Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 49:7-39

Yeremia 49:7-39 NENO

Kuhusu Edomu: Hili ndilo asemalo BWANA wa majeshi: “Je, hakuna tena hekima katika Temani? Je, shauri limewapotea wenye busara? Je, hekima yao imechakaa? Geuka na ukimbie, jifiche katika mapango marefu kabisa, wewe uishiye Dedani, kwa kuwa nitaleta maafa juu ya Esau wakati nitakapomwadhibu. Je, kama wachuma zabibu wangekuja kwako, wasingebakiza zabibu chache? Kama wezi wangekujia usiku, je, si wangeiba tu kiasi ambacho wangehitaji? Lakini nitamvua Esau nguo abaki uchi, nitayafunua maficho yake, ili asiweze kujificha. Watoto wake, jamaa na majirani wataangamia, naye hatakuwepo tena. Waache yatima wako; nitayalinda maisha yao. Wajane wako pia wanaweza kunitumaini mimi.” Hili ndilo asemalo BWANA: “Kama wasiostahili kukinywea kikombe ni lazima wakinywe, kwa nini wewe usiadhibiwe? Hutakwepa kuadhibiwa, ni lazima ukinywe. Ninaapa kwa nafsi yangu,” asema BWANA, “kwamba Bosra utakuwa magofu na kitu cha kutisha, cha aibu na cha kulaania; miji yake yote itakuwa magofu milele.” Nimesikia ujumbe kutoka kwa BWANA: Mjumbe alitumwa kwa mataifa kusema, “Jikusanyeni ili kuushambulia! Inukeni kwa ajili ya vita!” “Sasa nitakufanya mdogo miongoni mwa mataifa, uliyedharauliwa miongoni mwa watu. Vitisho vyako na kiburi cha moyo wako vimekudanganya, wewe unayeishi katika majabali ya miamba, wewe unayedumu katika miinuko ya kilima. Ujapojenga kiota chako juu sana kama cha tai, nitakushusha chini kutoka huko,” asema BWANA. “Edomu atakuwa kitu cha kutisha; wote wapitao karibu watashangaa na kuzomea kwa sababu ya majeraha yake yote. Kama vile Sodoma na Gomora zilivyoangamizwa, pamoja na miji iliyokuwa jirani nayo,” asema BWANA, “vivyo hivyo hakuna mtu yeyote atakayeishi humo. Naam, hakuna mtu yeyote atakayekaa humo. “Kama simba anayepanda kutoka vichaka vya Yordani kuja kwenye nchi ya malisho mengi, ndivyo nitakavyomfukuza Edomu kutoka nchi yake ghafula. Ni nani aliye mteule nitakayemweka kwa ajili ya jambo hili? Ni nani aliye kama mimi, na ni nani awezaye kunipinga? Tena ni mchungaji yupi awezaye kusimama kinyume nami?” Kwa hiyo, sikia kile BWANA alichokipanga dhidi ya Edomu, kile alichokusudia dhidi ya wale wanaoishi Temani: Aliye mchanga katika kundi ataburutwa mbali; yeye ataharibu kabisa malisho yao kwa sababu yao. Kwa sauti ya anguko lao, dunia itatetemeka. Kilio chao kitasikika hadi Bahari ya Shamu. Tazama! Tai atapaa juu angani na kuruka chini kwa ghafula, akitandaza mabawa yake juu ya Bosra. Katika siku hiyo, mioyo ya mashujaa wa Edomu itakuwa kama moyo wa mwanamke katika uchungu wa kuzaa. Kuhusu Dameski: “Hamathi na Arpadi imetahayarika, kwa kuwa wamesikia habari mbaya. Wamevunjika moyo na wametaabika kama bahari iliyochafuka. Dameski amedhoofika, amegeuka na kukimbia, hofu ya ghafula imemkamata sana; amepatwa na uchungu na maumivu, maumivu kama ya mwanamke katika uchungu wa kuzaa. Kwa nini mji unaosifika haujaachwa, mji wenye sifa, na wa furaha yangu? Hakika, vijana wake wanaume wataanguka barabarani; askari wake wote watanyamazishwa siku hiyo,” asema BWANA wa majeshi. “Nitatia moto kuta za Dameski; utaangamiza ngome za Ben-Hadadi.” Kuhusu Kedari na falme za Hazori, ambazo Nebukadneza mfalme wa Babeli alizishambulia: Hili ndilo asemalo BWANA: “Inuka, ushambulie Kedari na kuwaangamiza watu wa mashariki. Mahema yao na makundi yao ya kondoo yatachukuliwa; vibanda vyao vitatwaliwa, pamoja na mali yao yote na ngamia wao. Watu watawapigia kelele, ‘Hofu kuu iko kila upande!’ “Kimbieni haraka! Kaeni kwenye mapango marefu sana, ninyi mnaoishi Hazori,” asema BWANA. “Nebukadneza, mfalme wa Babeli amepanga njama dhidi yenu; amebuni hila dhidi yenu. “Inuka na ulishambulie taifa lililostarehe, linaloishi kwa kujiamini,” asema BWANA, “taifa lisilo na malango wala makomeo; watu wake wanaishi peke yao. Ngamia wao watakuwa nyara, nayo mifugo yao itatekwa. Walio maeneo ya mbali nitawatawanya pande zote, nami nitaleta maafa juu yao kutoka kila upande,” asema BWANA. “Hazori itakuwa makao ya mbweha, mahali pa ukiwa milele. Hakuna atakayeishi humo; hakuna mtu atakayekaa ndani yake.” Hili ndilo neno la BWANA lililomjia nabii Yeremia kuhusu Elamu, mapema katika utawala wa Sedekia mfalme wa Yuda: Hili ndilo asemalo BWANA wa majeshi: “Tazama, nitavunja upinde wa Elamu, ulio tegemeo la nguvu zao. Nitaleta pepo nne dhidi ya Elamu toka pande nne za mbingu, nitawatawanya katika hizo pande nne, wala hapatakuwa na taifa ambalo watu wa Elamu waliofukuzwa hawataenda. Nitamfadhaisha Elamu mbele ya adui zao, mbele yao wanaoutafuta uhai wao; nitaleta maafa juu yao, naam, hasira yangu kali,” asema BWANA. “Nitawafuatia kwa upanga hadi nitakapowamaliza. Nitaweka kiti changu cha enzi huko Elamu na kumwangamiza mfalme wake na maafisa wake,” asema BWANA. “Lakini nitarudisha mateka wa Elamu katika siku zijazo,” asema BWANA.