Kutoka 33:1-6
Kutoka 33:1-6 NENO
Kisha BWANA akamwambia Musa, “Ondoka mahali hapa, wewe pamoja na hao watu uliowapandisha kutoka Misri, mpande hadi nchi niliyomwahidi Abrahamu, Isaka na Yakobo kwa kiapo, nikisema, ‘Nitawapa wazao wenu nchi hii.’ Nitamtuma malaika mbele yenu, naye atawafukuza Wakanaani, Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. Pandeni mwende katika nchi inayotiririka maziwa na asali. Lakini mimi sitaenda pamoja nanyi, kwa sababu ninyi ni watu wenye shingo ngumu, nisije nikawaangamiza njiani.” Watu waliposikia habari hizo za huzuni, wakaanza kuomboleza wala hakuna mtu aliyevaa mapambo yoyote. Kwa kuwa BWANA alikuwa amemwambia Musa, “Waambie Waisraeli, ‘Ninyi ni watu wenye shingo ngumu. Kama ningefuatana nanyi hata kwa muda mfupi, ningewaangamiza. Sasa vueni mapambo yenu, nami nitaamua nitakalowatendea.’ ” Hivyo Waisraeli wakavua mapambo yao katika Mlima Horebu.