Hosea 5:5-15
Hosea 5:5-15 NENO
Kiburi cha Israeli kinashuhudia dhidi yao; Waisraeli, hata Efraimu, wanajikwaa katika dhambi zao; pia Yuda atajikwaa pamoja nao. Wanapoenda na makundi yao ya kondoo na ngʼombe kumtafuta BWANA, hawatampata; yeye amejiondoa kutoka kwao. Wao si waaminifu kwa BWANA; wamezaa watoto haramu. Sasa sikukuu zao za Mwandamo wa Mwezi zitawaangamiza wao pamoja na mashamba yao. “Pigeni tarumbeta huko Gibea, na baragumu huko Rama. Pazeni kelele za vita huko Beth-Aveni; ongoza, ee Benyamini. Efraimu ataachwa ukiwa katika siku ya kuadhibiwa. Miongoni mwa makabila ya Israeli ninatangaza lile ambalo halina budi kutukia. Viongozi wa Yuda ni kama wale wanaosogeza mawe ya mpaka. Nitamwaga ghadhabu yangu juu yao kama mafuriko ya maji. Efraimu amedhulumiwa, amekanyagwa katika hukumu kwa kuwa amekusudia kufuatia sanamu. Mimi ni kama nondo kwa Efraimu, na kama uozo kwa watu wa Yuda. “Efraimu alipoona ugonjwa wake, naye Yuda vidonda vyake, ndipo Efraimu aligeukia Ashuru, na kuomba msaada kwa mfalme mkuu. Lakini hawezi kukuponya, hawezi kukuponya vidonda vyako. Kwa maana nitakuwa kama simba kwa Efraimu, kama simba mkubwa kwa Yuda. Nitawararua vipande vipande na kuondoka; nitawachukua mbali, na hakuna wa kuwaokoa. Kisha nitarudi mahali pangu hadi watakapokubali kosa lao. Nao watautafuta uso wangu; katika taabu yao watanitafuta kwa bidii.”