Yeremia 40:1-6
Yeremia 40:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi-Mungu wakati Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, alipomruhusu Yeremia aondoke Rama. Huyo kapteni alimchukua Yeremia amefungwa minyororo, akawachukua pia pamoja naye mateka wengine wote wa Yerusalemu na Yuda ambao walikuwa wamepelekwa uhamishoni Babuloni. Kapteni wa walinzi alimchukua Yeremia, akamwambia “Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, alitangaza maafa dhidi ya mahali hapa. Na sasa Mwenyezi-Mungu ametekeleza jambo hilo na kutenda kama alivyosema, kwa sababu nyinyi nyote mlimkosea Mwenyezi-Mungu na kukataa kumtii, jambo hilo limewapata. Haya! Leo nazifungua pingu mikononi mwako. Kama unaona ni vema kwenda pamoja nami mpaka Babuloni, basi twende pamoja; mimi nitakutunza vizuri. Lakini kama unaona si vizuri kwako kwenda pamoja nami mpaka Babuloni, basi, usije. Ujue kwamba waweza kwenda popote katika nchi hii; basi nenda popote unapoamua kuwa pazuri kwenda. Kama ukiamua kubaki, basi rudi kwa Gedalia mwana wa Ahikamu, mjukuu wa Shafani, ambaye mfalme wa Babuloni amemteua kuwa mtawala wa miji yote ya Yuda, ukakae naye miongoni mwa wananchi wengine. La sivyo, nenda popote unapoona ni sawa kwenda.” Basi, kapteni wa walinzi akampa Yeremia masurufu na zawadi, kisha akamwacha aende zake. Kisha Yeremia akaenda Mizpa kwa Gedalia mwana wa Ahikamu, akakaa naye pamoja na wananchi waliobaki nchini.
Yeremia 40:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, baada ya wakati ule Nebuzaradani, mkuu wa askari walinzi, alipomwacha aende zake toka Rama, baada ya kumchukua akiwa amefungwa minyororo, pamoja na wafungwa wote wa Yerusalemu na Yuda, waliochukuliwa wakiwa wamefungwa mpaka Babeli. Naye mkuu wa askari walinzi akamtwaa Yeremia, akamwambia, BWANA, Mungu wako, alitamka mabaya haya juu ya mahali hapa; naye BWANA ameyaleta, na kufanya kama alivyosema; kwa sababu mmemwasi BWANA, wala hamkuitii sauti yake; ndiyo maana neno hili limewajia ninyi. Na sasa, tazama, nakufungulia leo minyororo hii iliyo mikononi mwako. Kama ukiona ni vema kwenda Babeli pamoja nami, haya! Njoo, nami nitakutunza sana; lakini kama ukiona ni vibaya kwenda Babeli pamoja nami, basi, acha; tazama, nchi yote iko mbele yako; palipo pema machoni pako na pa kukufaa, nenda huko. Alipokuwa bado hajaenda, akasema, Rudi sasa kwa Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, ambaye mfalme wa Babeli amemweka kuwa mtawala juu ya miji ya Yuda, ukakae pamoja naye kati ya watu; au nenda popote utakapoona mwenyewe kuwa pakufaa. Basi, mkuu wa askari walinzi akampa vyakula na zawadi, akamwacha aende zake. Basi, Yeremia akaenda kwa Gedalia, mwana wa Ahikamu, huko Mizpa, akakaa pamoja naye kati ya watu wale waliosalia katika nchi.
Yeremia 40:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa BWANA, baada ya wakati ule Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, alipomwacha aende zake toka Rama, baada ya kumchukua hali ya kufungwa minyororo, pamoja na wafungwa wote wa Yerusalemu na Yuda, waliochukuliwa hali ya kufungwa mpaka Babeli. Naye amiri wa askari walinzi akamtwaa Yeremia, akamwambia, BWANA, Mungu wako, alitamka mabaya haya juu ya mahali hapa; naye BWANA ameyaleta, na kufanya kama alivyosema; kwa sababu mmemwasi BWANA, wala hamkuitii sauti yake; ndiyo maana neno hili limewajia ninyi. Na sasa, tazama, nakufungulia leo minyororo hii iliyo mikononi mwako. Kama ukiona ni vema kwenda Babeli pamoja nami, haya! Njoo, nami nitakutunza sana; lakini kama ukiona ni vibaya kwenda Babeli pamoja nami, basi, acha; tazama, nchi yote i mbele yako; palipo pema machoni pako na pa kukufaa, enenda huko. Alipokuwa bado hajaenda, akasema, Rudi sasa kwa Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, ambaye mfalme wa Babeli amemweka kuwa liwali juu ya miji ya Yuda, ukakae pamoja naye kati ya watu; au enenda po pote utakapoona mwenyewe kuwa pakufaa. Basi, amiri wa askari walinzi akampa vyakula na zawadi, akamwacha aende zake. Basi, Yeremia akaenda kwa Gedalia, mwana wa Ahikamu, huko Mizpa, akakaa pamoja naye kati ya watu wale waliosalia katika nchi.
Yeremia 40:1-6 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Neno likamjia Yeremia kutoka kwa BWANA baada ya Nebuzaradani mkuu wa askari walinzi wa mfalme kumfungua huko Rama. Alikuwa amemkuta Yeremia akiwa amefungwa kwa minyororo miongoni mwa mateka wote kutoka Yerusalemu na Yuda waliokuwa wakipelekwa uhamishoni Babeli. Mkuu wa askari walinzi alipomwona Yeremia, akamwambia, “BWANA Mungu wako aliamuru maafa haya kutokea mahali hapa. Sasa BWANA ameyaleta haya, amefanya sawasawa na alivyosema angefanya. Yote haya yametokea kwa sababu ninyi mlifanya dhambi dhidi ya BWANA na hamkumtii. Lakini leo ninakufungua minyororo iliyo kwenye viwiko vya mikono yako. Ukiona ni vema, twende pamoja hadi Babeli; nami nitakutunza. Lakini kama hutaki, basi usije. Tazama, nchi yote iko mbele yako, nenda kokote unakotaka.” Lakini kabla Yeremia hajageuka kuondoka, Nebuzaradani akaongeza kusema, “Rudi kwa Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani, ambaye mfalme wa Babeli amemchagua awe juu ya miji ya Yuda, ukaishi naye miongoni mwa watu, au uende popote panapokupendeza.” Kisha huyo kiongozi akampa posho yake na zawadi, akamwacha aende zake. Kwa hiyo Yeremia akaenda kwa Gedalia mwana wa Ahikamu huko Mispa, na kuishi naye miongoni mwa watu walioachwa katika nchi.