama, sisi tu mkononi mwako; basi kama uonavyo kuwa ni vyema na haki kwako wewe kututenda, tutende hivyo. Naye akawafanyia hivyo, na kuwaokoa na mkono wa wana wa Israeli, ili wasiwaue. Siku iyo hiyo Yoshua akawafanya kuwa ni wenye kupasua kuni, na wenye kuteka maji, kwa ajili ya mkutano, na kwa ajili ya madhabahu ya BWANA, hata siku hii ya leo, katika mahali hapo atakapopachagua.
Yoshua 9:16-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha ikawa, mwisho wa siku ya tatu baada ya kufanya hilo agano nao, walisikia habari ya kuwa watu hao ni jirani zao, na ya kwamba waliketi kati yao. Kisha wana wa Israeli walisafiri, wakaifikilia miji ya watu hao siku ya tatu. Basi miji ya watu hao ilikuwa ni hii, Gibeoni, na Kefira, na Beerothi, na Kiriath-yearimu. Wana wa Israeli hawakuwapiga, kwa sababu wakuu wa mkutano walikuwa wamekwisha kuwaapia kwa BWANA, Mungu wa Israeli. Nao mkutano wote wakawanung’unikia hao wakuu. Lakini wakuu wote waliwaambia mkutano wote, Sisi tumewaapia kwa BWANA, Mungu wa Israeli; basi sasa hatuwezi kuwagusa watu hawa. Tutawafanyia neno hili, kisha tutawaacha wawe hai; hasira isije juu yetu, kwa ajili ya hicho kiapo tulichowaapia. Wakuu waliwaambia, Waacheni wawe hai; basi wakawa wenye kupasua kuni, na wenye kuteka maji, kwa ajili ya mkutano wote; vile vile kama hao wakuu walivyowaambia. Basi Yoshua akawaita, akanena nao, na kuwaambia, Mbona ninyi mmetudanganya, huku mkisema, Sisi tu mbali sana na ninyi; nanyi kumbe! Mwakaa kati yetu? Basi sasa mmelaaniwa kisha hatakosekana kuwapo mtu wa kwenu aliye mtumwa, wenye kupasua kuni, na wenye kuteka maji, kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu. Nao wakamjibu Yoshua, na kusema, Ni kwa sababu ya sisi watumishi wako kuambiwa hakika, jinsi huyo BWANA, Mungu wako alivyomwamuru mtumishi wake Musa kuwapa ninyi nchi hii yote, na kuwaangamiza wenyeji wote wa nchi hii watoke mbele zenu; kwa sababu hii tuliogopa mno kwa ajili ya uhai wetu kwa sababu yenu, nasi tumefanya neno hili. Basi sasa, tazama, sisi tu mkononi mwako; basi kama uonavyo kuwa ni vyema na haki kwako wewe kututenda, tutende vivyo. Naye akawafanyia hivyo, na kuwaokoa na mkono wa wana wa Israeli, ili wasiwaue. Siku iyo hiyo Yoshua akawafanya kuwa ni wenye kupasua kuni, na wenye kuteka maji, kwa ajili ya mkutano, na kwa ajili ya madhabahu ya BWANA, hata siku hii ya leo, katika mahali hapo atakapopachagua.
Yoshua 9:16-27 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Siku ya tatu baada ya kufanya mkataba na Wagibeoni, Waisraeli wakapata habari kuwa watu hao ni majirani zao, walioishi karibu nao. Ndipo Waisraeli wakasafiri, na siku ya tatu wakafika kwenye miji yao: yaani Gibeoni, Kefira, Beerothi na Kiriath-Yearimu. Lakini Waisraeli hawakuwashambulia kwa kuwa viongozi wa kusanyiko walikuwa wamewaapia kwa BWANA, Mungu wa Israeli. Kusanyiko lote wakanungʼunika dhidi ya hao viongozi, lakini viongozi wote wakawajibu, “Tumeshawaapia kwa BWANA, Mungu wa Israeli, kwa hiyo hatuwezi kuwagusa sasa. Hivi ndivyo tutakavyowafanyia: Tutawaacha waishi, ili ghadhabu isije juu yetu kwa kuvunja kiapo tulichowaapia.” Wakaendelea kusema, “Waacheni waishi, lakini wawe wapasua kuni na wachota maji kwa ajili ya jamii yote.” Hivyo ahadi waliyoweka viongozi kwao ikawa hivyo. Kisha Yoshua akawaita Wagibeoni na kuwaambia, “Kwa nini mmetudanganya kwa kutuambia, ‘Tunaishi mbali nanyi,’ ilhali mnaishi karibu nasi? Sasa mko chini ya laana: Daima mtakuwa wapasua kuni na wachota maji kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu.” Wakamjibu Yoshua, “Watumwa wako waliambiwa waziwazi jinsi BWANA Mungu wenu alivyomwamuru mtumishi wake Musa kuwapa ninyi nchi hii yote na kuwaangamiza wakazi wake wote toka mbele zenu. Kwa hiyo tuliogopa mno kwa ajili ya uhai wetu kwa sababu yenu, ndiyo maana tukafanya neno hili. Sasa tupo mikononi mwako. Tufanyieni lolote mnaloona kuwa jema na haki kwenu.” Kwa hiyo Yoshua akawaokoa mikononi mwa Waisraeli, nao hawakuwaua. Siku hiyo Yoshua akawafanya Wagibeoni wapasua kuni na wachota maji kwa ajili ya jamii na kwa ajili ya madhabahu ya BWANA mahali pale BWANA angepachagua. Hivyo ndivyo walivyo hadi hivi leo.