Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 49:7-39

Yeremia 49:7-39 Biblia Habari Njema (BHN)

Kuhusu Edomu. Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Je, hakuna tena hekima mjini Temani? Je, wenye busara wao hawana shauri tena? Hekima imetoweka kabisa? Kimbieni enyi wakazi wa Dedani; geukeni mkaishi mafichoni! Maana nitawaleteeni maangamizi enyi wazawa wa Esau; wakati wa kuwaadhibu umefika. Wachuma zabibu watakapokuja kwenu hawatabakiza hata zabibu moja. Usiku ule wezi watakapofika, wataharibu kila kitu mpaka watosheke. Lakini nimemnyanganya Esau kila kitu, naam, nimeyafunua maficho yake, wala hawezi kujificha tena. Watoto, ndugu na jirani zake wameangamizwa; hakuna hata mmoja aliyebaki. Niachieni watoto wenu yatima nami nitawatunza; waacheni wajane wenu wanitegemee.” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Ikiwa wale ambao hawakustahili kunywa kikombe cha adhabu ni lazima wanywe, je, wewe utaachwa bila kuadhibiwa? La! Hutakosa kuadhibiwa; ni lazima unywe hicho kikombe! Maana nimeapa kwa nafsi yangu kwamba mji wa Bosra utakuwa kioja na kichekesho, utakuwa uharibifu na laana; vijiji vyote vitakuwa magofu daima. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.” Nimepata habari kutoka kwa Mwenyezi-Mungu, mjumbe ametumwa ayatangazie mataifa: “Jikusanyeni pamoja dhidi ya Edomu; inukeni mwende kuushambulia! Mimi Mwenyezi-Mungu nitakufanya wee Edomu kuwa mdogo kuliko mataifa yote. Ulimwengu wote utakudharau. Vitisho unavyotoa na kiburi chako vimekudanganya, ewe ukaaye katika mapango ya miamba, unayeishi juu ya kilele cha mlima! Ingawa unaweka makao yako juu kama ya tai, mimi nitakuporomosha kutoka huko uliko. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. “Edomu itakuwa kitisho na kila mtu atakayepita karibu yake atashangaa, na kuizomea kwa sababu ya maafa yatakayoipata. Kama vile Sodoma na Gomora na miji jirani yake ilivyoangamizwa, mimi Mwenyezi-Mungu nasema, hakutakuwa na mtu yeyote atakayeishi Edomu wala kufanya mashauri humo. Kama vile simba anavyochomoza kutoka msitu wa mto Yordani na kuingia kwenye malisho mazuri, ndivyo nitakavyowafukuza ghafla Waedomu kutoka nchi yao. Nami nitamweka huko kiongozi yeyote nitakayemchagua. Maana, ni nani anayeweza kulinganishwa nami? Nani awezaye kunishtaki? Ni mchungaji gani awezaye kunipinga? Kwa hiyo, sikilizeni mpango ambao mimi Mwenyezi-Mungu nimepanga dhidi ya Edomu pamoja na mambo niliyokusudia kuwafanyia wakazi wa Temani: Hakika, watoto wao wadogo wataburutwa na kuchukuliwa; kweli kutakuwa na mshangao mkubwa katika makao yao! Kwa kishindo cha kuanguka kwao, dunia itatetemeka; sauti ya kilio chao itasikika mpaka bahari ya Shamu. Tazama, adui atapanda juu na kuruka kama tai na kutandaza mabawa yake juu ya Bosra. Siku hiyo moyo wa mashujaa wa Edomu utakumbwa na hofu kama ya mwanamke anayejifungua.” Kuhusu Damasko: “Miji ya Hamathi na Arpadi, imejaa wasiwasi kwa kufikiwa na habari mbaya; mioyo ya watu wake inayeyuka kwa hofu, imefadhaika kama bahari isiyoweza kutulia. Watu wa Damasko wamekufa moyo; wamegeuka wapate kukimbia; hofu kubwa imewakumba, uchungu na huzuni vimewapata, kama mwanamke anayejifungua Ajabu kuachwa kwa mji maarufu, mji uliokuwa umejaa furaha! Basi vijana wake wataanguka viwanjani mwake, askari wake wote wataangamizwa siku hiyo. Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema. Nitawasha moto katika kuta za Damasko, nao utateketeza ngome za mfalme Ben-hadadi.” Kuhusu Kedari na falme za Hazori ambazo Nebukadneza mfalme wa Babuloni, alizishambulia na kuzishinda, Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Inuka uende kulishambulia kabila la Kedari! Waangamize watu wa mashariki! Hema zao na kondoo wao vitachukuliwa, kadhalika mapazia yao na mali yao yote; watanyanganywa ngamia wao, na kilio kitasikika: ‘Kitisho kila upande!’ Kimbieni, nendeni mbali, kaeni mashimoni. Enyi wakazi wa Haziri, kimbieni mtangetange na kukaa mafichoni! Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Maana Nebukadneza mfalme wa Babuloni, amefanya mpango dhidi yenu, amepania kuja kuwashambulia. Inuka uende kulishambulia taifa linalostarehe, taifa linaloishi kwa usalama. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Taifa hilo halina malango wala pao za chuma; ni taifa ambalo liko peke yake. “Ngamia wao watatekwa mifugo yao itachukuliwa mateka. Nitawatawanya kila upande, watu wale wanaonyoa denge. Nitawaletea maafa kutoka kila upande. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Mji wa Hazori utakuwa makao ya mbweha, utakuwa jangwa daima; hakuna mtu atakayekaa humo, wala atakayeishi humo.” Neno la Mwenyezi-Mungu lililomjia nabii Yeremia kuhusu Elamu, mwanzoni mwa utawala wa Sedekia, mfalme wa Yuda. Mwenyezi-Mungu wa majeshi, asema hivi: “Nitavunja upinde wa watu wa Elamu ulio msingi wa nguvu zao. Nitaleta upepo kutoka pande zote za mbingu; nitawatawanya kila mahali, wala hapatakuwa na taifa lolote ambalo halitakuwa na wakimbizi wa Elamu. Nitawafadhaisha watu wa Elamu mbele ya maadui zao na mbele ya wale wanaotaka kuyaangamiza maisha yao. Nitawaletea maafa na hasira yangu kali. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Nitawaletea upanga kuwafuata mpaka niwaangamize kabisa. Nitaweka kiti changu cha enzi huko Elamu na kumwangamiza mfalme wao pamoja na wakuu wao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Lakini katika siku za mwisho, nitaurudishia mji wa Elamu fanaka yake. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

Shirikisha
Soma Yeremia 49

Yeremia 49:7-39 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kuhusu Edomu. BWANA wa majeshi asema hivi, Je! Hakuna tena hekima katika Temani? Mashauri yamewapotea wenye busara? Je! Imetoweka hekima yao? Kimbieni, rudini nyuma, kaeni chini sana, enyi mnaokaa Dedani; maana nitaleta msiba wa Esau juu yake, wakati nitakapomwangalia. Je! Kama wachuma zabibu wangekujia, wasingeacha zabibu ziokotwe? Kama wangekujia wezi usiku, wasingeharibu hata watakapopata vya kutosha? Lakini nimemwacha akiwa hana kitu Esau, nimepafunua mahali pake pa siri, wala hataweza kujificha; kizazi chake kimeangamizwa, na ndugu zake, na jirani zake, naye mwenyewe hayuko. Waache watoto wako wasio na baba, mimi nitawahifadhi hai, na wajane wako na wanitumaini mimi. Maana BWANA asema hivi, Tazama, wale wasioandaliwa kunywea kikombe, watakinywea, ni hakika; na wewe je! U mtu ambaye hataadhibiwa kabisa? Hukosi utaadhibiwa, naam, kunywa utakunywa. Kwa maana nimeapa kwa nafsi yangu, asema BWANA, kwamba Bozra utakuwa ajabu, na aibu, na ukiwa, na laana; na miji yake yote itakuwa ukiwa wa daima. Nimepata habari kwa BWANA, Na mjumbe ametumwa kati ya mataifa, Akisema, Jikusanyeni, mkaujie, Mkainuke kwenda vitani. Maana nimekufanya mdogo kati ya mataifa, Na kudharauliwa katika watu. Kuhusu kuogofya kwako, Kiburi cha moyo wako kimekudanganya, Wewe ukaaye katika pango za majabali, Ushikaye kilele cha milima; Ujapofanya kiota chako juu sana kama