Yeremia 9:1-16
Yeremia 9:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Laiti kichwa changu kingekuwa kisima cha maji, na macho yangekuwa chemchemi ya machozi ili nipate kulia mchana na usiku, kwa ajili ya watu wangu waliouawa! Laiti ningekuwa na mahali pa kukaa jangwani, ambamo ningewaacha watu wangu na kwenda zangu.” Mwenyezi-Mungu asema: “Wote ni watu wazinzi, ni genge la watu wahaini. Hupinda maneno yao kama pinde; wameimarika kwa uongo na si kwa haki. Huendelea kutoka uovu hata uovu, wala hawanitambui mimi. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Kila mmoja ajihadhari na jirani yake! Hata ndugu yeyote haaminiki, kila ndugu ni mdanganyifu, na kila jirani ni msengenyaji. Kila mmoja humdanganya jirani yake, hakuna hata mmoja asemaye ukweli. Wamezifundisha ndimi zao kusema uongo; hutenda uovu kiasi cha kushindwa kabisa kutubu. Wanarundika dhuluma juu ya dhuluma, na udanganyifu juu ya udanganyifu. Wanakataa kunitambua mimi. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Kwa hiyo mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema: Tazama, nitawayeyusha na kuwajaribu! Au, nifanye nini zaidi na watu wangu waovu? Ndimi zao ni kama mishale yenye sumu, daima haziishi kudanganya; kila mmoja huongea vema na jirani yake, lakini moyoni mwake hupanga kumshambulia. Je, nisiwaadhibu kwa sababu ya mambo haya? Je, nisilipe kisasi kwa taifa kama hili? Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Nitaililia na kuiomboleza milima; nitayaombolezea malisho nyikani, kwa sababu yamekauka kabisa, hakuna mtu apitaye mahali hapo. Hakusikiki tena sauti za ng'ombe; ndege na wanyama wamekimbia na kutoweka. Mwenyezi-Mungu asema: “Nitaifanya Yerusalemu magofu matupu, naam, nitaifanya kuwa pango la mbweha; na miji ya Yuda nitaifanya kuwa jangwa, mahali pasipokaliwa na mtu yeyote.” Nami nikauliza, “Je kuna mtu mwenye hekima kiasi cha kuweza kueleza mambo haya? Mwenyezi-Mungu aliongea na nani hata huyo aweze kutangaza kitu hicho? Kwa nini nchi imeharibiwa na kufanywa tupu kama jangwa hata hakuna mtu apitaye humo?” Mwenyezi-Mungu akajibu: “Kwa kuwa wamekataa kushika sheria yangu niliyowapa, wamekataa kutii sauti yangu na kufuata matakwa yake. Badala yake wamefuata kwa ukaidi fikira za mioyo yao, wakaenda kuyaabudu Mabaali kama walivyofundishwa na wazee wao. Basi, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Tazama nitawalisha watu hawa uchungu na kuwapa maji yenye sumu wanywe. Nitawatawanya kati ya mataifa ambayo wao wenyewe wala wazee wao hawakupata kuyajua; nitawafanya waandamwe na vita mpaka hapo nitakapowaangamiza wote.”
