Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 31:1-14

Yeremia 31:1-14 NEN

“Wakati huo, nitakuwa Mungu wa koo zote za Israeli nao watakuwa watu wangu,” asema BWANA. Hili ndilo asemalo BWANA: “Watu watakaopona upanga watapata upendeleo jangwani; nitakuja niwape Israeli pumziko.” BWANA alitutokea wakati uliopita, akisema: “Nimekupenda kwa upendo wa milele, nimekuvuta kwa wema. Nitakujenga tena nawe utajengeka upya, ewe Bikira Israeli. Utachukua tena matari yako na kwenda kucheza na wenye furaha. Utapanda tena shamba la mizabibu juu ya vilima vya Samaria, wakulima watapanda na kufurahia matunda yake. Itakuja siku wakati walinzi watakapowapigia kelele juu ya vilima vya Efraimu wakisema, ‘Njooni, twendeni juu Sayuni, kwake BWANA Mungu wetu.’ ” Hili ndilo asemalo BWANA: “Mwimbieni Yakobo kwa furaha, mpigieni kelele aliye mkuu wa mataifa. Zifanyeni sifa zenu zisikike, nanyi mseme, ‘Ee BWANA, okoa watu wako, mabaki ya Israeli.’ Tazama, nitawaleta kutoka nchi ya kaskazini na kuwakusanya kutoka miisho ya dunia. Miongoni mwao watakuwepo vipofu na viwete, mama wajawazito na wenye utungu wa kuzaa. Umati mkubwa wa watu utarudi. Watakuja wakilia; wataomba wakati ninawarudisha. Nitawaongoza kando ya vijito vya maji katika mapito yaliyo tambarare ambapo hawatajikwaa, kwa sababu mimi ndimi baba wa Israeli, naye Efraimu ni mzaliwa wangu wa kwanza. “Sikieni neno la BWANA, enyi mataifa, litangazeni katika nchi za pwani ya mbali: ‘Yeye aliyewatawanya Israeli atawakusanya na atalichunga kundi lake la kondoo kama mchungaji.’ Kwa kuwa BWANA atamlipia fidia Yakobo na kuwakomboa mkononi mwa walio na nguvu kuliko wao. Watakuja na kupiga kelele kwa furaha katika miinuko ya Sayuni; watashangilia ukarimu wa BWANA: nafaka, divai mpya na mafuta, wana-kondoo wachanga na ndama wa makundi ya ngʼombe nitakaowapa. Watakuwa kama bustani iliyonyeshewa vizuri, wala hawatahuzunika tena. Kisha wanawali watacheza na kufurahi, vijana waume na wazee pia. Nitageuza maombolezo yao kuwa furaha, nitawapa faraja na furaha badala ya huzuni. Nitawashibisha makuhani kwa wingi, nao watu wangu watajazwa kwa ukarimu wangu,” asema BWANA.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha