Yeremia 9:1-16
Yeremia 9:1-16 NENO
Laiti kichwa changu kingekuwa chemchemi ya maji na macho yangu yangekuwa kisima cha machozi! Ningelia usiku na mchana kwa kuuawa kwa watu wangu. Laiti ningekuwa na nyumba ya kukaa wasafiri jangwani, ningewaacha watu wangu na kwenda mbali nao, kwa kuwa wote ni wazinzi, kundi la watu wadanganyifu. “Huweka tayari ndimi zao kama upinde, ili kurusha uongo; wamekuwa na nguvu katika nchi lakini si katika ukweli. Wanatoka dhambi moja hadi nyingine, hawanitambui mimi,” asema BWANA. “Jihadhari na rafiki zako; usiwaamini ndugu zako. Kwa kuwa kila ndugu ni mdanganyifu, na kila rafiki ni msingiziaji. Rafiki humdanganya rafiki, hakuna yeyote asemaye kweli. Wamefundisha ndimi zao kudanganya, wanajichosha wenyewe katika kutenda dhambi. Unakaa katikati ya udanganyifu; katika udanganyifu wao wanakataa kunitambua mimi,” asema BWANA. Kwa hiyo hili ndilo asemalo BWANA wa majeshi: “Tazama, nitawasafisha na kuwajaribu, kwani ni nini kingine niwezacho kufanya kwa sababu ya dhambi ya watu wangu? Ndimi zao ni mshale wenye sumu, hunena kwa udanganyifu. Kwa kinywa chake kila mmoja huzungumza maneno mazuri na jirani yake, lakini moyoni mwake humtegea mtego. Je, nisiwaadhibu kwa ajili ya jambo hili?” asema BWANA. “Je, nisijilipizie kisasi kwa taifa kama hili?” Nitalia na kuomboleza kwa ajili ya milima na kuomboleza kuhusu malisho ya jangwani. Yamekuwa ukiwa, wala hakuna apitaye humo, milio ya ngʼombe haisikiki. Ndege wa angani wametoroka na wanyama wamekimbia. “Nitaifanya Yerusalemu lundo la magofu, makao ya mbweha; nami nitaifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa, asiwepo atakayeishi humo.” Ni mtu yupi aliye na hekima ya kutosha ayaelewe haya? Ni nani aliyefundishwa na BWANA awezaye kuyaeleza haya? Kwa nini nchi imeharibiwa na kufanywa ukiwa kama jangwa ambapo hakuna awezaye kupita? BWANA akasema, “Ni kwa sababu wameiacha sheria yangu, niliyoiweka mbele yao: hawajaniheshimu mimi wala kufuata sheria yangu. Badala yake wamefuata ukaidi wa mioyo yao, wamefuata Mabaali, kama baba zao walivyowafundisha.” Kwa hiyo, hivi ndivyo asemavyo BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli: “Tazama, nitawafanya watu hawa wale chakula kichungu na kunywa maji yenye sumu. Nitawatawanya katika mataifa ambayo wao wala baba zao hawakuyajua, nikiwafuata kwa upanga hadi niwaangamize kabisa.”