Yeremia 9:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Laiti kichwa changu kingekuwa maji, na macho yangu kuwa chemchemi ya machozi, ili nipate kulia mchana na usiku kwa ajili yao waliouawa wa binti ya watu wangu! Laiti ningekuwa na mahali pa kukaa jangwani, kibanda cha wasafiri; nipate kuwaacha watu wangu, na kuondoka kwao! Maana wao ni wazinzi, wote pia, mkutano wa watu wenye hiana. Huupinda ulimi wao, kana kwamba ni upinde, ili kusema uongo; nao wamepata nguvu katika nchi, lakini si katika uaminifu; maana huendelea toka ubaya hata ubaya, wala hawanijui mimi, asema BWANA. Jihadharini, kila mtu na jirani yake, wala msimtumaini ndugu awaye yote; maana kila ndugu atachongea, na kila jirani atakwenda huku na huko na kusingizia. Nao watadanganya kila mtu jirani yake, wala hawatasema kweli; wameuzoesha ulimi wao kusema uongo; hujidhoofisha ili kutenda uovu. Makao yako ya katikati ya hadaa; kwa hadaa wanakataa kunijua mimi, asema BWANA. Basi, kwa hiyo BWANA wa majeshi asema hivi, Tazama, nitawayeyusha na kuwajaribu; maana nisipotenda hivi, nitende nini kwa ajili ya binti ya watu wangu? Ulimi wao ni mshale ufishao; husema maneno ya hadaa; mtu mmoja husema maneno ya amani na mwenzake kwa kinywa chake, lakini moyoni mwake humwotea. Je! Nisiwaadhibu kwa mambo hayo? Asema BWANA; na nafsi yangu je! Nisijilipize kisasi juu ya taifa la namna hii? Kwa milima nitalia na kulalama, Na kwa malisho ya nyikani nitafanya maombolezo; Kwa sababu yameteketea, hata hakuna apitaye, Wala hapana awezaye kusikia sauti ya ng'ombe; Ndege wa angani, na wanyama wa mwituni, Wamekimbia, wamekwenda zao. Nami nitafanya Yerusalemu kuwa magofu, Makao ya mbweha; Nami nitaifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa, Isikaliwe na mtu awaye yote. Ni nani aliye na hekima, apate kuelewa haya? Tena ni nani ambaye kinywa cha BWANA kimesema naye, apate kuyatangaza? Nayo ni nini maana yake nchi hii kuharibika, na kuteketea kama nyika, asipite mtu? Naye BWANA asema, Ni kwa sababu wameiacha sheria yangu niliyoweka mbele yao, wala hawakuitii sauti yangu, wala kuenda katika hiyo; bali wameenda katika ushupavu wa mioyo yao wenyewe, na kuandamana na Mabaali, kama walivyofundishwa na baba zao. Basi, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, nitawalisha pakanga, naam, watu hawa, nami nitawapa maji yenye sumu wayanywe. Nami nitawatawanya kati ya mataifa, ambao wao hawakuwajua; wala baba zao, nami nitatuma upanga nyuma yao, hata nitakapowaangamiza kabisa.
Yeremia 9:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Laiti kichwa changu kingekuwa maji, na macho yangu kuwa chemchemi ya machozi, ili nipate kulia mchana na usiku kwa ajili yao waliouawa wa binti ya watu wangu! Laiti ningekuwa na mahali pa kukaa jangwani, kibanda cha wasafiri; nipate kuwaacha watu wangu, na kuondoka kwao! Maana wao ni wazinzi, wote pia, mkutano wa watu wenye hiana. Huupinda ulimi wao, kana kwamba ni upinde, ili kusema uongo; nao wamepata nguvu katika nchi, lakini si katika uaminifu; maana huendelea toka ubaya hata ubaya, wala hawanijui mimi, asema BWANA. Jihadharini, kila mtu na jirani yake, wala msimtumaini ndugu awaye yote; maana kila ndugu atachongea, na kila jirani atakwenda huko na huko na kusingizia. Nao watadanganya kila mtu jirani yake, wala hawatasema kweli; wameuzoeza ulimi wao kusema uongo; hujidhoofisha ili kutenda uovu. Makao yako ya katikati ya hadaa; kwa hadaa wanakataa kunijua mimi, asema BWANA. Basi, kwa hiyo BWANA wa majeshi asema hivi, Tazama, nitawayeyusha na kuwajaribu; maana nisipotenda hivi, nitende nini kwa ajili ya binti ya watu wangu? Ulimi wao ni mshale ufishao; husema maneno ya hadaa; mtu mmoja husema maneno ya amani na mwenzake kwa kinywa chake, lakini moyoni mwake humwotea. Je! Nisiwapatilize kwa mambo hayo? Asema BWANA; na nafsi yangu je! Nisijilipize kisasi juu ya taifa la namna hii? Kwa milima nitalia na kulalama, Na kwa malisho ya nyikani nitafanya maombolezo; Kwa sababu yameteketea, hata hapana apitaye, Wala hapana awezaye kusikia sauti ya ng’ombe; Ndege wa angani, na wanyama wa mwituni, Wamekimbia, wamekwenda zao. Nami nitafanya Yerusalemu kuwa magofu, Makao ya mbweha; Nami nitaifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa, Isikaliwe na mtu awaye yote. Ni nani aliye na hekima, apate kuelewa na haya? Tena ni nani ambaye kinywa cha BWANA kimesema naye, apate kuyatangaza? Nayo ni nini maana yake nchi hii kuharibika, na kuteketea kama nyika, asipite mtu? Naye BWANA asema, Ni kwa sababu wameiacha sheria yangu niliyoweka mbele yao, wala hawakuitii sauti yangu, wala kuenenda katika hiyo; bali wameenenda katika ushupavu wa mioyo yao wenyewe, na kuandamana na Mabaali, kama walivyofundishwa na baba zao. Basi, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, nitawalisha pakanga, naam, watu hawa, nami nitawapa maji ya uchungu wayanywe. Nami nitawatawanya kati ya mataifa, ambao wao hawakuwajua; wala baba zao, nami nitatuma upanga nyuma yao, hata nitakapowaangamiza kabisa.