tai, Nitakushusha kutoka huko; asema BWANA. Na Edomu atakuwa ajabu; kila mtu apitaye atashangaa, na kuzomea, kwa sababu ya mapigo yake yote. Kama vile vilivyotokea wakati wa kuangushwa Sodoma na Gomora, na miji iliyokuwa karibu nayo, asema BWANA; hapana mtu atakayekaa huko, wala hapana mwanadamu atakayekaa huko kama mgeni akaavyo. Angalia, atapanda kama simba toka kiburi cha Yordani juu ya malisho yasiyonyauka; lakini nitamkimbiza ghafla ayaache; na yeye aliye mteule nitamweka juu yake; maana ni nani aliye kama mimi? Tena ni nani atakayeniandikia muda? Tena ni mchungaji yupi atakayesimama mbele zangu? Basi, lisikieni shauri la BWANA; Alilolifanya juu ya Edomu; Na makusudi yake aliyoyakusudia Juu yao wakaao Temani; Hakika watawaburura, naam, wadogo wa kundi; Hakika malisho yao yatafadhaika kwa ajili yao. Nchi yatetemeka kwa sauti ya kuanguka kwao; Kuna kilio, sauti yake yasikiwa katika Bahari ya Shamu. Tazama, atapanda na kuruka kama tai, na kutandaza mabawa yake juu ya Bozra; na mioyo ya mashujaa wa Edomu siku hiyo itakuwa kama moyo wa mwanamke akiwa katika uchungu wa kujifungua. Kuhusu Dameski. Hamathi umetahayarika, na Arpadi pia; Maana wamesikia habari mbaya; Wameyeyuka kabisa; Wamesumbuka kama bahari, isiyoweza kutulia. Dameski umedhoofika; Umejigeuza kukimbia; tetemeko limeushika; Dhiki na huzuni zimeupata, Kama za mwanamke katika uchungu wake. Imekuwaje mji wa sifa haukuachwa, mji wa furaha yangu? Kwa hiyo vijana wake wataanguka katika njia zake kuu, na watu wote wa vita watanyamazishwa katika siku hiyo, asema BWANA wa majeshi. Nami nitawasha moto katika ukuta wa Dameski, nao utayateketeza majumba ya Ben-hadadi. Kuhusu Kedari, na falme za Hazori, ambazo Nebukadneza, mfalme wa Babeli, alizipiga. BWANA asema hivi, Ondokeni, pandeni hadi Kedari, mkawateke nyara wana wa mashariki. Hema zao na makundi yao watayatwaa; watachukulia mbali mapazia yao kwa faida yao wenyewe, na vyombo vyao vyote, na ngamia wao; nao watawapigia kelele wakisema, Hofu ziko pande zote. Kimbieni ninyi, nendeni mbali mkitangatanga, kaeni chini sana, enyi mkaao Hazori, asema BWANA; maana Nebukadneza, mfalme wa Babeli, amefanya shauri juu yenu, naye amekusudia neno juu yenu. Ondokeni, pandeni hata taifa lililo katika hali ya raha, likaalo bila kuhangaika, asema BWANA; wasio na malango wala makomeo, wakaao peke yao. Na ngamia wao watakuwa mateka, na wingi wa makundi yao utakuwa nyara; nami nitawatawanya katika pande zote watu wale wanyoao denge; nami nitaleta msiba wao toka pande zao zote, asema BWANA. Na Hazori utakuwa kao la mbwamwitu; ukiwa milele; hakuna mtu atakayekaa huko, wala hakuna mwanadamu atakayekaa huko kama mgeni akaavyo. Neno la BWANA lililomjia Yeremia, nabii, juu ya Elamu, mwanzo wa kumiliki kwake Sedekia, mfalme wa Yuda, kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, Tazama nitauvunja upinde wa Elamu, ulio mkuu katika nguvu zao. Na juu ya Elamu nitazileta pepo nne, toka pembe nne za mbinguni, nami nitawatawanya katika pande zote nne, wala hakuna taifa ambalo hawatalifikia watu wa Elamu waliofukuzwa. Nami nitawafadhaisha watu wa Elamu mbele ya adui zao, na mbele ya hao wanaowatafuta roho zao; nami nitawaletea mabaya, naam, hasira yangu kali, asema BWANA; nami nitautuma upanga uwafuatie, hadi nitakapowaangamiza; nami nitaweka kiti changu cha enzi huko Elamu, nami nitawaharibu, mfalme na wakuu, watoke huko, asema BWANA. Lakini itakuwa, katika siku za mwisho, nitawarudisha wafungwa wa Elamu, asema BWANA.

