YouVersion Logo
Search Icon

Yohana 20:1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15, 16, 17, 18

Yohana 20:1 NENO

Alfajiri na mapema siku ya kwanza ya juma, kulipokuwa bado giza, Mariamu Magdalene alienda kaburini na kukuta lile jiwe limeondolewa penye ingilio.

Yohana 20:2 NENO

Hivyo akakimbia kwa Simoni Petro pamoja na yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, na kusema, “Wamemwondoa Bwana kaburini, na hatujui walikomweka!”

Yohana 20:3 NENO

Petro na yule mwanafunzi mwingine wakaondoka mara moja kuelekea kaburini.

Yohana 20:4 NENO

Wote wawili walikuwa wanakimbia, lakini yule mwanafunzi mwingine akakimbia mbio kuliko Petro, akatangulia kufika kaburini.

Yohana 20:5 NENO

Akainama na kuchungulia mle kaburini, akaona vile vitambaa vya kitani, lakini hakuingia.

Yohana 20:6 NENO

Ndipo Simoni Petro akaja akimfuata nyuma, akaingia ndani ya kaburi. Naye akaona vile vitambaa vya ile sanda vikiwa pale chini

Yohana 20:7 NENO

na kile kitambaa kilichokuwa kichwani mwa Yesu. Kitambaa hicho kilikuwa kimekunjwa peke yake, mbali na vile vitambaa vya kitani vya ile sanda.

Yohana 20:8 NENO

Kisha yule mwanafunzi aliyetangulia kufika kaburini akaingia ndani, akaona, na akaamini.

Yohana 20:9 NENO

(Kwa kuwa hadi wakati huo walikuwa bado hawajaelewa kutoka Maandiko kwamba ilikuwa lazima Yesu afufuke kutoka kwa wafu.)

Yohana 20:10 NENO

Kisha hao wanafunzi wakaondoka, wakarudi nyumbani mwao.

Yohana 20:11 NENO

Lakini Mariamu Magdalene akasimama nje ya kaburi akilia. Alipokuwa akilia, akainama kuchungulia mle kaburini

Yohana 20:12 NENO

naye akaona malaika wawili wamevaa mavazi meupe, wameketi pale mwili wa Yesu ulipokuwa umelazwa, mmoja upande wa kichwani na mwingine upande wa miguuni.

Yohana 20:13 NENO

Wakamuuliza Mariamu, “Mwanamke, mbona unalia?” Akawaambia, “Nalia kwa kuwa wamemchukua Bwana wangu, na sijui walikomweka.”

Yohana 20:14 NENO

Baada ya kusema hayo, akageuka, akamwona Yesu amesimama, lakini hakumtambua.

Yohana 20:15 NENO

Yesu akamwambia, “Mwanamke, mbona unalia? Unamtafuta nani?” Mariamu, akidhani alikuwa anaongea na mtunza bustani, akamwambia, “Bwana, kama ni wewe umemchukua, tafadhali nioneshe ulikomweka, nami nitamchukua.”

Yohana 20:16 NENO

Yesu akamwita, “Mariamu!” Ndipo Mariamu akamgeukia Yesu na kusema naye kwa Kiebrania, “Raboni!” (maana yake “Mwalimu”).

Yohana 20:17 NENO

Yesu akamwambia, “Usinishike, kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini nenda kwa ndugu zangu ukawaambie, ‘Ninapaa kwenda kwa Baba yangu ambaye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu ambaye ni Mungu wenu.’ ”

Yohana 20:18 NENO

Kwa hiyo Mariamu Magdalene akaenda kuwatangazia wanafunzi wa Yesu, akisema, “Nimemwona Bwana!” Naye akawaambia kwamba Yesu alikuwa amemweleza mambo hayo yote.