Yeremia 9:1-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Laiti kichwa changu kingekuwa chemchemi ya maji na macho yangu yangekuwa kisima cha machozi! Ningelia usiku na mchana kwa kuuawa kwa watu wangu. Laiti ningekuwa na nyumba ya kukaa wasafiri jangwani, ningewaacha watu wangu na kwenda mbali nao, kwa kuwa wote ni wazinzi, kundi la watu wadanganyifu. “Huweka tayari ndimi zao kama upinde, ili kurusha uongo; wamekuwa na nguvu katika nchi lakini si katika ukweli. Wanatoka dhambi moja hadi nyingine, hawanitambui mimi,” asema BWANA. “Jihadhari na rafiki zako; usiwaamini ndugu zako. Kwa kuwa kila ndugu ni mdanganyifu, na kila rafiki ni msingiziaji. Rafiki humdanganya rafiki, hakuna yeyote asemaye kweli. Wamefundisha ndimi zao kudanganya, wanajichosha wenyewe katika kutenda dhambi. Unakaa katikati ya udanganyifu; katika udanganyifu wao wanakataa kunitambua mimi,” asema BWANA. Kwa hiyo hili ndilo asemalo BWANA wa majeshi: “Tazama, nitawasafisha na kuwajaribu, kwani ni nini kingine niwezacho kufanya kwa sababu ya dhambi ya watu wangu? Ndimi zao ni mshale wenye sumu, hunena kwa udanganyifu. Kwa kinywa chake kila mmoja huzungumza maneno mazuri na jirani yake, lakini moyoni mwake humtegea mtego. Je, nisiwaadhibu kwa ajili ya jambo hili?” asema BWANA. “Je, nisijilipizie kisasi kwa taifa kama hili?” Nitalia na kuomboleza kwa ajili ya milima na kuomboleza kuhusu malisho ya jangwani. Yamekuwa ukiwa, wala hakuna apitaye humo, milio ya ngʼombe haisikiki. Ndege wa angani wametoroka na wanyama wamekimbia. “Nitaifanya Yerusalemu lundo la magofu, makao ya mbweha; nami nitaifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa, asiwepo atakayeishi humo.” Ni mtu yupi aliye na hekima ya kutosha ayaelewe haya? Ni nani aliyefundishwa na BWANA awezaye kuyaeleza haya? Kwa nini nchi imeharibiwa na kufanywa ukiwa kama jangwa ambapo hakuna awezaye kupita? BWANA akasema, “Ni kwa sababu wameiacha sheria yangu, niliyoiweka mbele yao: hawajaniheshimu mimi wala kufuata sheria yangu. Badala yake wamefuata ukaidi wa mioyo yao, wamefuata Mabaali, kama baba zao walivyowafundisha.” Kwa hiyo, hivi ndivyo asemavyo BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli: “Tazama, nitawafanya watu hawa wale chakula kichungu na kunywa maji yenye sumu. Nitawatawanya katika mataifa ambayo wao wala baba zao hawakuyajua, nikiwafuata kwa upanga hadi niwaangamize kabisa.”