Wagalatia 5:7-26
Wagalatia 5:7-26 NENO
Mlikuwa mkipiga mbio vizuri. Ni nani aliyewazuia msiitii kweli? Ushawishi kama huo haukutoka kwa yule anayewaita. “Chachu kidogo huchachua donge zima.” Nina hakika katika Bwana kwamba hamtakuwa na msimamo mwingine. Mtu anayewachanganya anastahili adhabu, hata awe nani. Lakini ndugu zangu, kama mimi bado ninahubiri kuhusu kutahiriwa, kwa nini bado ninateswa? Katika hiyo hali basi, kwazo la msalaba limeondolewa. Laiti hao wanaowavuruga wangejihasi wao wenyewe! Ndugu zangu, ninyi mliitwa ili mwe huru, hivyo msitumie uhuru wenu kama fursa ya kufuata tamaa za mwili, bali tumikianeni ninyi kwa ninyi kwa upendo. Kwa maana sheria yote hukamilika katika amri moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.” Lakini mkiumana na kutafunana, angalieni msije mkaangamizana. Kwa hiyo nasema, nendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa maana mwili hutamani yale yaliyo kinyume na Roho, naye Roho hutamani yale yaliyo kinyume na mwili. Roho na mwili hupingana na kwa sababu hiyo hamwezi kufanya mnayotaka. Lakini mkiongozwa na Roho, hamko chini ya sheria. Basi matendo ya mwili ni dhahiri, nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi, kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi ufalme wa Mungu. Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria. Wote walio wa Kristo Yesu wameusulubisha mwili na shauku zake pamoja na tamaa zake. Kwa kuwa tunaishi kwa Roho, basi, tuenende kwa Roho. Tusijisifu bure, tukichokozana na kuoneana wivu.