Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Isaya 1:1-9

Isaya 1:1-9 NENO

Maono kuhusu Yuda na Yerusalemu ambayo Isaya mwana wa Amozi aliyaona wakati wa utawala wa Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda. Sikieni, enyi mbingu! Sikilizeni, enyi dunia! Kwa maana BWANA amesema: “Nimewalisha watoto na kuwalea, lakini wameniasi mimi. Ngʼombe anamjua bwana wake, naye punda anajua hori la mmiliki wake, lakini Israeli hajui, watu wangu hawaelewi.” Ole wa taifa lenye dhambi, watu waliolemewa na uovu, uzao wa watenda mabaya, watoto waliozoelea upotovu! Wamemwacha BWANA, Wamemkataa kwa dharau yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli na kumgeuzia kisogo. Kwa nini mzidi kupigwa? Kwa nini kudumu katika uasi? Kichwa chako chote kimejeruhiwa, moyo wako wote ni mgonjwa. Kutoka wayo wako wa mguu hadi kwenye utosi wa kichwa chako hakuna uzima: ni majeraha matupu na makovu na vidonda vinavyotoa damu, havikusafishwa au kufungwa wala kulainishwa kwa mafuta. Nchi yenu imekuwa ukiwa, miji yenu imeteketezwa kwa moto; mashamba yenu yameachwa tupu na wageni mbele ya macho yenu, yameharibiwa kama yaliyopinduliwa na wageni. Binti Sayuni ameachwa kama kipenu katika shamba la mizabibu, kama kibanda katika shamba la matango, kama mji uliozingirwa. Kama BWANA wa majeshi hakutuachia walionusurika, tungekuwa kama Sodoma, tungefanana na Gomora.