Isaya 1:1-9
Isaya 1:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Maono aliyoyaona Isaya, mwana wa Amozi, kuhusu Yuda na mji wa Yerusalemu, nyakati za utawala wa Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Sikilizeni enyi mbingu, tega sikio ee dunia. Mimi nimewalea wanangu wakakua, lakini sasa wameniasi! Ngombe humfahamu mwenyewe, punda hujua kibanda cha bwana wake; lakini Waisraeli hawajui, watu wangu, hawaelewi!” Ole wako wewe taifa lenye dhambi, watu waliolemewa na uovu, wazawa wa wenye kutenda maovu, watu waishio kwa udanganyifu! Nyinyi mmemwacha Mwenyezi-Mungu, mmemdharau Mtakatifu wa Israeli, mmefarakana naye na kurudi nyuma. Kwa nini huachi uasi wako? Mbona wataka kuadhibiwa bado? Kichwa chote ni majeraha matupu, na moyo wote unaugua! Toka wayo hadi kichwa hamna penye nafuu, umejaa majeraha na vidonda vitoavyo damu, navyo havikuoshwa, kufungwa wala kutiwa mafuta. Nchi yenu imeharibiwa kabisa; miji yenu imeteketezwa kwa moto. Wageni wananyakua nchi yenu mkiona kwa macho, imeharibiwa kama uharibifu wa Sodoma. Mji Siyoni umeachwa kama kibanda shambani, kama kitalu katika shamba la matango, kama mji uliozingirwa. Mwenyezi-Mungu wa majeshi asingalituachia wachache, tungalikwisha kuwa kama watu wa Sodoma, tungalikuwa hali ileile ya Gomora.
Isaya 1:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Haya ni maono ya Isaya, mwana wa Amozi aliyoyaona kuhusu Yuda na Yerusalemu, siku za Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda. Sikieni, enyi mbingu, tega sikio, Ee nchi, kwa maana BWANA amenena; Nimewalisha watoto na kuwalea, nao wameniasi. Ng'ombe amjua bwana wake, Na punda ajua kibanda cha bwana wake; Bali Israeli hajui, watu wangu hawafikiri. Ole wake, taifa lenye dhambi, watu wanaochukua mzigo wa uovu, wazao wa watenda mabaya, watoto wanaoharibu; wamemwacha BWANA, wamemdharau yeye aliye Mtakatifu wa Israeli, wamefarakana naye na kurudi nyuma. Mbona mnataka kupigwa, hata sasa, hata mkazidi kuasi? Kichwa chote ni kigonjwa, moyo wote umezimia. Toka wayo wa mguu hadi kichwani hamna uzima ndani yake; bali jeraha na machubuko na vidonda vitokavyo usaha; havikufungwa, havikuzongwazongwa, wala havikulainishwa kwa mafuta. Nchi yenu ni ukiwa; miji yenu imeteketezwa kwa moto; nchi yenu, wageni wameila mbele ya macho yenu; nayo ni ukiwa, kana kwamba imeangamizwa na wageni. Na binti Sayuni ameachwa kama kibanda katika shamba la mizabibu, kama kipenu katika shamba la matango, kama mji uliohusuriwa. Kama BWANA wa majeshi asingalituachia mabaki machache sana, tungalikuwa kama Sodoma, tungalifanana na Gomora.
Isaya 1:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Haya ni maono ya Isaya, mwana wa Amozi, aliyoyaona katika habari za Yuda na Yerusalemu, siku za Uzia na Yothamu na Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda. Sikieni, enyi mbingu, tega sikio, Ee nchi, kwa maana BWANA amenena; Nimewalisha watoto na kuwalea, nao wameniasi. Ng’ombe amjua bwana wake, Na punda ajua kibanda cha bwana wake; Bali Israeli hajui, watu wangu hawafikiri. Ole wake, taifa lenye dhambi, watu wanaochukua mzigo wa uovu, wazao wa watenda mabaya, watoto wanaoharibu; wamemwacha BWANA, wamemdharau yeye aliye Mtakatifu wa Israeli, wamefarakana naye na kurudi nyuma. Mbona mnataka kupigwa hata sasa, hata mkazidi kuasi? Kichwa chote ni kigonjwa, moyo wote umezimia. Tangu wayo wa mguu hata kichwani hamna uzima ndani yake; bali jeraha na machubuko na vidonda vitokavyo usaha; havikufungwa, havikuzongwa-zongwa, wala havikulainishwa kwa mafuta. Nchi yenu ni ukiwa; miji yenu imeteketezwa kwa moto; nchi yenu, wageni wameila mbele ya macho yenu; nayo ni ukiwa, kana kwamba imeangamizwa na wageni. Na binti Sayuni ameachwa kama kibanda katika shamba la mizabibu, kama kipenu katika shamba la matango, kama mji uliohusuriwa. Kama BWANA wa majeshi asingalituachia mabaki machache sana, tungalikuwa kama Sodoma, tungalifanana na Gomora.
Isaya 1:1-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Maono kuhusu Yuda na Yerusalemu ambayo Isaya mwana wa Amozi aliyaona wakati wa utawala wa Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda. Sikieni, enyi mbingu! Sikilizeni, enyi dunia! Kwa maana BWANA amesema: “Nimewalisha watoto na kuwalea, lakini wameniasi mimi. Ngʼombe anamjua bwana wake, naye punda anajua hori la mmiliki wake, lakini Israeli hajui, watu wangu hawaelewi.” Ole wa taifa lenye dhambi, watu waliolemewa na uovu, uzao wa watenda mabaya, watoto waliozoelea upotovu! Wamemwacha BWANA, Wamemkataa kwa dharau yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli na kumgeuzia kisogo. Kwa nini mzidi kupigwa? Kwa nini kudumu katika uasi? Kichwa chako chote kimejeruhiwa, moyo wako wote ni mgonjwa. Kutoka wayo wako wa mguu hadi kwenye utosi wa kichwa chako hakuna uzima: ni majeraha matupu na makovu na vidonda vinavyotoa damu, havikusafishwa au kufungwa wala kulainishwa kwa mafuta. Nchi yenu imekuwa ukiwa, miji yenu imeteketezwa kwa moto; mashamba yenu yameachwa tupu na wageni mbele ya macho yenu, yameharibiwa kama yaliyopinduliwa na wageni. Binti Sayuni ameachwa kama kipenu katika shamba la mizabibu, kama kibanda katika shamba la matango, kama mji uliozingirwa. Kama BWANA wa majeshi hakutuachia walionusurika, tungekuwa kama Sodoma, tungefanana na Gomora.