Kutoka 33:1-6
Kutoka 33:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Anza safari uondoke hapa, wewe na watu hao uliowatoa nchini Misri, mwende katika nchi niliyomwapia Abrahamu, Isaka na Yakobo, nikisema, ‘Nitawapa wazawa wenu nchi hii’. Nitamtuma malaika awaongoze; nitawafukuza Wakaanani, Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. Nendeni katika nchi hiyo inayotiririka maziwa na asali. Lakini kwa sababu nyinyi ni wenye vichwa vigumu sitakwenda pamoja nanyi, nisije nikawaangamiza njiani.” Watu walilia waliposikia habari hizi mbaya; wala hakuna aliyevaa mapambo yake. Walifanya hivyo kwani Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwambia Mose, “Waambie Waisraeli, ‘Nyinyi ni watu wenye vichwa vigumu; nikienda pamoja nanyi kwa muda mfupi tu, nitawaangamiza. Hivyo vueni mapambo yenu ili nijue namna ya kuwatendea.’” Basi, Waisraeli waliyavua mapambo yao tangu walipoondoka mlimani Horebu.
Kutoka 33:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akanena na Musa, Haya, ondokeni, katokeni hapo, wewe na hao watu uliowaleta wakwee kutoka nchi ya Misri, waende nchi hiyo niliyomwapia Abrahamu, na Isaka, na Yakobo, niliposema, Nitakipa kizazi chako nchi hii; nami nitamtuma malaika aende mbele yako; nami nitawafukuza Mkanaani, na Mwamori, na Mhiti, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi; waifikie nchi imiminikayo maziwa na asali; kwa maana mimi sitakwenda kati yenu; kwa sababu ninyi ni watu wenye shingo ngumu; nisiwaangamize ninyi katika njia. Watu waliposikia habari hizo mbaya wakaomboleza wala hakuna mtu aliyevaa mapambo yake. BWANA akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli, Ninyi ni watu wenye shingo ngumu; kama mimi nikiingia kati yenu dakika moja, nitawaangamiza; basi sasa vueni mapambo yenu ili nipate kujua nitakalowatenda. Basi wana wa Israeli wakavua mapambo yao, tangu mlima wa Horebu na mbele.
Kutoka 33:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akanena na Musa, Haya, ondokeni, katokeni hapo, wewe na hao watu uliowaleta wakwee kutoka nchi ya Misri, waende nchi hiyo niliyomwapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, niliposema, Nitakipa kizazi chako nchi hii; nami nitamtuma malaika aende mbele yako; nami nitawafukuza Mkanaani, na Mwamori, na Mhiti, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi; waifikilie nchi imiminikayo maziwa na asali; kwa maana mimi sitakwenda kati yenu; kwa sababu ninyi ni watu wenye shingo ngumu; nisiwaangamize ninyi katika njia. Watu waliposikia habari hizo mbaya wakaomboleza wala hapana mtu aliyevaa vyombo vyake vya uzuri. BWANA akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli, Ninyi ni watu wenye shingo ngumu; kama mimi nikiingia kati yenu dakika moja, nitawaangamiza; basi sasa vueni vyombo vyenu vya uzuri ili nipate kujua nitakalowatenda. Basi wana wa Israeli wakavua vyombo vyao vyote vya uzuri, tangu mlima wa Horebu na mbele.
Kutoka 33:1-6 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kisha BWANA akamwambia Musa, “Ondoka mahali hapa, wewe pamoja na hao watu uliowapandisha kutoka Misri, mpande hadi nchi niliyomwahidi Abrahamu, Isaka na Yakobo kwa kiapo, nikisema, ‘Nitawapa wazao wenu nchi hii.’ Nitamtuma malaika mbele yenu, naye atawafukuza Wakanaani, Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. Pandeni mwende katika nchi inayotiririka maziwa na asali. Lakini mimi sitaenda pamoja nanyi, kwa sababu ninyi ni watu wenye shingo ngumu, nisije nikawaangamiza njiani.” Watu waliposikia habari hizo za huzuni, wakaanza kuomboleza wala hakuna mtu aliyevaa mapambo yoyote. Kwa kuwa BWANA alikuwa amemwambia Musa, “Waambie Waisraeli, ‘Ninyi ni watu wenye shingo ngumu. Kama ningefuatana nanyi hata kwa muda mfupi, ningewaangamiza. Sasa vueni mapambo yenu, nami nitaamua nitakalowatendea.’ ” Hivyo Waisraeli wakavua mapambo yao katika Mlima Horebu.