Shirikisha
Soma Yeremia 49

Yeremia 49:7-39 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Habari za Edomu. BWANA wa majeshi asema hivi, Je! Hapana tena hekima katika Temani? Mashauri yamewapotea wenye busara? Je! Imetoweka hekima yao? Kimbieni, rudini nyuma, kaeni chini sana, enyi mnaokaa Dedani; maana nitaleta msiba wa Esau juu yake, wakati nitakapomwangalia. Je! Kama wachuma zabibu wangekujia, wasingeacha zabibu ziokotwe? Kama wangekujia wevi usiku, wasingeharibu hata watakapopata vya kutosha? Lakini nimemwacha Esau hana kitu, nimepafunua mahali pake pa siri, wala hataweza kujificha; kizazi chake kimeangamizwa, na ndugu zake, na jirani zake, naye mwenyewe hayuko. Waache watoto wako wasio na baba, mimi nitawahifadhi hai, na wajane wako na wanitumaini mimi. Maana BWANA asema hivi, Tazama, wale wasioandikiwa kunywea kikombe, watakinywea, ni hakika; na wewe je! U mtu ambaye hataadhibiwa kabisa? Hukosi utaadhibiwa, naam, kunywa utakunywa. Kwa maana nimeapa kwa nafsi yangu, asema BWANA, kwamba Bozra utakuwa ajabu, na aibu, na ukiwa, na laana; na miji yake yote itakuwa ukiwa wa daima. Nimepata habari kwa BWANA, Na mjumbe ametumwa kati ya mataifa, Akisema, Jikusanyeni, mkaujie, Mkainuke kwenda vitani. Maana nimekufanya mdogo kati ya mataifa, Na kudharauliwa katika watu. Katika habari za kuogofya kwako, Kiburi cha moyo wako kimekudanganya, Wewe ukaaye katika pango za majabali, Ushikaye kilele cha milima; Ujapofanya kioto chako juu sana kama tai, Nitakushusha kutoka huko; asema BWANA. Na Edomu atakuwa ajabu; kila mtu apitaye atashangaa, na kuzomea, kwa sababu ya mapigo yake yote. Kama vile vilivyotokea wakati wa kuangushwa Sodoma na Gomora, na miji iliyokuwa karibu nayo, asema BWANA; hapana mtu atakayekaa huko, wala hapana mwanadamu atakayekaa huko kama mgeni akaavyo. Angalia, atapanda kama simba toka kiburi cha Yordani juu ya malisho yasiyonyauka; lakini nitamkimbiza ghafula ayaache; na yeye aliye mteule nitamweka juu yake; maana ni nani aliye kama mimi? Tena ni nani atakayeniandikia muda? Tena ni mchungaji yupi atakayesimama mbele zangu? Basi, lisikieni shauri la BWANA; Alilolifanya juu ya Edomu; Na makusudi yake aliyoyakusudia Juu yao wakaao Temani; Hakika watawaburura, naam, wadogo wa kundi; Hakika malisho yao yatafadhaika kwa ajili yao. Nchi yatetemeka kwa sauti ya kuanguka kwao; Kuna kilio, sauti yake yasikiwa katika Bahari ya Shamu. Tazama, atapanda na kuruka kama tai, na kutandaza mabawa yake juu ya Bozra; na mioyo ya mashujaa wa Edomu siku hiyo itakuwa kama moyo wa mwanamke katika utungu wake. Habari za Dameski. Hamathi umetahayarika, na Arpadi pia; Maana wamesikia habari mbaya; Wameyeyuka kabisa; Huzuni iko baharini, haiwezi kutulia. Dameski umedhoofika; Umejigeuza kukimbia; tetemko limeushika; Dhiki na huzuni zimeupata, Kama za mwanamke katika utungu wake. Imekuwaje mji wa sifa haukuachwa, mji wa furaha yangu? Kwa hiyo vijana wake wataanguka katika njia kuu zake, na watu wote wa vita watanyamazishwa katika siku hiyo, asema BWANA wa majeshi. Nami nitawasha moto katika ukuta wa Dameski, nao utayateketeza majumba ya Ben-hadadi. Habari za Kedari, na za falme za Hazori, ambazo Nebukadreza, mfalme wa Babeli, alizipiga. BWANA asema hivi, Ondokeni, pandeni hata Kedari, mkawateke nyara wana wa