Yeremia 40:1-6
Yeremia 40:1-6 NENO
Neno likamjia Yeremia kutoka kwa BWANA baada ya Nebuzaradani mkuu wa askari walinzi wa mfalme kumfungua huko Rama. Alikuwa amemkuta Yeremia akiwa amefungwa kwa minyororo miongoni mwa mateka wote kutoka Yerusalemu na Yuda waliokuwa wakipelekwa uhamishoni Babeli. Mkuu wa askari walinzi alipomwona Yeremia, akamwambia, “BWANA Mungu wako aliamuru maafa haya kutokea mahali hapa. Sasa BWANA ameyaleta haya, amefanya sawasawa na alivyosema angefanya. Yote haya yametokea kwa sababu ninyi mlifanya dhambi dhidi ya BWANA na hamkumtii. Lakini leo ninakufungua minyororo iliyo kwenye viwiko vya mikono yako. Ukiona ni vema, twende pamoja hadi Babeli; nami nitakutunza. Lakini kama hutaki, basi usije. Tazama, nchi yote iko mbele yako, nenda kokote unakotaka.” Lakini kabla Yeremia hajageuka kuondoka, Nebuzaradani akaongeza kusema, “Rudi kwa Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani, ambaye mfalme wa Babeli amemchagua awe juu ya miji ya Yuda, ukaishi naye miongoni mwa watu, au uende popote panapokupendeza.” Kisha huyo kiongozi akampa posho yake na zawadi, akamwacha aende zake. Kwa hiyo Yeremia akaenda kwa Gedalia mwana wa Ahikamu huko Mispa, na kuishi naye miongoni mwa watu walioachwa katika nchi.