Yobu 1:13-21
Yobu 1:13-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Ikawa siku moja, watoto wa kiume na wa kike wa Yobu walikuwa wanakula na kunywa pamoja nyumbani kwa kaka yao mkubwa. Basi, mtumishi akafika kwa Yobu, akamwambia, “Tulikuwa tunalima kwa majembe ya kukokotwa na ng'ombe. Punda nao walikuwa wanakula hapo karibu. Basi Wasabea wakatuvamia na kuwachukua wanyama na kuwaua watumishi kwa upanga. Mimi peke yangu nimenusurika ili kuja kukuarifu.” Kabla hajamaliza kusema, mwingine akawasili, akasema, “Umeme wa radi umewachoma na kuwateketeza kondoo na watumishi, mimi tu peke yangu nimenusurika ili kuja kukuarifu.” Huyo naye kabla hajamaliza kusema, mwingine akawasili, akasema, “Wakaldayo walijipanga makundi matatu wakashambulia ngamia, wakawachukua, na kuwaua watumishi wako kwa upanga! Mimi peke yangu nimenusurika ili kuja kukuarifu.” Kabla hajamaliza kusema, akaja mwingine, akasema, “Watoto wako wa kiume na wa kike walikuwa wanakula na kunywa divai nyumbani kwa kaka yao mkubwa. Mara kimbunga kikavuma kutoka jangwani, kikaipiga nyumba hiyo kila upande nayo ikawaangukia, na vijana wote wamekufa, mimi peke yangu nimenusurika ili kuja kukuarifu.” Kisha Yobu akasimama, akararua mavazi yake, akanyoa nywele zake, akajitupa chini na kumwabudu Mungu. Akasema, “Uchi nilikuja duniani, uchi nitaondoka duniani; Mwenyezi-Mungu amenipa, Mwenyezi-Mungu amechukua; litukuzwe jina lake Mwenyezi-Mungu.”
Yobu 1:13-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ilitukia siku moja hao watoto wake wa kiume na kike walipokuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa, mjumbe akamfikia Ayubu na kumwambia, Hao ng'ombe walikuwa wakilima, na punda walikuwa wakila karibu nao; mara Waseba wakawashambulia, wakawachukua wakaenda nao; naam, wamewaua hao watumishi kwa makali ya upanga, mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Huyo alipokuwa angali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Moto wa Mungu umeanguka kutoka mbinguni na kuwateketeza kondoo, na wale watumishi, na kuwaangamiza; mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Wakaldayo walifanya vikosi vitatu, wakawaangukia ngamia, wakaenda nao, naam, wamewaua wale watumishi kwa makali ya upanga; mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Huyo alipokuwa angali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Wanao wa kiume na wa kike walikuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa; mara, tazama, upepo wenye nguvu ukatoka pande za jangwani, ukaipiga hiyo nyumba pembe zake nne, nayo ikawaangukia hao vijana, nao wamekufa; na mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Ndipo Ayubu akainuka, akalirarua joho lake, kisha akanyoa kichwa chake, na kuanguka chini, na kusujudia; akasema, Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nikiwa uchi, nami nitarudi tena huko uchi vile vile; BWANA alitoa, na BWANA ametwaa; jina la BWANA na libarikiwe.
Yobu 1:13-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ilitukia siku moja hao wanawe na binti zake walipokuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa, mjumbe akamfikilia Ayubu na kumwambia, Hao ng’ombe walikuwa wakilima, na punda walikuwa wakilisha karibu nao; mara Waseba wakawashambulia, wakawachukua wakaenda nao; naam, wamewaua hao watumishi kwa makali ya upanga, mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Moto wa Mungu umeanguka kutoka mbinguni na kuwateketeza kondoo, na wale watumishi, na kuwaangamiza; mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Wakaldayo walifanya vikosi vitatu, wakawaangukia ngamia, wakaenda nao, naam, wamewaua wale watumishi kwa makali ya upanga; mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Wanao na binti zako walikuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa; mara, tazama, upepo wenye nguvu ukatoka pande za jangwani, ukaipiga hiyo nyumba pembe zake nne, nayo ikawaangukia hao vijana, nao wamekufa; na mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari. Ndipo Ayubu akainuka, akalirarua joho lake, kisha akanyoa kichwa chake, na kuanguka chini, na kusujudia; akasema, Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami nitarudi tena huko uchi vilevile; BWANA alitoa, na BWANA ametwaa; jina la BWANA na libarikiwe.
Yobu 1:13-21 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Siku moja watoto wa Ayubu walipokuwa wakifanya karamu wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa, akaja mjumbe kwa Ayubu na kusema, “Maksai walikuwa wakilima na punda walikuwa wakilisha karibu nao, Waseba wakawashambulia na kuchukua mifugo. Kisha wakawaua watumishi kwa upanga, mimi peke yangu ndiye niliyenusurika kukuletea habari!” Alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Moto wa Mungu ulishuka kutoka mbinguni na kuteketeza kondoo na watumishi, mimi peke yangu ndiye niliyenusurika kukuletea habari!” Alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Wakaldayo waliunda vikosi vitatu vya uvamizi na kuwaangukia ngamia wako na kuwachukua wakaondoka nao. Wakawaua watumishi kwa upanga, mimi peke yangu ndiye niliyenusurika kukuletea habari.” Alipokuwa bado ananena, mjumbe mwingine akaja na kusema, “Wana wako wa kiume na wa kike walipokuwa wakifanya karamu, wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa, ghafula upepo wenye nguvu ukavuma kutoka jangwani, nao ukaipiga nyumba hiyo pembe zake nne. Ikawaangukia hao watoto nao wamekufa, mimi peke yangu ndiye niliyenusurika kukuletea habari!” Ndipo Ayubu akasimama, akararua joho lake na kunyoa nywele zake. Kisha akasujudu na kuabudu, akasema: “Nilitoka tumboni mwa mama yangu uchi, nami nitaondoka uchi, BWANA alinipa, naye BWANA ameviondoa; jina la BWANA litukuzwe.”