mashariki. Hema zao na makundi yao watayatwaa; watachukulia mbali mapazia yao kwa faida yao wenyewe, na vyombo vyao vyote, na ngamia zao; nao watawapigia kelele wakisema, Hofu ziko pande zote. Kimbieni ninyi, enendeni mbali mkitanga-tanga, kaeni chini sana, enyi mkaao Hazori, asema BWANA; maana Nebukadreza, mfalme wa Babeli, amefanya shauri juu yenu, naye amekusudia neno juu yenu. Ondokeni, pandeni hata taifa lililo katika hali ya raha, likaalo bila kuhangaika, asema BWANA; wasio na malango wala makomeo, wakaao peke yao. Na ngamia zao watakuwa mateka, na wingi wa makundi yao utakuwa nyara; nami nitawatawanya hata pepo zote watu wale wanyoao denge; nami nitaleta msiba wao toka pande zao zote, asema BWANA. Na Hazori utakuwa kao la mbwa-mwitu; ukiwa milele; hapana mtu atakayekaa huko, wala hapana mwanadamu atakayekaa huko kama mgeni akaavyo. Neno la BWANA lililomjia Yeremia, nabii, juu ya Elamu, mwanzo wa kumiliki kwake Sedekia, mfalme wa Yuda, kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, Tazama nitauvunja upinde wa Elamu, ulio mkuu katika nguvu zao. Na juu ya Elamu nitazileta pepo nne, toka pembe nne za mbinguni, nami nitawatawanya hata pepo nne zote, wala hapana taifa ambalo hawatalifikilia watu wa Elamu waliofukuzwa. Nami nitawafadhaisha watu wa Elamu mbele ya adui zao, na mbele ya hao wanaowatafuta roho zao; nami nitawaletea mabaya, naam, hasira yangu kali, asema BWANA; nami nitautuma upanga uwafuatie, hata nitakapowaangamiza; nami nitaweka kiti changu cha enzi huko Elamu, nami nitawaharibu, mfalme na wakuu, watoke huko, asema BWANA. Lakini itakuwa, katika siku za mwisho, nitawarudisha wafungwa wa Elamu, asema BWANA.

Shirikisha
Soma Yeremia 49

Yeremia 49:7-39 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Kuhusu Edomu: Hili ndilo asemalo BWANA wa majeshi: “Je, hakuna tena hekima katika Temani? Je, shauri limewapotea wenye busara? Je, hekima yao imechakaa? Geuka na ukimbie, jifiche katika mapango marefu kabisa, wewe uishiye Dedani, kwa kuwa nitaleta maafa juu ya Esau wakati nitakapomwadhibu. Je, kama wachuma zabibu wangekuja kwako, wasingebakiza zabibu chache? Kama wezi wangekujia usiku, je, si wangeiba tu kiasi ambacho wangehitaji? Lakini nitamvua Esau nguo abaki uchi, nitayafunua maficho yake, ili asiweze kujificha. Watoto wake, jamaa na majirani wataangamia, naye hatakuwepo tena. Waache yatima wako; nitayalinda maisha yao. Wajane wako pia wanaweza kunitumaini mimi.” Hili ndilo asemalo BWANA: “Kama wasiostahili kukinywea kikombe ni lazima wakinywe, kwa nini wewe usiadhibiwe? Hutakwepa kuadhibiwa, ni lazima ukinywe. Ninaapa kwa nafsi yangu,” asema BWANA, “kwamba Bosra utakuwa magofu na kitu cha kutisha, cha aibu na cha kulaania; miji yake yote itakuwa magofu milele.” Nimesikia ujumbe kutoka kwa BWANA: Mjumbe alitumwa kwa mataifa kusema, “Jikusanyeni ili kuushambulia! Inukeni kwa ajili ya vita!” “Sasa nitakufanya mdogo miongoni mwa mataifa, uliyedharauliwa miongoni mwa watu. Vitisho vyako na kiburi cha moyo wako vimekudanganya, wewe unayeishi katika majabali ya miamba, wewe unayedumu katika miinuko ya kilima. Ujapojenga kiota chako juu sana kama cha tai, nitakushusha chini kutoka huko,” asema BWANA. “Edomu atakuwa kitu cha kutisha; wote wapitao karibu watashangaa na kuzomea kwa sababu ya majeraha