Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ayubu 1:13-21

Ayubu 1:13-21 NENO

Siku moja watoto wa Ayubu walipokuwa wakifanya karamu wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa, akaja mjumbe kwa Ayubu na kusema, “Maksai walikuwa wakilima na punda walikuwa wakilisha karibu nao, Waseba wakawashambulia na kuchukua mifugo. Kisha wakawaua watumishi kwa upanga, mimi peke yangu ndiye niliyenusurika kukuletea habari!” Alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Moto wa Mungu ulishuka kutoka mbinguni na kuteketeza kondoo na watumishi, mimi peke yangu ndiye niliyenusurika kukuletea habari!” Alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Wakaldayo waliunda vikosi vitatu vya uvamizi na kuwaangukia ngamia wako na kuwachukua wakaondoka nao. Wakawaua watumishi kwa upanga, mimi peke yangu ndiye niliyenusurika kukuletea habari.” Alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Wana wako wa kiume na wa kike walipokuwa wakifanya karamu, wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa, ghafula upepo wenye nguvu ukavuma kutoka jangwani, nao ukaipiga nyumba hiyo pembe zake nne. Ikawaangukia hao watoto nao wamekufa, mimi peke yangu ndiye niliyenusurika kukuletea habari!” Ndipo Ayubu akasimama, akararua joho lake na kunyoa nywele zake. Kisha akasujudu na kuabudu, akasema: “Nilitoka tumboni mwa mama yangu uchi, nami nitaondoka uchi, BWANA alinipa, naye BWANA ameviondoa; jina la BWANA litukuzwe.”