yake yote. Kama vile Sodoma na Gomora zilivyoangamizwa, pamoja na miji iliyokuwa jirani nayo,” asema BWANA, “vivyo hivyo hakuna mtu yeyote atakayeishi humo. Naam, hakuna mtu yeyote atakayekaa humo. “Kama simba anayepanda kutoka vichaka vya Yordani kuja kwenye nchi ya malisho mengi, ndivyo nitakavyomfukuza Edomu kutoka nchi yake ghafula. Ni nani aliye mteule nitakayemweka kwa ajili ya jambo hili? Ni nani aliye kama mimi, na ni nani awezaye kunipinga? Tena ni mchungaji yupi awezaye kusimama kinyume nami?” Kwa hiyo, sikia kile BWANA alichokipanga dhidi ya Edomu, kile alichokusudia dhidi ya wale wanaoishi Temani: Aliye mchanga katika kundi ataburutwa mbali; yeye ataharibu kabisa malisho yao kwa sababu yao. Kwa sauti ya anguko lao, dunia itatetemeka. Kilio chao kitasikika hadi Bahari ya Shamu. Tazama! Tai atapaa juu angani na kuruka chini kwa ghafula, akitandaza mabawa yake juu ya Bosra. Katika siku hiyo, mioyo ya mashujaa wa Edomu itakuwa kama moyo wa mwanamke katika uchungu wa kuzaa. Kuhusu Dameski: “Hamathi na Arpadi imetahayarika, kwa kuwa wamesikia habari mbaya. Wamevunjika moyo na wametaabika kama bahari iliyochafuka. Dameski amedhoofika, amegeuka na kukimbia, hofu ya ghafula imemkamata sana; amepatwa na uchungu na maumivu, maumivu kama ya mwanamke katika uchungu wa kuzaa. Kwa nini mji unaosifika haujaachwa, mji wenye sifa, na wa furaha yangu? Hakika, vijana wake wanaume wataanguka barabarani; askari wake wote watanyamazishwa siku hiyo,” asema BWANA wa majeshi. “Nitatia moto kuta za Dameski; utaangamiza ngome za Ben-Hadadi.” Kuhusu Kedari na falme za Hazori, ambazo Nebukadneza mfalme wa Babeli alizishambulia: Hili ndilo asemalo BWANA: “Inuka, ushambulie Kedari na kuwaangamiza watu wa mashariki. Mahema yao na makundi yao ya kondoo yatachukuliwa; vibanda vyao vitatwaliwa, pamoja na mali yao yote na ngamia wao. Watu watawapigia kelele, ‘Hofu kuu iko kila upande!’ “Kimbieni haraka! Kaeni kwenye mapango marefu sana, ninyi mnaoishi Hazori,” asema BWANA. “Nebukadneza, mfalme wa Babeli amepanga njama dhidi yenu; amebuni hila dhidi yenu. “Inuka na ulishambulie taifa lililostarehe, linaloishi kwa kujiamini,” asema BWANA, “taifa lisilo na malango wala makomeo; watu wake wanaishi peke yao. Ngamia wao watakuwa nyara, nayo mifugo yao itatekwa. Walio maeneo ya mbali nitawatawanya pande zote, nami nitaleta maafa juu yao kutoka kila upande,” asema BWANA. “Hazori itakuwa makao ya mbweha, mahali pa ukiwa milele. Hakuna atakayeishi humo; hakuna mtu atakayekaa ndani yake.” Hili ndilo neno la BWANA lililomjia nabii Yeremia kuhusu Elamu, mapema katika utawala wa Sedekia mfalme wa Yuda: Hili ndilo asemalo BWANA wa majeshi: “Tazama, nitavunja upinde wa Elamu, ulio tegemeo la nguvu zao. Nitaleta pepo nne dhidi ya Elamu toka pande nne za mbingu, nitawatawanya katika hizo pande nne, wala hapatakuwa na taifa ambalo watu wa Elamu waliofukuzwa hawataenda. Nitamfadhaisha Elamu mbele ya adui zao, mbele yao wanaoutafuta uhai wao; nitaleta maafa juu yao, naam, hasira yangu kali,” asema BWANA. “Nitawafuatia kwa upanga hadi nitakapowamaliza. Nitaweka kiti changu cha enzi huko Elamu na kumwangamiza mfalme wake na maafisa wake,” asema BWANA. “Lakini nitarudisha mateka wa Elamu katika siku zijazo,” asema BWANA.

Shirikisha
Soma Yeremia 49